Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-28 15:04:17    
Vivutio vya Mji Pingyao

cri

China ni nchi yenye historia ya miaka elfu 5, na katika historia ndefu kama hiyo ipo miji mingi ya kale, mji mdogo uitwao Ping Yao ni mmoja kati yake.

Mji wa Ping Yao uko katika sehemu ya kaskazini ya China, mkoani Shanxi. Kutokana na utamaduni wake usio wa kawaida, mwezi Desemba mwaka 1997 mji huo uliorodheshwa na Unesco kwenye kumbukumbu za urithi wa utamaduni wa dunia.

Watu wameamka alfajiri mapema na kuanza maisha ya siku mpya. Wakazi wa mji wa Ping Yao kizazi kwa kizazi wameishi katika mji huo mdogo kwa zaidi ya miaka 600. Ni siku hizi tu ambapo kutokana na kuimarika kwa utalii na hasa baada ya kuorodheshwa na Unesco kweneye kumbukumbu za utamaduni wa dunia, mji huo uliokuwa kimya umepata umaarufu nchini China na nje.

Mji wa Ping Yao una umbo la mraba, na eneo la kilomita 2.25 tu. Barabara iliyonyooka toka kusini hadi kaskazini inapita katikati ya mji na inakutana na barabara nyingine iliyonyoooka kutoka mashariki hadi magharibi kwenye kitovu cha mji. Barabara hizi mbili ndio mawasiliano pekee katika mji huo. Paa za rangi ya manjano za makazi ya maofisa wa kifalme na mahekalu na paa zenye rangi za kijivujivu za nyumba za wananchi wa kawaida zinaonyesha wazi tabaka za watu katika jamii ya zamani nchini China.

Mwongozaji wa utalii Bibi Liang Yuru alimwambia mwandisi wetu wa habari kuwa, kama kuangalia Mji Pingyao kutoka angani, unaweza kushangaa na kuona kuwa umbo la mji huo wa kale ni kama kobe mmoja mkubwa! Akisema:

Unaweza kuona kuwa umbo la mlango wa kusini wa mji Pingyao kama kichwa cha kobe, na tunaweza kuona visima viwili nje ya mlango huo, ambavyo vinamithilisha macho mawili ya kobe. Na umbo la mlango wa kaskazini ya mji ni kama mkia wa kobe, ambapo ni sehemu ya chini zaidi mjini humo.

Kwa kulinganishwa na mtindo wa ujenzi katika sehemu ya kusini ya China, mtindo wa mji wa Ping Yao unaonekana wa adhama zaidi. Mtindo wake wa China ya kaskazini, ukuta wa kiwanja chenye nyumba pande nne ni mrefu, nyumba zina safu kadhaa ambazo mtindo huo ni kama kiwanja chenye nyumba pande nne mjini Beijing, lakini unaonekana wenye mafumbo zaidi. Kwenye madirisha na milango kuna michongo ya sanaa, ambayo ni makini sana."

Makazi katika mji wa Ping Yao ni nyumba zilizojengwa kwenye pande nne zikiacha uwazi katikati, huu ni mtindo wa ujenzi wa kaskazini mwa China, ambao huwa na mstari katikati, na pande mbili za mstari huo zinalingana, aghlabu nyumba huwa na safu mbili au hata tatu kutoka nje hadi ndani. Karibu na nyumba kuna ukuta mrefu kiasi cha mita 8 hivi bila ya dirisha ili kukinga upepo wenye mchanga. Kwenye milango na madirisha kuna michongo makini ikionyesha upendo au matumaini mema ya wenye nyumba.

Nyumba nyingi za raia zilijengwa katika Enzi ya Ming na Qing ambapo hadi sasa zimefikia miaka zaidi ya 600, na hadi sasa zimesalia nzima zaidi ya 400. Katika muda wa zaidi ya nusu karne hivi, wakazi wa mji wa Ping Yao walikuwa wakishughulika na maisha yao kimya kimya katika mji huo. Mtalii kutoka sehemu nyingine nchini China Bibi Li Yu alivutiwa sana na majengo ya kale mjini Pingyao akisema:

Majengo hayo yamedumisha umaalumu wa zama za kale, nikiyaangalia nafikiri kuwa wakati wa zama za kale, mji huo kweli ulikuwa na usitawi mkubwa, hivyo natembeatembea mjini humo, hata naweza kujisikia kuwa kama nimerudi katika zama za kale.

Katika historia ya China, miji yote inapokuwa na hadhi fulani hujenga ukuta wa miji, hali kadhalika mji wa Ping Yao. Ukuta wa Mji wa Ping Yao sasa bado upo na ni kivutio kwa watalii.

Inasemekana kwamba kiasi cha miaka 2,800 iliyopita, watawala wa enzi hizo walipiga kambi ya kijeshi katika mji huo, wakajenga ukuta kwa udongo, na ndio ukuta wa kiasili wa mji huo. Mwaka 1370 ukuta wa sasa wenye urefu wa mita elfu 6 na kimo cha mita 12 ulijengwa upya kwa matofali na mawe.

Tunapozungumzia mji wa Ping Yao hatuwezi kuwasahau wafanyabiashara wa mji huo, ambao walikuwa wamesambaa kote nchini China, na mji wa Ping Yao ukajulikana kama "Wall Street" ya China.

Mapema mwaka 1823 Enzi ya Kifalme ya Qing, katika mji huo kulianzishwa duka la ubadilishaji wa fedha lililojulikana kama "Re Sheng Chang" ambalo ni la kwanza kabisa katika historia ya China kutumia hundi badala ya fedha taslimu. Kuansishwa kwa duka hili ina maana ya mwanzo wa kipindi kipya katika mambo ya fedha nchini China.

Barabara ya magharibi inastahiki kuitwa barabara ya biashara katika enzi hizo. Hadi sasa pembeni mwa barabara hiyo maduka yanashikamana, hali inayoonyesha ustawi ulivyokuwa zamani. Nyumba zenye maduka si za ghorofa lakini hazionekani kama zimechakaa ingawa miaka mingi imepita. Biashara inaendelea kuwa moto moto kana kwamba ilikuwepo miaka zaidi ya 100 iliyopita. Duka la kwanza la kubadilisha fedha za kisehemu bado lipo miongoni mwa maduka mengi. Kutokana na hali yake duka hili halionyeshi kama ni la kifahari, lakini lilikuwa kituo cha mambo ya fedha nchini China. Katikati ya karne ya 19 duka hili lilikuwa katika kipindi chake cha ustawi kabisa, na lilikuwa na jumla ya matawi 40 ambapo 22 kati hayo yalikuwa katika mji huo. Ni jambo la ajabu kwamba kabla ya miaka 100 iliyopita wenye mabenki wa mwanzo wa China walihifadhi fedha zao kwa hundi katika barabara hii yenye urefu wa kiasi cha mita 100 tu.

Profesa wa chuo kikuu cha Tokyo cha Japan Bwana Hamasita Takesi aliwahi kutembelea mjini Pingyao, alipoona duka la "Re Sheng Chang" alisema:

Katika historia ya China, wafanyabiashara wa Mji wa Ping Yao hawakuwa wakifanya biashara humu nchini tu bali pia katika nchi za nje. Hata katika taasisi ya chuo kikuu chetu tumegundua data nyingi kuhusu shughuli za wafanyabishara wa Shanxi, China.

Wafanyabiashara wa mji wa Ping Yao walianza kugawanyika katika makaundi walipokuwa katika Enzi ya Ming, na wakati wa Enzi ya Qing biashara yao ilikuwa katika hali nzuri kabisa. Biashara yao na nchi za nje, hasa na Russia, ilikuwa ya kubadilishana ngozi na chai. Hii ilikuwa biashara yenye faida kubwa.

Baada ya kutajirika wafanyabiashara walijenga majumba ya chama cha wafanyabiashara. Hadi leo zaidi ya majumba hayo 100 yapo katika mikoa ya Shandong, Henan na mji wa Beijing. Majumba yote hayo ni ya kifahari ambapo yanaonyesha kwamba wafanyabiashara wa enzi zile walikuwa matajiri sana.

Ukitembelea mjini Ping Yao utagundua kwamba ukuta wa mji, barabara, makazi, maduka na mahekalu kimsingi yanahifadhiwa vizuri. Huko wenyeji ni waaminifu, wanazingatia sana kuhifadhi majengo ya zamani na wanajivunia mji wao. Walisema, tunaposhughulika na ujenzi wa kisasa, tunapaswa kuhifadhi baadhi ya majengo muhimu ya kihistoria. Ping Yao ni mji uliokamilika katika miji maarufu ya kistoria nchini China.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-28