Robot ni uvumbuzi mkubwa uliofanywa na binadamu katika karne ya 20. Hivi sasa, zaidi ya miaka 40 imepita tangu robot ivumbuliwe, uvumbuzi huo umepata maendeleo makubwa, sisi binadamu tumekuwa na robot ya kiviwanda, robot ya kuwaongoza wasafiri, robot ya matibabu na robot za aina nyingine nyingi, robot hizo zimekuwa wasaidizi wakubwa wa binadamu.
Kwa kuwa kuwashirikisha vijana katika miradi ya kutafiti na kutengeneza robot ni hatua inayoweza kuwapa vijana hamu na shauku juu ya kutengeneza robot, hivyo nchi mbalimbali zinatilia maanani kazi hiyo ili vijana wengi zaidi wawe wataalamu wa robot katika siku zijazo. China ni moja ya nchi hizo, hatua muhimu zinazochukuliwa na serikali ya China ni kufanya mashindano ya robot kati ya vyuo vikuu mbalimbali kila baada ya muda fulani.
Mashindano ya 4 ya robot yalifanyika siku za karibuni hapa Beijing. Timu 39 kutoka vyuo vikuu mbalimbali zikiwa na robot zao zinashiriki kwenye mashindano hayo, robot hizo zinasanifiwa na kutengenezwa na wanafunzi wenyewe, na uzito wa kila robot inayoshiriki kwenye mashindano hayo unatakiwa kuwa chini ya kilogram 50. Kusanifu na kutengeneza robot si jambo rahisi, kunahitaji ujuzi wa kozi mbalimbali, hivyo wanafunzi hao huwa wanashirikiana kwenye kazi hiyo. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Wuhan, China, Huang Zhenglie akifahamisha alisema:
"Timu yetu ina wanafunzi 18, wakiwemo wanafunzi wa mwaka wa pili, tatu na wa nne, na sisi tunasomea kozi mbalimbali, kwetu, ushirikiano ni muhimu sana."
Mashindano hayo ni ya mchujo, kila timu ina mipira 32, na inatakiwa kushindana na timu nyingine kwa kuendesha robot yake kuweka mipira hiyo kwenye vyombo 9, na timu inayoweka mipira mingi zaidi kwenye vyombo hivyo itakuwa mshindi, na timu inayoshindwa itaondolewa.
Mwandishi wetu wa habari alitazama mchezo mmoja, aliona robot za aina mbalimbali zikishiriki kwenye mashindano hayo, baadhi zina urefu wa mita 1.7, na baadhi zina kasi kubwa, nyingine zinaweza kujiendesha zenyewe, na nyingine baadhi zinaendeshwa na binadamu. Wakati wa mashindano, kila robot ilikuwa na mbinu yake nzuri, kwa mfano, ili kuweka mipira kwenye chombo kirefu, robot ndefu ilitumia mkono wake mrefu, na roboti fupi ilitumia chombo kinachofanana na mtutu na kuirushia mipira hiyo kwenye chombo hicho; kama ni chombo kifupi chenye mtelemko, baadhi ya robot zilisukuma mipira kwenye mtelemko hadi kwenye chombo, nyingine zilitumia kamba yake ya kusafirishia kuiweka mipira kwenye chombo.
Robot inayoitwa Mfalme ilitengenezwa na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Zhejiang, robot hiyo ni ndogo na inaendeshwa na binadamu. Msanifu wa robot hiyo mwanafuzi Zhang Jun alisema:
"Inaonekana ni vigumu kusanifu na kutengeneza robot yenye uwezo mkubwa kama huo, lakini tunatumia kanuni za msingi za sayansi, ambazo sisi sote tunazifahamu na kuzitumia katika maisha yetu ya kila siku."
Wakati wa mashindano, jitihada za kuweka mipira mingi zaidi kwenye chombo hazitoshi kuipatia timu moja ushindi, na timu ikitaka kushinda inapaswa kutilia maanani ulinzi. Kwa upande wa ulinzi, kila robot ina silaha yake ya kipekee, kwa mfano, robot Mfalme tuliyoitaja ina kiyoyozi kimoja. Msanifu wake Zhang Jun akifahamisha kazi ya kiyoyozi hicho alisema:
"Kiyoyozi hicho chenye nguvu kubwa kinaweza kutoa upepo kwa upande mmoja, na upepo huo una nguvu za kutosha za kutoa mipira ambayo imewekwa kwenye chombo."
Mbali na kiyoyozi, robot nyingine zina silaha zao kali, kwa mfano, robot moja ina wavu, baada ya kuweka mipira kwenye chombo, itafunika mdomo wa chombo hicho kwa wavu, ili robot nyingine zisiweze kuweka mpira hata mmoja; baadhi ya roboti kubwa zinaangusha roboti ndogo, lakini robot ndogo haziogopi, zinaziweka robot kubwa vizuizi njiani.
Mashindano hayo ni ya kusisimua. Hali ya mashindano inabadilika kila wakati, na kuwavutia watazamaji. Mmoja wa watazamaji Bw. Li Tao alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kivutio cha mashindano hayo ni kutokuwa na timu moja yenye uhakika mkubwa wa kushinda, kila timu ina uwezo wa kupata ushindi, alisema:
"Naona kuwa kupitia mashindano hayo, kiwango cha usanifu na utengenezaji wa robot kitainuka zaidi, hii ndiyo maana ya kufanyika kwa mashindano hayo."
Mwishoni, Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Beijing kilipata ushindi. Mkurugenzi wa tume ya waamuzi ya mashindano hayo, Profesa Zong Huaguang ambaye alikuwa mwamuzi wa mashindano hayo tangu yafanyike kwa mara ya kwanza hadi kwenye mashindano hayo ya mara ya 4, alieleza maoni yake kuhusu mashindano ya robot, akisema:
"Naona kuwa viwango vya robot zilizoshiriki kwenye mashindano hayo vimeinuka kwa kiasi kikubwa, ya kwanza, wanafunzi waliposanifu robot hizo walitoa dhana nzuri; ya pili, ustadi wa utengenezaji umeboreshwa; ya tatu, wanafunzi walitumia mikakati mizuri katika kuendesha robot zao kushidana."
|