Katika sehemu ya kusini ya China, karibu na mji wa Shanghai ukisasfiri kwa gari kwa muda wa saa mbili hivi utafika kwenye mji mmoja mdogo unaoitwa Nantong. Siku chache zilizopita wakuu wa majumba ya makumbusho zaidi ya 130 kutoka nchini China na nchi za nje walikusanyika katika mji huo kuadhimisha miaka mia moja tokea jumba la makumbusho la kwanza lianzishwe nchini China. Mwenyekiti wa Shirikisho la Kimataifa la Majumba ya Makubusho Bi. Alissandra Cummins aliyetoka makao makuu ya UNESCO mjini Paris pia alihudhuria maadhimisho hayo.
Mwaka 1905 ni mwaka unaostahili kukumbukwa katika historia ya China. Wakati huo China ilikuwa chini ya mfalme wa Enzi ya Qing. Tokea vita vya kasumba mwaka 1840, Enzi ya Qing ililazimika kusaini mikataba mingi isiyo ya usawa chini ya nguvu za kijeshi za nchi za Magharibi, China ikawa nchi nusu koloni na nusu nchi ya umwinyi. Katika kipindi hicho tajiri mmoja mwanamke aliyeitwa Zhang Jian alijaribu kuliokoa taifa la China kwa kustawisha elimu, mwaka 1905 alianzisha jumba la makumbusho lililokuwa la kwanza kabisa nchini China katika mji wa Nantong. Bi. Chen Dongyun ambaye ni mkuu wa sasa wa jumba hilo la makumbusho, alisema, usanifu wa jumba hilo la makumbusho ulikuwa ni wa busara, hadi sasa haujapitiwa na wakati. Alisema, "Hapo awali jumba hilo lilikuwa na kumbi tatu, yaani ukumbi wa historia, ukumbi wa sanaa na ukumbi wa historia ya maumbile. Licha ya kumbi hizo pia kulikuwa na makumbusho uani, ambako kulikuwa na maonesho ya mimea na wanyama walio hai. Jumba hilo la makumbusho lilikuwa na nia ya kusaidia elimu ya shuleni, uenezi wa sayansi kwa umma, na kuwapatia watu mahali pa kuburudika."
Majumba ya makumbusho nchini China yana historia ndefu, lakini aina mpya ya majumba ya makukmbusho ilitokea kama aina mpya ya shule kulingana na jinsi jamii inavyoendelea. Mwaka 1682, jumba la makumbusho ya sanaa na vitu vya kale katika Chuo Kikuu cha Oxford lilifunguliwa kwa watu wote. Hili ni jumba la makumbusho la kwanza kabisa kuwepo duniani. Katikati ya karne ya 19, fikra za nchi za Magharibi za kuyafanya makumbusho yawe ya kuhifadhi utamaduni pamoja na kueneza elimu, zilipokelewa na wasomi wenye mawazo ya kimaendeleo wa China, kuanzisha majumba ya makumbusho kulikuwa ni hatua zao muhimu za "kuwaelimisha wananchi" wa China.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Kimataifa la Majumba ya Makumbusho Bi. Alissandra Cummins baada ya kuangalia jumba la makumbusho la Nantong alisifu na kusema, "Ingawa jumba hili lilijengwa mwanzoni mwa karne iliyopita, lakini mkazo wake wa kuunganisha shughuli za utafiti na hifadhi ya vitu vya utamaduni kwa pamoja ulikuwa mapema kuliko nchi za Magharibi ambazo zilianza katika miaka ya 30 ya karne iliyopita. Kwa hiyo jumba hili ni mfano kwa sehemu nyingine."
Kutokana na data, mwanzoni wa karne ya 20, yalikuwepo majumba 70 ya makumbusho nchini China, lakini katika miaka ya 30 hadi 40, vita vya uvamizi wa Japan nchini China viliharibu vibaya majumba hayo na utamaduni wa China. Mwaka 1949 Jamhuri ya Watu wa China ilipoanzishwa, kulikuwa na majumba 25 tu ya makumbusho yaliyosalia, mojawapo likiwa ni jumba la makumbusho la mji wa Nantong. Mkuu wa sasa wa jumba la makumbusho la Nantong Bi. Wang Dongyun alisema, jeshi la Japan lilikalia jumba hilo, vitu vyote kwenye jumba la makumbusho viliporwa, hasara ilikuwa kubwa, hali ya makumbusho ilikuwa mbaya kama ilivyokuwa hali ya taifa la China. Alisema, "Jumba la Makumbusho mjini Nantong liliwahi kukumbwa na matatizo mengi. Katika miaka ya Bw. Zhang Jian kazi ya makumbusho ilikuwa nzuri kutokana na msaada wake, lakini baada ya yeye kufariki, na hasa katika miaka ya vita vya uvamizi wa Japan, jumba hilo lilitumika kama makao makuu ya jeshi la Japan, na vitu vya utamaduni pia viliporwa na askari wa Japan."
Baada ya Jamhuri ya Watu wa China kuasisiwa, serikali ilitambua umuhimu wa jumba la makumbusho la Nantong kutokana na kuwepo kwake kwa miaka mingi, jumba hilo lilikarabatiwa, na vitu vya makumbusho viliongezeka mwaka hadi mwaka. Kabla ya maadhimisho ya miaka mia moja ya jumba hilo, serikali ya Nantong ilitenga fedha nyingi na kujenga majumba mengine ya makumbusho mjini kuonesha historia ya maendeleo ya mambo mbalimbali katika mji huo.
Hali ya maendeleo ya majumba ya makumbusho mjini Nantong ni kama kielelezo cha maendeleo ya majumba ya makumbusho nchini China. Katika miaka ya karibuni, serikali ya China imeongeza nguvu katika kuimarisha utamaduni. Jumba la Makumbusho la Taifa limekuwa likipanuliwa sasa, na baada ya kukamilisha eneo la jumba hilo la taifa litakuwa kubwa mara mbili kuliko zamani, katika miji mingine ya Shanghai, Xi'an na Zhengzhou majumba mengi ya makumbusho ya kisasa yamejengwa. Katika mji mdogo wa Nantong hivi sasa yamejengwa majumba 23 yakionesha sanaa, michezo na maendeleo ya mji. Kwa wastani kila wakazi elfu 50 wana jumba moja la makumbusho. Mkuu wa Jumba la Makumbusho la Taifa Bw. Shan Jixiang alieleza kwa furaha?"Katika muda wa karne moja iliyopita, mambo ya makumbusho nchini China yamepata maendeleo makubwa. Hivi sasa kuna majumba ya makumbusho 2300 yenye vitu vya kuhifadhiwa milioni 20 na kutembelewa na watazamaji milioni 150 kila mwaka, na jumba la kwanza la makumbusho lililoanzishwa na Bi. Zhang Jian limetoa mchango mkubwa katika maendeleo hayo."
China ni nchi kubwa kwa eneo na kwa idadi ya watu, hali ya uchumi katika sehemu za mashariki, katikati na magharibi inatofautiana sana, tofauti hiyo ya uchumi imesababisha maendeleo tofauti ya utamaduni. Mwenyekiti wa Shirikisho la Majumba ya Makumbusho la China Bw. Zhang Wenbin alisema, serikali za mikoa kwenye sehemu ya mashariki na pwani zina uwezo wa kuendeleza huduma za umma zikiwa ni pamoja na mambo ya makumbusho, lakini katika sehemu zilizo nyuma kiuchumi uwezo ni mdogo. Alisema, "Kwa ujumla mambo ya makumbusho yameendelea haraka nchini China, lakini bado hayajaridhika, katika sehemu za mashariki ambapo uchumi unaendelea haraka, mambo hayo yanaendelea haraka, lakini katika sehemu za katikati na za magharibi mambo hayo yanaenda pole pole, kwa hiyo serikali inapaswa kutenga fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo ya makumbusho ya sehemu za magharibi ili mambo ya makumbusho yaende kwa uwiano."
Bw. Zhang Wenbin alisema, makumbusho ni urithi wa utamaduni wa taifa, na maendeleo ya taifa hayawezi kutengana na utamaduni wake, tuna uhakika kuwa sambamba na maendeleo ya uchumi wa China, mambo ya makumbusho pia yatapata maendeleo makubwa zaidi nchini China.
|