Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-23 20:35:40    
Kujenga miji inayozingatia afya ni sehemu muhimu ya ujenzi wa jamii yenye masikilizano

cri

Kwenye mkutano uliofunguliwa tarehe 20 mjini Shanghai kuhusu ujenzi wa miji inayozingatia afya, waziri wa afya wa China Bw. Gao Qiang alisema kuwa ujenzi wa miji inayozingatia afya unaochipuka kwa nguvu hivi sasa umekuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa jamii yenye masikilizano nchini China.

Kutokana na maelezo, kuanzia katikati ya miaka ya 80 ya karne iliyopita, kutokana na kukabiliana na changamoto ya afya itakayoletwa na ujenzi wa miji kwenye karne ya 21, WHO ilitoa wito wa kujenga miji inayozingatia afya. Miji elfu kadhaa imeshiriki kwenye harakati hizo, na kati ya miji hiyo, miji mingi ni ya nchi zinazoendelea. Mwaka 1996 China ilijiunga na harakati hizo. Mtaa wa Mashariki katika mji wa Beijing, mtaa wa Jiading katika mji wa Shanghai, mtaa wa Yuzhong katika mji wa Chongqing na mji wa Haikou mkoani Hainan ni miji ya kwanza iliyoshiriki kwenye harakati hizo, kisha miji mingine kama Dalian, Baoding na Suzhou pia ilishiriki. Mwaka 2003 mji wa Shanghai ulitangaza kushiriki kwenye harakati hizo kwa mji mzima. Huu ni mji wa kwanza ulio mkubwa kushiriki kwenye harakati hizo kwa mji mzima nchini China.

Bw. Gao Qiang alisema, ingawa ujenzi wa miji inayozingatia afya hivi sasa uko mwanzoni tu, lakini kabla ya hapo, "vuguvugu la afya" lililofanywa kote nchini China katika miaka ya 50 limeweka msingi na ni nguvu ya kusukuma mbele harakati hizo. Jukumu kubwa la serikali la kutaka kulinda afya ya umma na matumaini makubwa ya umma ya kutaka kuboresha hali ya afya ni nguvu kubwa ya kuendeleza harakati hizo.

Bw. Gao Qiang alisema kuwa ujenzi wa miji unatakiwa kufuata kanuni tatu muhimu zifuatazo:

Kwanza, harakati lazima ziambatane na hali ilivyo ya miji yenyewe. Harakati zifanywe kwa mujibu wa hali ilivyo ya miji yenyewe hatua kwa hatua. Tusiweke kigezo au masharti sawa kwa miji yote ili miji mingi zaidi ishiriki kwenye harakati hizo. Hii inalingana na mahitaji ya maendeleo ya afya ya miji yenye hali tofauti ya China. Kila mji uanzishe harakati hizo kwa mujibu wa hali yake ilivyo na kuchagua njia inayofaa na kutoa lengo linaloweza kufikiwa, kuweka mpango kwa sayansi na kukusanya nguvu zinazoweza kutumika kwenye hatakati hizo, kuboresha mazingira ya afya na ya jamii, kuongeza mwamko wa umma wa kulinda afya na kuwa na mazoea mazuri ya kimaisha, kuinua kiwango cha afya ya umma, kuhimiza maendeleo endelevu ya uchumi, jamii na afya katika hali ya uwiano.

Pili, harakati za kujenga miji inayozingatia afya zifanywe pole pole kutoka mambo machache hadi mambo mengi, na kutoka uchache mpaka wingi. China ina ardhi kubwa na watu wengi, miji katika sehemu tofauti inatofautiana katika uchumi, usimamiaji wa jamii na huduma za jamii, mambo yanayoathiri afya ya umma pia ni tofauti, na mtizamo wa umma kuhusu afya na matakwa yao pia ni tofauti. Kwa hiyo harakati zinafaa kufanywa kwa mujibu wa hali ilivyo na hatua kwa hatua, miji fulani itangulie kwanza kutekeleza harakati hizo na mwishowe kutapakaa kwenye miji yote na nchini kote.

Tatu, mila nzuri itukuzwe na kuvumbua njia mpya. Katika harakati za kujenga miji inayozingatia afya, uzoefu wa "vuguvugu la afya" lililofanywa kote nchini China katika miaka ya 50 unahitaji kuenziwa, idara za serikali zishirikiane na kuwa nguvu moja, kuuhamasisha umma ushiriki kwenye harakati hizo kwa juhudi, kueneza elimu ya afya na kuleta mazingira ya kujenga miji hiyo katika jamii nzima na "kuyafanya mazingira, binadamu na jamii yaendelee kwa uwiano".