Tarehe 27 Novemba mwaka huu mkutano wa mawaziri wa elimu wa China na Afrika ulifanyika hapa Beijing, mawaziri wa elimu kutoka nchi 17 za Afrika akiwemo waziri Joseph J. Mungai wa Tanzania walihudhuria mkutano huo. Baada ya mkutano mwandishi wetu wa habari alipata fursa ya kufanya mahojiano na Bw. Mungai kuhusu sera ya elimu ya Tanzania na jinsi serikali ya Tanzania inavyochukua hatua kueneza elimu ya msingi kwa watoto wote.
Bw. Mungai alisema kuwa, sera ya elimu ya Tanzania ni elimu ya msingi kwa watoto wote wenye rika la umri wa miaka 7 hadi 13, yaani elimu ya msingi ya bure, asilimia 50 ya watoto wenye rika la umri wa miaka 14 hadi 19 wasome shule ya sekondari ifikapo mwaka 2010. Akisema:
"Sera ya elimu ya Tanzania ni elimu ya msingi kwa watoto wote, tumechukua hatua katika sheria kwamba ni lazima mtoto akifika miaka saba aandikishwe kuanza darasa la kwanza, na kutokufanya hivyo ni kosa la jinai. Kwa sababu tumeifanya elimu ya msingi kuwa ya bure, wazazi hawawezi kuwanyima watoto wao fursa ya kwenda shule kwa kizingisio cha kutokuwa na pesa. Na ndiyo maana kiasi cha watoto wanaosoma shuleni kimeongezeka kwa kasi, kuanzia asilimia 58 ya mwaka 2000 hadi asilimia 95 ya mwaka huu."
"Kwa ngazi ya sekondari, mwaka 2000 asilimia 6 ya watoto walisoma katika shule ya sekondari, na kiasi hicho kimeongezeka kufikia asilimia 12 mwaka huu, na ifikapo mwaka 2010 angalau nusu ya watoto wataweza kusoma shule za sekondari. Na elimu ya sekondari kwa 50 % ya watoto wote tunataka iwe na usawa kwa jinsia zote kwa wavulana na wasichana. Baada ya hapo ndiyo tunaandaa mpango mwingine wa kuifikisha elimu ya sekondari kwa watoto wote."
Bw. Mungai alisema kuwa, wanafunzi wa Tanzania wanatakiwa kufanya mitihani ya taifa katika darasa la saba, kidato cha nne na kidato cha sita. Wakifaulu mtihani wa taifa wa kidato cha sita, wataweza kujiunga na chuo kikuu.
Bw. Mungai alisema katika miaka hii mitano iliyopita, Tanzania imeongeza uandikishaji wa watoto wenye rika la miaka 7 hadi 13 katika shule za msingi, pia imeanzisha mpango mkubwa wa kupanua elimu ya sekondari, lakini kutokana na matatizo ya kiuchumi, imekumbwa na upungufu mkubwa wa miundo mbinu ambayo ni pamoja na shule, madarasa, maabara na walimu. Pia Tanzania ina asilimia 5 ya watoto ambao hawawezi kwenda shule kutokana na sababu mbalimbali. Watoto hao wako katika visiwa vilivyo mbali, maeneo ya delta, maeneo yasiyofikika kwa urahisi, hasa kwa wafugaji wanaohamahama, watoto wa makabila mengine kama kabila la Wahadzabe ambao hawafugi, hawalimi, wanaishi kwa kutegemea matunda ya porini na kuwinda, na watoto walemavu. Tanzania bado ina tatizo la kutoa elimu ya msingi kwa watoto walemavu.
Idhaa ya kiswahili 2005-11-29
|