Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-15 16:35:50    
Barua 1115

cri
Msikilizaji wetu Okongo Okeya wa sanduku la posta 381 Iganga Uganda ametuletea barua akisema kuwa, yeye ni msikilizaji wa Radio China kimataifa, na hii ni mara yake ya kwanza kuandika barua kwa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa. Anapenda kutoa pongezi kwa serikali ya China na watu wake, anasema serikali ya China ya Jamhuri ya watu wa China ni serikali nzuri, wananchi wake ni waaminifu sana kwa ushirikiano, umoja na mshikamano, na wana upendo kwa watu wote duniani.

Anasema yeye mfanyabiashara na anaendesha duka moja huko Nango Malongo wilayani Mayuge nchini Uganda. Anasema anatushukuru sana wafanyakazi wa Radio China kimataifa kwa kazi yetu nzuri tunayoyafanya. Anasema watu wengi wanachagua kusikiliza Radio China kimataifa, anatutaka watangazaji wa Radio China kimataifa tuendelee kuchapa kazi ili radio hii iendelee kusikika vizuri zaidi.

Msikilizaji wetu Ramadhan Y. Kayungilo wa sanduku la posta 799 Kahama Shinyanga Tanzania anasema katika barua yake kuwa, ana furaha kubwa kuona kwamba mambo ya Radio China kimataifa yanazidi kufanikiwa baada ya kusikia kuwa baada ya siku chache zijazo utajengwa mtambo wa matangazo ya Radio China kimataifa nchini Kenya hata huenda nchini Tanzania yatakayorushwa hewani kwenye masafa ya F.M. Wamefurahishwa sana na hatua hiyo ya Radio China kimataifa. Na wanaamini kuwa matangazo yatasikika vizuri na kupendeza na Radio China kimataifa itafahamika kote Tanzania.

Anasema amejaribu kuwaelimisha wanafunzi na walimu wa hapo shuleni kwao juu ya Radio China kimataifa, wanasema kuwa hawajawahi kupata mwanafunzi ambaye anapenda kusikiliza vyombo vya habari kama yeye, hivyo anapendwa na kupewa sifa hapo shuleni kama kaka mkuu wa shule, mweka hazina, nahodha wa timu ya mpira wa miguu, yote hayo yamekuja sababu ya Radio China kimataifa. Hivyo nao wanaomba kujiunga na Radio China kimataifa na kuwa wasikilizaji bora na wataelimisha wengine kama alivyowaelimisha wao. Na kushirikiana na Radio China kimataifa kwa nguvu zote na kuhakikisha uhusiano kati ya China na Tanzania unaendelea zaidi.

Na Msikilizaji wetu Paschal Mbonja wa sanduku la posta 799 Kahama Shinyanga Tanzania anasema katika barua yake kuwa anaomba kujiunga na shindano la chemsha bongo la Radio China kimataifa. Anasema anapenda na kuvutiwa sana na matangazo ya Radio China kimataifa kwani ni radio yenye mpangilio wa hali ya juu. Amevutiwa na jarida dogo la daraja la urafiki, akiwa kama msikilizaji mpya wa Radio China kimataifa, anaahidi kuwa atashirikiana nasi bega kwa bega kuhakikisha Radio China kimataifa inafahamika kote duniani, mijini na vijijini.

Anasema amefurahi kusikia kuwa siku za usoni matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa yatarushwa hewani kwa kupitia Radio Tanzania Dar es Salaam na Radio Tanzania Zanzibar. Kwani hali ya usikivu wa matangazo ya kupitia masafa mafupi kweli siyo nzuri sana, anatarajia matangazo hayo yatasikika vizuri kupitia masafa ya FM nchini Tanzania mapema iwezekanavyo.

Tunawashukuru sana Bwana Kayungilo na Bwana Paschal Mbojja kwa barua zao na juhudi zao za kusikiliza idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, siku hizi tunafanya juhudi za kuhimiza kazi za kuyawezesha matangazo yetu yarushwe hewani kwa kupitia masafa ya FM ya Radio Tanzania Dar es Salaam na Radio Tanzania Zanzibar, tunaamini kuwa, baada ya juhudi za pande mbili, wasikilizaji wetu walioko Afrika ya mashariki wengi watasikia vizuri matangazo yetu katika siku za usoni, labda ni siku chache baadaye.

Msikilizaji wetu Edwin Mashola wa shule ya sekondaru ya Lake sanduku la posta 567, Mwanza Tanzania ametuletea shairi moja la kuisifu lugha ya Kiswahili, shairi hilo linasema hivi:

Ni lugha gani ni tamu, itamkwapo kinywani

Kutamka huishi hamu, popote ulimwenguni

Miaka mingi yadumu, toka enzi ya mkoloni

Kiswahili lugha yetu, ndugu zangu tuipende

Maneno yake mazuri, mithili ndege tausi

Kiswahili siyo siri, chamtukuza mtu mweusi

Radio China kimataifa, yatangazwa kirahisi

Kiswahili lugha yetu, ndugu zangu tuipende

Tanzania twatukuza, lugha yetu Kiswahili

Uganda yakitangaza, Kenya pia Usomali

Afrika chatuliwaza, na mashariki ya mbali

Kiswahili lugha yetu, ndugu zangu tuipende

Beti ya nne nimefika, ushauri pokeeni

Lazima kuwajibika, Kiswahili tukilindeni

Na tamati nimefika, kalamu naweka chini

Kiswahili lugha yetu, ndugu zangu tuipende

Na Bwana Edwin Mashola anasema kuwa, ushauri wake kwa vijana wenzake ni kuwa wasome kwa bidii kuiletea Tanzania maendeleo na wajikinge dhidi ya ukimwi kwani, wao ndio taifa la kesho.

Na msikilizaji wetu zipporah K. Anari wa sanduku la posta 2995, Kisii Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu, akitumai kuwa sisi hapa Beijing ni wazima. Anatupa hongera kwa vipindi vyetu na matangazo yetu, kwani wanapokea matangazo ya Radio China kimataifa kutoka Beijing kwa hali iliyo safi.

Anasema yeye anatutakia kila la heri sisi watangazaji wote wa Radio China kimataifa. Jamaa zakeo pamoja na wanafunzi wenzake wanapenda kusikiliza Radio China kimataifa, ingawa yeye ni mwanachama mpya wa Radio China kimataifa anasikiliza asilimia 85 na kwa hivyo mawazo yake yanapendelea akimaliza shule awe mtangazaji wa Radio China kimataifa.

Anasema yeye ni mwanafunzi katika shule ya upili Mokwerero na yuko kidato cha tatu. Ingawa yeye ni mwanafunzi anatumia wakati mwingi kwa kusikiliza vipindi vyetu kama vile Klabu ya utamaduni, sayansi na teknolojia na kipindi cha sanduku la barua kinachorushwa hewani kila jumapili.

Anasema yeye ni mwanachama mpya kwa hiyo anaomba tumtumie bahasha zilizolipiwa na kitabu cha kujifunza kichina, na kalenda na jarida dogo la daraja la urafiki pamoja na stika zetu za CRI. Na hapo ana wanachama wapya wanaotaka kujiunga nasi kwa matangazo yetu na vipindi vyetu lakini hawana njia ya kuwasiliana nasi na kwa hivyo anatuomba tuweze kuwatumia bahasha zilizolipiwa. Majina ya wanachama hao ni kama wafuatao: Dorca, Kwamboka, Anari, Joel, Ngoko, Dinah, Kerubo, Albert, Justine, Zilpah, Abner, Mohgare, Noah, Divimah, Esther, Vincent, Eunice, Easter, Bob, Zippy, Dorothy, Jared, Hellen, Susan, Olpha, Alberto, Edward hawa wote wanatuomba tuwatumie bahasha ambazo zimelipiwa ili waanze kuwasiliana nasi.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu hao wanaoomba kujiunga nasi, sisi tunawakaribisha na ni matumaini yetu kuwa wataendelea kusikiliza kwa makini vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo mbalimbali juu ya vipindi vyetu ili tuwahudumie vizuri zaidi wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Albert M. Anari wa sanduku la posta 2995 wa Kisii Kenya anasema katika barua yake kuwa, anatoa shukrani kwa watangazaji wote wa Radio China kimataifa kwa vipindi vyetu na matangazo yetu. Anasema vipindi vyetu na matangazo yetu yanawaelimisha vijana kama yeye, ambao wamejifunza mengi kutoka kwenye matangazo yetu. Anasema katika barua yake ijayo atatutumia picha au michoro. Kutokana na alivyoandika kwenye barua yake, tunaona yeye anapenda kuchora picha, na hata sarufi yake ya Kiswahili ni nzuri, na hata mwandiko wake ni mzuri kama anachora.

Msikilizaji wetu Benson Mbigura wa Sanduku la posta 137 Kakamega Kenya anasema katika barua kuwa, yeye kwenye kipindi cha Sanduku la barua angependa hasa kutushukuru watayarishaji wa vipindi kwa kuweza kukusanya watu wenye asili mbalimbali kote duniani, ili waweze kutoa mafundisho mengi na ya muhimu kupitia Radio China kimataifa. Kwake binafsi anatoa shukrani zake kutokana na ule muda ambao Radio China kimataifa imeweza kuongezewa kutoka dakika 30 hadi saa moja. Na hiyo inaonesha kwamba Radio China kimataifa inajali maoni ya wasikilizaji wake.

Anasema anapenda pia kutoa pongezi kwa kuweza kuwatumia jarida la jarida la daraja la urafiki. Wanafurahi kuwa sasa wataweza kuwafahamu wenzao kwa kuziona picha zao kwenye jarida la daraja la urafiki. Na zaidi ni lile shindano la chemsha bongo, hili shindano litawawezesha wasikilizaji kuonana na mashabiki uso kwa uso kutoka kote ulimwenguni na kubadlishana nao maoni.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-15