Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-25 18:18:41    
Mkenya aionavyo China kwa macho yake

cri

Bwana Nobil Macharia anatoka mji wa Kisumu, sehemu ya magharibi mwa Kenya. Kuanzia tarehe 20 Oktoba hadi tarehe 28 Novemba ameshiriki kwenye semina ya bioteknolojia ya chakula iliyoandaliwa na wizara ya biashara ya China na taasisi ya utafiti wa chakula na uumuaji wa chakula cha China KALIFI. Amejifunza mambo mengi katika semina hiyo. Kwenye sherehe ya kufungwa kwa semina hiyo iliyofanyika tarehe 25 Novemba, Bw. Macharia kwa niaba ya wanafunzi wengine kutoka Kenya alitoa hotuba fupi akisema:

"Bioteknolojia ya chakula imechangia katika kukua kwa uchumi wa dunia nzima, tumeona jinsi China inavyoongoza katika sekta hii. Tunaishukuru China kwa kukubali kushirikiana na nchi zinazoendelea katika kutupatia maarifa na ujuzi. Tungependa kuihakikishia serikali ya China kuwa tutafanya kadiri tuwezavyo ili kufanikisha mafunzo ambayo tumepata kusambazwa kwa wakenya wenzetu na kupendekeza kwa serikali mabadiliko katika sera zake, ili kujulisha mambo ya bioteknolojia hasa zile zinazohusu ushirikiano baina ya watafiti na wawekezaji. Tumeiomba serikali ya China iendelea na msaada na ushirikiano katika tekinolojia ili kuweza kuboresha uwekezaji katika sekta ya chakula."

Licha ya kushiriki kwenye mihadhara iliyotolewa na wahadhiri wa China kuhusu bioteknolojia ya chakula, Bw. Macharia na wanafunzi wengine pia walipangiwa kutembelea viwanda vya kutengeneza chakula ili waone kwa macho yao wenyewe jinsi teknolojia ya China ya kutengeneza chakula inavyofanya kazi.

Bwana Macharia pia ametembelea sehemu mbalimbali zenye vivutio, kama vile uwanja wa Tiananmen, kasri la wafalme wa enzi ya Qing, ukuta mkuu, na hekalu la Shaolin.

Kama waafrika wengine, Bwana Macharia pia anapenda sana Gongfu ya kichina, zamani aliwahi kutazama filamu nyingi kuhusu Gongfu ya China. Mara hii amepata nafasi ya kutembelea mwenyewe hekalu la Shaolin, mkoani Henan, ambako ni mahali maarufu pa Gongfu ya kichina, na kuona kwa macho yake mwenyewe maonesho ya Gongfu ya kichina.

Bw. Macharia alisema kusikia siyo kuona, kabla ya kufika China alisikia habari nyingi kuhusu China, lakini kuona kwa macho yake mwenyewe ndiyo kumempa picha halisi kuhusu China. Akisema:

"Kusema kweli, nilikuwa nimesoma mambo mengi kuhusu China, lakini yale tunayosoma na yale tunaona yana tofauti kubwa. Nilipofika hapa China nilishangaa sana kuona jinsi wachina walivyoendelea. Kuanzia mabarabara yao, makazi yao hata mazingira yao, wameyapanga kwa utaratibu tofauti na jinsi ilivyo kwenye nchi zetu zinazoendelea.

Watu wa China ni wakarimu. Nilishangaa kwamba, maneno ya uhalifu katika nchi hii hata kwenye miji mikubwa si mambo ya kawaida, unaweza kutembea usiku bila kuogopa."