Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-11-29 14:24:29    
Uchumi unaokuzwa kwenye sehemu ya kati ya China

cri

Sehemu ya mashariki ya China ni sehemu iliyotangulia kutekeleza sera za kufungua mlango na kuongoza maendeleo ya uchumi nchini China. Ikilinganishwa na sehemu hiyo, sehemu ya magharibi ni sehemu iliyokuwa nyuma kiuchumi lakini inaharakisha hatua zake za maendeleo ya kiuchumi kutokana na kuhimizwa na sera husika za serikali, ila sehemu ya kati inaonekana kama imesahauliwa. Hivi sasa sehemu ya kati ya China imeanza kushuhudia maendeleo ya uchumi wa taifa, na imechukua hatua mbalimbali kuharakisha hatua zake za maendeleo ya uchumi kwa kutumia nafasi nzuri ambayo serikali kuu inasawazisha maendeleo ya uchumi ya maeneo mbalimbali na kufanya marekebisho ya muundo wa uchumi.

Eneo la kustawisha uchumi na teknolojia la Nanchang mkoani Jiangxi, sehemu ya kati ya China, ni moja ya maeneo muhimu ya maendeleo ya uchumi mkoani humo. Hivi sasa eneo hilo linafanya ushirikiano na mikoa ya jirani iliyoko kwenye sehemu ya pwani katika sekta ya uchukuzi na kutafuta njia mpya za kuhimiza maendeleo ya uchumi wa sehemu ya kati ya China.

Naibu mkurugenzi wa kamati ya usimamizi wa eneo la kustawisha uchumi bibi Deng Yuhui, akiongoza waandishi wa habari kutembelea kampuni moja ya uchukuzi alisema,

"Hapa kwetu hakuna bandari, katika miaka ya karibuni serikali ya mji ilitoa wazo la 'bandari isiyo na maji', yaani kujenga njia moja ya mkato inayoingia baharini kwa kufanya ushirikiano na miji mingine kama ya Shenzhen, Xiamen, Ningbo na Shanghai, na kurefusha huduma nzuri ya forodha ya miji ya pwani hadi sehemu ya ndani ya China."

Mtindo wa ushirikiano wa uchumi wa eneo la kustawisha uchumi na tekinolojia la Nanchang unaigwa polepole na sehemu nyingine za mkoa huo wa Jiangxi. Mkoa wa Jiangxi ni mkoa pekee unaopakana na delta ya mto Changjiang na delta ya mto Lulu, sehemu zilizoendelea kiuchumi nchini China. Pamoja na maendeleo ya uchumi ya sehemu zilizoendelea za pwani na marekebisho ya muundo sekta ya uzalishaji mali, mkoa wa jiangxi unatumia ipasavyo fursa hiyo nzuri na kukuza uchumi wake kwa kutumia sekta ya uzalishaji mali iliyohamia mkoani humo kutoka sehemu za nje pamoja na maliasili na rasilimali zake.

Mbinu hiyo ya mkoa wa Jiangxi ni njia muhimu ya kukuza uchumi ya mikoa iliyoko sehemu ya kati ya China. Mikoa 6 ya China iko katika sehemu ya kati ambayo inapakana na mikoa ya sehemu ya pwani isipokuwa mkoa wa Hubei.

Kuanzia mwaka 2004, mikoa mbalimbali ya sehemu ya kati ya China iliimarisha ushirikiano wa kiuchumi na sehemu iliyoendelea ya pwani. Hivi sasa mzunguko wa uchumi wa delta ya mto Lulu umeendelezwa hadi kufikia baadhi ya sehemu za mikoa ya Hunan na Jianxi; Mikoa ya Anhui na Hubei imejenga ushirikiano na mzunguko wa uchumi wa delta ya mto Changjiang; Mikoa ya Shanxi na Henan inajitahidi kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na sehemu nyingine zilizoendelea za pwani ya China. Kutokana na kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya sehemu ya kati na sehemu ya pwani, sehemu hiyo itapata misaada mingi zaidi ya fedha na teknolojia katika maendeleo ya uchumi wake, vilevile itachangia marekebisho ya muundo wa sekta zake za uzalishaji.

Aidha, sehemu ya kati ya China imeimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya sehemu hiyo na mikoa mingine ya China. Mkuu wa mkoa wa Jiangxi Bw. Huang Zhiquan alipoeleza mbinu ya mkoa wao alisema kuwa, katika maendeleo ya mkoa wa Jiangxi ushirikiano katika sekta za uzalishaji mali ni kitu muhimu sana.

"Katika mambo ya kilimo ikiwemo miundo-mbinu ya kilimo, tumekuwa na uhusiano mkubwa na mikoa ya Hunan na Hubei. Katika upande wa nishati, nusu ya kiasi cha makaa ya mawe yanayohitajiwa na mkoa wa Jiangxi inatoka mikoa ya Anhui, Shanxi na Henan. Vilevile maliasili nyingi za mkoa wetu zikiwemo shaba na tungsten zinasafirishwa kwenda kwenye mikoa mingine ya sehemu ya kati."

Hivi sasa mikoa mingine ya sehemu ya kati inazingatia sana kukuza uwezo wake wa ushindani katika maendeleo ya uchumi. Tokea muda mrefu uliopita, sehemu ya kati ilikuwa kituo muhimu cha viwanda, kilimo na nishati, baadhi ya mikoa ilikuwa viunganisho vya mawasiliano na vituo muhimu vya usambazaji bidhaa. Ni katika miaka ya karibuni tu, ambapo mikoa ya sehemu ya kati imekuwa nyuma katika maendeleo ya uchumi. Kwa mfano, mkoa wa Hubei ulikuwa mkoa ulioendelea. Mwaka 1984 mkoa wa Hubei ulichukua nafasi ya 6 katika maendeleo ya uchumi hapa nchini, lakini katika miaka ya karibuni mkoa huo ulichukua nafasi ya 10 hivi.

Alipozungumzia sera zinazobuniwa, ofisa wa serikali ya mkoa wa Hubei Bw. Zhang Changer alisema kuwa, kuhimiza maendeleo ya uchumi wa sehemu za pembezoni kwa kutegemea miji muhimu, ni mbinu nzuri ya kukuza uchumi wa kikanda. Katika muda mrefu uliopita, mji mkuu wa mkoa wa Hubei, Wuhan, ulikuwa kituo cha viwanda nchini China na pia ulikuwa mji muhimu wa biashara. Hivyo mkoa wa Hubei unajitahidi kujenga mzunguko wa uchumi wenye eneo la kilomita 100 ambao una miji 8 na kitovu chake ni mji wa Wuhan. Nguvu ya uchumi ya mzunguko huo inazidi nusu ya nguvu ya uchumi wa mkoa wa Hubei.

"Mkoa mzima unatakiwa kuunga mkono kuharakisha ujenzi wa mzunguko wa uchumi wa mji wa Wuhan, tunatakiwa kukuza nguvu ya mji wa Wuhan. Hivi sasa viwanda na kampuni nyingi zimehamia Wuhan. Kwa upande mwingine tunatakiwa kuimarisha ujenzi wa miundo-mbinu ya eneo hilo la uchumi na mpango wa sekta zake za uzalishaji mali."

Bw. Zhang Changer aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kutokana na ujenzi wa mzunguko wa uchumi wa mji wa Wuhan, watakamilisha muundo wa uzalishaji mali ambao mji wa Wuhan utakuwa sehemu ya utafiti na teknolojia, na sehemu nyingine za pembezoni mwake zitakuwa za nguvukazi. Wakati huo muundo wa sekta ya uzalishaji mali ya Wuhan itaboreshwa zaidi na kuwa kitovu cha wataalamu, usafirishaji bidhaa, upashanaji habari na mzunguko wa mitaji cha mzunguko huo wa uchumi. Hivi sasa ujenzi wa barabara za kasi kati ya Wuhan na miji mingine ya mzunguko huo wa uchumi umeanza na utakamilika mwaka 2007. Wakati huo mawasiliano kati ya mji wa Wuhan na miji mingine 8 yatahitaji saa 1 hivi kwa gari.

Miji mingi ya sehemu ya kati ya China ni ya kilimo. Kutokana na kilimo chake kutokuwa cha kisasa, pato la wakulima bado ni la chini, hali ambayo imekuwa kikwazo kwa maendeleo ya uchumi wa sehemu ya kati. Katika miaka ya karibuni, serikali ya China katika ngazi mbalimbali zimebuni sera kadhaa nafuu za kuhimiza maendeleo ya kilimo.

Habari zinasema kuwa hata hivyo, sehemu ya kati bado ina ubora wa rasilimali katika maendeleo ya uchumi. Kwa mfano, mkoa wa Shanxi unachukua nafasi ya kwanza kwa wingi wa utoaji wa makaa ya mawe hapa nchini; mikoa ya Jiangxi, Hubei na Anhui ina maliasili nyingi ya madini; mkoa wa Henan ni mkoa wa kwanza kwa wingi wa idadi ya watu na nguvukazi. Ubora huo utanufaisha maendeleo ya uchumi ya sehemu ya kati ya China.

Kijiografia, sehemu ya kati ina ubora wake. Njia mbili za reli ambazo ni kutoka Beijing hadi mji wa Guangzhou na kutoka Beijing hadi Hong Kong zinapita kwenye sehemu hiyo; Mito miwili muhimu kabisa nchini China ya Changjiang na mto Manjano vilevile inapita kwenye sehemu hiyo. Pamoja na kuimarika kwa nguvu ustawishaji kuhusu sehemu ya magharibi na sehemu ya kaskazini mashariki za China, sehemu ya kati ya China itafanya kazi muhimu za kuhimiza kuimarisha uhusiano wa kiuchumi kati ya sehemu ya mashariki na magharibi na kati ya kusini na kaskazini.

Idhaa ya kiswahili 2005-11-29