Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-21 19:26:19    
Safari ya kuangalia mambo ya kidini mkoani Shanxi

cri

Mkoa wa Shanxi uko kwenye sehemu ya kaskazini ya China, ni mkoa kati ya sehemu muhimu kwa maendeleo ya utamaduni wa dini za Kibudha n Kidao nchini China, ambapo utamaduni murua wa kidini, majengo, sanamu na michoro ya kidini vinaonekana katika sehemu nyingi. Licha ya hayo, mkoa wa Shanxi pia ni bahari ya vitu vya sanaa vya kidini na ni moja ya sehemu zenye mabaki mengi ya dini ya kibudha nchini China.

Ukisafari kutoka Beijing kuelekea upande wa magharibi kwa garimoshi baada ya saa 5 utafika Datong, ambao ni mji wa pili kwa ukubwa mkoani Shanxi. Jina la Datong limevuma sana nchini China kutokana na mapango ya mawe yaliyoko kwenye sehemu ya Yungang yaliyojengwa miaka zaidi ya 1,500 iliyopita. Mapango ya mawe ya Yungang yamepangana kwa umbali wa mita 1,000 kutoka upande wa mashariki hadi upande wa magharibi kwenye mlima wa Wuzhou, ulioko kwenye kiunga cha magharibi cha mji wa Datong. Data zilizohifadhiwa zinaonesha kuwa mapango hayo ya mawe yalianza kutengenezwa mwaka 460 kutokana na pendekezo la mtawa Tan Yao. Hivi sasa ni mapango 53 tu ambayo watu wanaweza kuyaona yenye sanamu za budhaa za mawe zaidi ya 51,000. Kati ya hizo iliyo kubwa kabisa ina kimo cha mita 17 na iliyo ndogo kabisa ina kimo cha sentimita kadhaa tu. Hayo ni moja ya mapango makubwa ya mawe nchini na pia ni "bahari" maarufu ya vitu vya sanaa duniani. Mapango ya mawe ya Yungang yanajulikana sana duniani kutokana na ukubwa wake na sanamu zilizochongwa kwa ufundi wa kiwango cha juu. Siyo tu kuwa sanamu hizo zilichongwa kwa kutumia sanaa za dini ya kibudhaa, bali pia zilitumia mtindo wa sanaa za jadi za kichina. Mtalii kutoka Italia Bibi Filomena riccarda alivutiwa sana alipotembelea mapango ya mawe ya Yungang, alisema: Ni mara yangu ya kwanza kuona mapango makubwa namna hiyo, yamenishangaza sana. Sanamu hizo za Buddha ni za kuchongwa kwa ufundi wa kiwango cha juu, ambazo zinafanana na watu hai. Naona utamaduni wa dini ya kibudha wa China ni mkubwa na adhimu. Ingawa safari za utalii ni za kuchosha, lakini ninapoona sanamu hizo, nasahau uchovu wangu, sanamu nzuri sana ajabu.

Baada ya kuangalia mapango ya mawe ya Yungang, kusafiri kwa gari kwa muda wa saa mbili au tatu hivi kuelekea magharibi, watu wanafika kwenye mlima wa Heng ambao ni sehemu nyingine ya utalii inayohusika sana na mambo ya kidini mkoani Shyanxi. Umaarufu wa mlima Heng unatokana na hekalu dogo lililoko kwenye mteremko wa mlima. Mlima Heng unaonekana kama sufuria moja lililotundikwa ambalo sehemu ya kati iliingia ndani, na hekalu hilo liko kwenye sehemu ya chini ya sufuria. Nchini China kuna msemo unaosema kuwa "nyumba yenye ghorofa" inajengwa kwenye ardhi, lakini ni kinyume cha msemo huo kuwa hekalu hilo dogo limejengwa kwenye genge la mlima ambalo linaonekana kama jingo lenye hatari ya kuanguka, hata hivyo jengo hilo hadi hivi sasa limedumu kwa miaka zaidi ya 1,4000.

Hekalu hilo lilijengwa kwa kutumia elimu za nguvu na uzuri zinazounganishwa na mambo ya kidini. Hekalu lililojengwa kwenye "sehemu ya chini ya sufuria" linaweza kukwepa athari ya upepo mkubwa. Mbali na hayo milima iliyoko mbele yake inaweza kuisitiri chini ya mwangaza mkali wa jua. Inasemekana kuwa katika siku za joto mwangaza wa jua unaweza kulipata hekalu hilo kwa saa mbili, tatu hivi kwa siku. Si ajabu kuwa hekalu hilo lililotundikwa kwa uimara kwenye mteremko wa mlima limeweza kuvumilia upepo, mvua hata tetemeko la ardhi katika miaka zaidi ya 1,400 iliyopita. Bw. Kong Yifan ambaye aliwahi kwenda huko kuangalia hekalu hilo, alisema kuwa, watu walioko kwenye hekalu hilo lililotundikwa huingiwa na hofu kubwa.

Alisema, kitu kilichonitisha zaidi ni kuingia kwenye ujia uliojengwa kwa mbao na kutundikwa angani baada ya kupita jukwaa lililoko mbele ya ukumbi wa Buddha, ambapo watu wanapita kwa uangalifu mkubwa na kuchuchumia kama wanapita kwenye barafu nyembamba mtoni, wanaogopa kuwa pengine wanakanyaga kwa nguvu wataangusha ule ujia na kuanguka kutoka angani.

Kulikuwa na sababu maalum ya kujenga juu kwa juu kwenye genge la mlima. Mtawa kijana Xuan Hao alisema, "Hapo zamani hap palikuwa njia muhimu ya kukwenda Wutai kwa upande wa kusini na kwenda Datong kwa upande wa kaskazini, hekalu kujengwa hapa ni rahisi kwa waumini kwenda kuabudu Buddha. Sababu ya pili ni kuwa maji ya mto Hun yanapita chini ya mlima ulioko mbele ya hekalu hilo ambapo kuna mafuriko ya mara kwa mara kutokana na mvua nyingi. Hivyo hekalu hilo lilijengwa kwenye genge la mlima lenye urefu wa zaidi ya mita 300 kwenda juu.

Ingawa hekalu hilo ni dogo, lakini ndani yake kuna mambo kemkem ikiwa ni pamoja na sanamu za Buddha zaidi ya 80 zilizotengenezwa kwa shaba, chuma, udongo wa ufinyanzi na mawe. Sanamu hizo ni zenye heshima na kuvutia watu. Umaalum mwingine ni kuwa sanamu za Sakyamuni, Laozi na Confucius ziko ndani ya ukumbi mmoja ulioko kwenye ghorofa la pili ambalo ni la juu kabisa katika jengo hilo. Hali ya waanzilishi wa dini tatu za kibudha, kidao na ki-Confucius kuwa katika ukumbi mmoja, ni nadra sana kuonekana katika sehemu nyingine nchini.

Baada ya kupita mlima Heng na kusafiri kwa saa tatu ndani ya gari, kuna mlima wa Wutai ambao ni mmoja kti ya milima mine mikubwa maarufu ya dini ya kibudha nchini China. Mlima huo unajulikana sana kama milima mingine ya Emei mkoani Sichuan, Putuo mkoani Zhejiang na Jiuhua mkoani Anhui. Sehemu iliyoinuka zaidi kwenye mlima Wutai ina urefu wa zaidi ya mita 3,000 juu ya usawa wa bahari, mlima huo umeundwa kwa milima mitano iliyoungana kwa umbo la mviringo. Vilevile na magenge ya milima pamoja na misonobari ya huko ni maridadi na ya kupendeza zaidi kuliko ya sehemu nyingine. Hivi sasa kuna mahekalu karibu 50 kwenye mlima Wutai yakiwa ni pamoja na yale maarufu sana ya Xiantong na Tayuan pamoja na mahekalu mengine ya Wanfu na Pusading. Majengo makubwa na nadhifu, sanamu zilizochongwa kwa ufundi mkubwa na mabaki ya vitu vya utamaduni vya kale vya huko, vinawafanya watu wajione kama wako kwenye mazingira yenye mambo mengi ya siri. Mwongoza safari kutoka kampuni ya utalii ya Yiyou ya Beijing Dada Li Jing ambaye anaongoza watalii kutembelea mlima wa Wutai mara kwa mara alisema kuwa, mlima Wutai uko katika sehemu ya kaskazini ya China na ni mahali pazuri pa kufanya utalii katika majira ya joto kutokana na mwinuko mkubwa wa sehemu hiyo. Alisema kuwa, si vizuri kwenda huko baada ya mwezai Oktoba, kwani mlima Wutai umeinuka sana, hivyo hali ya hewa ya huko ni baridi, siku alipokuwa huko ilianguka theluji. Vitu vinavyopendeza zaidi kwenye mlima Wutai ni mahekalu yake ambayo watu wengi wanayatembelea.


1  2