Hapo zamani katika majira ya baridi wakulima wa wilaya ya Anse mkoani Shanxi walikuwa hawafanyi kazi ila tu kuota jua. Hivi sasa wakulima hao wamejenga mabanda makubwa yaliyofunikwa kwa karatasi za plastiki ya kupandia mboga kwenye mteremko wa mlima, ili kuziwezesha mboga wanazopanda kupata mwangaza wa jua kwa saa nyingi zaidi kila siku katika majira ya baridi.
Wanaume wa mkoa wa Shanbei wanajulikana sana kwa ari yao kubwa katika maonesho ya mchezo wa kupiga ngoma wanazojifunga viunoni, na wanawake wa huko wanafahamika kwa uhodari wao katika ukataji wa picha kwenye karatasi. Lakini katika miaka mingi iliyopita wakulima wa Anse waliishi maisha magumu kutokana na ardhi ya huko kutokuwa na rutuba. Mwaka 1992, mkurugenzi wa kamati ya kijiji cha Hougoumen Bw. Yang Fengqi alipanda hekta 0.033 ya mboga kwa majaribio, ambapo wakulima wa kijijini walimwangalia kwa macho la mashaka, lakini mambo yalianza kubadilika.
Mwezi Oktoba mwaka huu, kutokana na uungaji mkono wa serikali ya wilaya, Bw. Yang Fengqi alipata mkopo wa Yuan 6,800, na alitumia fedha hizo kujenga banda moja kubwa la mboga kwenye mteremko wa mlima ambalo lilikuwa la kwanza kwenye sehemu ile. Miche ya matango ilikua vizuri ndani ya banda lake. Ilikuwa siku za kukaribia sikukuu kubwa ya jadi ya Spring ya China aliyauza matango yake na alipata Yuan zaidi ya 5,000. Tokea hapo maisha ya wakulima wa wilaya ya Anse yaliingia kwenye kipindi kipya.
Muda si muda wakulima wa wilaya hiyo walikuwa katika mkondo wa kujenga mabanda ya mboga. Kila mahali hata kwenye nyua za nyumba za wanakijiji yaliijengwa mabanda ya mboga. Maofisa wa serikali ya wilaya waliwashawishi wakulima wa huko wajenge mabanda ya mboga kwenye miteremko ya milima kwani mboga zinazopandwa huko zinaweza kupata mwangaza wa jua kwa saa moja zaidi. Ugunduzi huo uliwafurahisha sana wakulima, kwani wanathamini sana mwangaza wa jua, hivyo wakaanza kujenga mabanda ya mboga kwenye miteremko ya milima.
Wakulima wa mboga wanafahamu kuwa pato lao kutokana na mauzo ya mboga ni kubwa mara 30 kuliko kulima mazao ya chakula, tena mboga zinaweza kuuzwa haraka. Wataalamu wa taasisi ya sayansi baada ya kufanya uchunguzi huko wanasifu uvumbuzi huo wa "kufuatilia mwangaza wa jua", wanasema, "Anse imegundua njia moja yenye tumaini kwa sekta ya mazao ya kilimo yanayopandwa ndani ya mabanda ya plastiki".
Ili kuwasaidia wakulima wa mboga kujenga mabanda ya mboga kwenye miteremko ya milima yenye mwangaza mwingi zaidi, serikali ya wilaya ilitoa mikopo kwa wakulima wa mboga ambayo ni Yuan 4,800 hadi 5,000 kwa banda moja; Kuwasaidia wakulima kuepusha hasara; Kutoa tuzo ya zawadi ya fedha Yuan laki 4 kwa wakulima hodari wa mboga na kutenga Yuan milioni 10 kuanzisha shamba la majaribio la mbegu mpya za mboga, semina ya mafunzo ya teknolojia ya upandaji mboga na kuotesha miche ya mboga kwa njia ya kisasa.
Hivi sasa kijiji cha Hougoumen kimejenga mabanda zaidi ya 400 ya mboga ambayo pato la mwaka jana la kijiji hicho lilikuwa Yuan zaidi ya milioni 2.8, ambapo wastani wa pato la kila mtu ulikuwa Yuan 3,240. Hivi sasa wilaya ya Anse yenye idadi ya wakulima zaidi ya elfu 30, imejenga mabanda ya mboga zaidi ya elfu 30. Katika msimu wa nyanya, wanaweza kutoa tani zaidi ya 100 za nyanya. Takwimu ya ofisi ya mboga ya wilaya hiyo inaonesha kuwa pato la wilaya hiyo kutokana na mabanda ya mboga lilizidi Yuan milioni 100 kwa mwaka. Hivi sasa wakulima wa huko wanajitahidi kuendeleza uzalishaji wa mboga kwenye mabanda na kuinua kiwango cha maisha yao.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-24
|