Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-08 18:29:45    
Barua 1108

cri
Katika wiki kadhaa zilizopita, tuliwaletea makala nne za kipindi cha chemsha bongo juu ya ujuzi wa "Taiwan, kisiwa cha hazina cha China". Baada ya kusikiliza makala hizo, hakika wasikilizaji wetu wengi wameongeza ujuzi kuhusu Kisiwa cha China Taiwan na wataweza kujibu vizuri maswali tuliyotoa kwenye makala hizo, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatuletea majibu kwa wakati uliowekwa.

Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Kilulu Kulwa wa sanduku la posta 161 Bariadi Shinyanga Tanzania ametuletea barua akisema kuwa, yeye anaendelea tu kuchapa kazi na pia kusikiliza vipindi na habari motomoto kutoka Radio China kimataifa katika idhaa ya Kiswahili. Anatushukuru sana kwa ajili ya vipindi murua ambavyo tunawatangazia, pia anatushukuru sana kwa namna tunavyotayarisha vipindi, ambapo kwa hakika tunawashirikisha kikamilifu wasikilizaji wetu kwa kuzingatia michango yao kwa kutangaza barua zao zenye maoni na ushauri mbalimbali unaotolewa ,ili kuboresha vipindi na makala zetu tunazowatangazia, hivyo anatupongeza sana kwa kazi yetu hiyo tunayoifanya kwa umahili na umakini mkubwa.

Anasema hata mashindano ya chemsha bongo kuhusu ujuzi wa masuala na matukio muhimu nchini China ambayo yamekuwa yakiandaliwa na Radio China kimataifa kila mwaka, kwa kweli yanawavutia na kuwaelimisha sana wasikilizaji wetu, ingawa kushiriki katika mashindano hayo ni suala moja na kupata ushindi wa juu ni suala lingine.

Ukweli unabaki palepale kwamba mashindano pamoja na vipindi vyote vya Radio China kimataifa vina manufaa makubwa kwa wasikilizaji wake wote katika dunia nzima. Hivyo anatusihi tusichoke kuwahudumia wasikilizaji wetu na kuwapa maarifa na mbinu mbalimbali za kuifahamu China, kuitembelea China na kuwafanya kuwa marafiki wakubwa wa taifa la China na wananchi wake.

Bwana Kulwa anasema, anapenda atujulishe kuwa amepokea kifurushi chetu tulichomtumia mwezi Septemba ambapo ndani yake kulikuwa na gazeti la China Today lenye habari nzuri nzuri na picha za kuvutia sana. Vilevile amepokea bahasha zilizokwishalipiwa stempu, jambo hili ni zuri kabisa na anaomba Radio China kimataifa iendelee utaratibu huu. Yeye akiwa msikilizaji wetu ataendelea kutuunga mkono kwa hali mbalimbali.

Na mwisho Bwana Kulwa anasema, anapenda atuulize kuwa siku hizi Radio China kimataifa haichapishi kalenda za ukutani, na kama inachapisha basi inachapisha chache tu ambazo hazitoshelezi wasikilizaji wote. Kwani ana miaka mitano sasa hajapokea kalenda kubwa ya ukutani ya Radio China kimataifa. Anaomba kama tutachapisha kalenda ya mwaka 2006, anatushauri tuzingatie matukio ya miaka 55 ya kuzaliwa kwa China, yaani kuonesha ni matukio yapi muhimu yaliyotokea katika miaka 55. Hiyo kalenda inaweza kuwa moja ya zawadi ya motisha kwa wale watakaoshiriki kwenye mashindano ya ujuzi kuhusu miaka 55 ya China mpya. Vilevile zinaweza kutengenezwa beji au medali za viongozi mashuhuri wa China kama vile Mao Zedong, Zhou Enlai, Deng Xiaoping, na wengineo. Anafikiri linaweza kuwa suala zuri sana litakalowavutia wasikilizaji wengi wa Radio China kimataifa katika dunia nzima.

Tunamshukuru sana Bwana Kulwa kwa barua yake na maoni yake mazuri. Kuhusu kalenda, hapa tunasikitika kumwambia kuwa, kweli katika miaka ya hivi karibuni Radio China kimataifa haikuchapisha kalenda za ukutani, kwani idara husika ilisema kuwa hakuna fedha za kutosha. Hali ya mwaka huu ni ipi bado hatujaambiwa. Tunamwomba Bwana Kulwa na wasikilizaji wengine muelewe, kama kalenda itachapishwa, basi hakika tutawatumia wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Mogire O Machuki wa Kijiji cha Nyankware e sanduku la posta 646 Kisii Kenya anasema katika barua yake kuwa, wakati wa mwezi Agosti , Radio China kimataifa ilitangaza mambo mawili ambayo ni kivutio madhubuti kwao, kwanza ni taarifa za kuzinduliwa kwa chemsha bongo ya mwaka 2005, kuhusu Taiwan, kisiwa cha hazina cha China. Anasema amevutiwa sana na mada ya chemsha bongo hili. La muhimu kwao ni kuona hatimaye kisiwa cha Taiwan kurejea kwa China, watafurahi sana.

Pili ni kuwa Radio China kimataifa ilitangaza kuongezwa kwa muda wa matangazo yake kutoka nusu saa hadi saa moja. Aidha matangazo hayo kupitia KBC yatasikika kuanzia saa 9 hadi saa 10 jioni kila siku. Wakati huu bila shaka hautakuwa mwafaka kwa wengi wao lakini watajitahidi kusikiliza hata wakiwa kazini. Ingefaa vipindi hivyo visikike kuanzia saa 11 hadi 12 jioni saa za Afrika mashariki. Ni habari za kuvutia na bila shaka wengi wao watafurahia kwamba hatimaye CRI imesikia kilio chao.

Hivi majuzi alisikia kwenye kipindi cha Daraja la urafiki na kwenye sanduku la barua kuwa viongozi wa ngazi za juu kutoka idhaa ya Kiswahili ya KBC Nairobi waliotembelea China wakitangaza uhusiano mzuri kati ya Kenya na China. Hivyo wanatoa shukrani zao za dhati kwani kuanzia tarehe 1 Septemba mambo yalikuwa shwari zaidi.

Anasema anakumbuka Mama Chen alipozuru Kenya na kuwahutubia wasikilizaji wa CRI kwenye ukumbi wa Hoteli Zonic hapo Kisii aliwaahidi mambo kadha wa kadha ambayo anaona yaelekea kutimia. Kwanza aliwaahidia kuwa mwaka huu msikilizaji wa idhaa ya Kiswahili atazuru China, Xavier L.Telly Wambwa alibahatika, pili alizungumzia kwa kina swala la kuongezwa kwa muda na hili nalo limetimia. Aligusia kwenye hotuba yake juu ya kuongezwa kwa idadi ya watangazaji ili kupunguza uzito wa kazi ya uandaaji wa vipindi kwenye studio ya idara ya Kiswahili ya CRI, na kweli sasa hivi Radio China kimataifa imejaa sauti ngeni na za kuvutia.