Katika mji wa Beijing kuna jumuiya ya hifadhi ya mazingira isiyo ya kiserikali inayoitwa "kituo cha utamaduni wa mazingira cha kijiji cha dunia cha Beijing", watu hukiita "Kijiji cha dunia cha Beijing". "Kijiji" hicho kinafanya kazi nyingi katika kuhimiza ujenzi wa mtaa usiokuwa na uchafuzi na kuinua mwamko wa wakazi kuhusu hifadhi ya mazingira. Mwanzilishi wa kijiji hicho anaitwa Liao Xiaoyi.
Bi. Liao Xiaoyi ana umri wa zaidi ya miaka 50, amewahi kufanya kazi katika taasisi ya sayansi ya jamii ya China, mwaka 1993 hadi mwaka 1995 alikwenda kupata mafunzo nchini Marekani. Yeye siku zote anafuatilia masuala ya hifadhi ya mazingira ya China, hivyo aliacha fursa ya kubaki nchini Marekani na kurudi nchini China. Akisema:
"Kabla ya kwenda Marekani nilikuwa na kikundi cha wapiga picha za video, tulitengeneza filamu ya televisheni iitwayo 'ustaarabu kuhusu hifadhi ya mazingira nchini China'. Najua kuwa, China ina matatizo makubwa ya kimazingira ambayo bado hayajafuatiliwa vya kutosha na vyombo vya habari vya China, naona ninawajibika kufanya jambo hilo."
Baada ya kurudi China kutoka Marekani, Bi. Liao Xiaoyi si kama tu alimalizia filamu ya televisheni ya "ustaarabu kuhusu hifadhi ya mazingira nchini China", bali pia alianzisha "kituo cha utamaduni wa mazingira cha kijiji cha dunia cha Beijing", na kuanzisha kipindi maalum cha televisheni kiitwacho "hifadhi ya mazingira" kwenye kituo kikuu cha televisheni cha China CCTV. Lengo lake ni kuinua mwamko wa wananchi wa China kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira. Hadi leo, Bi. Liao Xiaoyi ameandika makala yenye maneno zaidi ya laki nne na kutengeneza vipindi zaidi ya 100 vya televisheni kuhusu hifadhi ya mazingira. Yeye pia amewahimiza wakazi wa Beijing kutilia maanani hifadhi ya mazingira kwa kuendesha shughuli za aina mbalimbali kama "matumizi endelevu na kuishi maisha katika mazingira yasiyo na uchafuzi", na kuwahimiza wanafunzi wa shule za msingi na wazazi wao kujaza kadi ya kuahidi kufuatilia hifadhi ya mazingira.
Bi. Liao Xiaoyi aliyejifunza somo la falsafa katika chuo kikuu anapenda kuzingatia mambo na kutekeleza mawazo yake kwa vitendo. Bi. Lili anayeshughulikia usimamizi wa miradi katika "kijiji cha dunia cha Beijing" alisema:
"Bi. Liao Xiaoyi ni shupavu, hawezi kusita katika kutekeleza mawazo yake kwa vitendo. "
Ili kuinua mwamko wa wananchi kuhusu umuhimu wa hifadhi ya mazingira, Bi. Liao Xiaoyi amekodi hekta 180 za msitu kwenye kitongoji cha Beijing na kulifanya eneo hilo kama "kituo cha elimu ya hifadhi ya mazingira", yaani "kijiji cha dunia cha Beijing". Wakazi waishio katika kijiji hicho wanatenganisha takataka za kimaisha, kutumia nishati ya mwangaza wa jua, kulima mazao ya kilimo bila kutumia dawa au mbolea za kemikali. Hivi sasa, kijiji hicho chenye misitu, ardhi oevu, pori, vijito na familia zaidi ya 40, kimekuwa sehemu ya utalii wa kimaumbile, ambacho kimewavutia watalii wengi.
Katika miaka 9 iliyopita, "kijiji cha dunia cha Beijing" kimekuwa na wafanyakazi rasmi 15, na waliojitolea zaidi ya elfu moja. Ikiwa jumuiya isiyo ya kiserikali ya China inayofanya utafiti wa nadharia, kutengeneza filamu, kutoa elimu na kufanya maingiliano ya kimataifa, "kijiji cha dunia cha Beijing" kimefuatiliwa sana na jumuiya ya kimataifa na vyombo vya habari vya kimataifa. Mwaka 2000, Bi. Liao Xiaoyi alipewa tuzo ya Sophie ya hifadhi ya mazingira ya kimataifa, pia alipewa sifa ya "Balozi wa ustaarabu wa hifadhi ya mazingira" na serikali ya China. Kamati ya maandalizi ya mashindano ya michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 ya Beijing imemwalika Bi. Liao Xiaoyi kuwa mshauri wa hifadhi ya mazingira.
Wakati watu wengi wanafuatilia maisha ya anasa na ya kisasa, Bi. Liao Xiaoyi anaishi maisha ya kawaida. Hapendi kuendesha gari na kutumia kiyoyozi. Anapendelea kupanda ngazi kwa miguu badala ya lifti. Akisema:
"Naona kuwa, kuthamini raslimali, kurahisisha maisha, kuongeza ujuzi, kujenga mwili, na kuheshimu dunia ya maumbile, mimi naridhika na maisha hayo. Tungefuatilia zaidi afya zetu, dunia ya maumbile na roho zetu kuliko mali."
Yeye anachukulia kuwa maisha ya binadamu yanatakiwa kufuatilia zaidi masikilizano kati ya binadamu, na kati ya binadamu na dunia ya maumbile.
Binti yake Kele ana umri wa miaka 18, kutokana na athari ya mama yake, Kele pia anafuatilia hifadhi ya mazingira. Yeye husafisha sakafu na choo kwa kutumia maji yaliyotumika baada ya kufua nguo na kusafisha mboga. Anapokula chakula katika mkahawa hutumia vijiti anavyokwenda navyo mwenyewe ili kuokoa raslimali ya miti. Akisema:
"Nampenda sana mama yangu, na vitendo vyake katika maisha ya kila siku vimeniathiri sana."
Hivi sasa, Kele anamsaidia mama yake kutengeneza filamu kuhusu utamaduni wa mazingira ya viumbe wa China. Akitumai kuwa, filamu hiyo itawahimiza watu wengi zaidi kufuatilia hifadhi ya mazingira ya viumbe, na kufuatilia dunia hii tunayoishi sote.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-17
|