Kwenye mlima mkubwa wa Wuling ulioko mkoani Hunan, katikati ya China kuna aina nyingi za mimea, na aina moja ya miti hiyo ni ya chai tamu ya porini.
Bw. Hu Yingxiang mwenye umri wa miaka 52 mwaka huu na familia yake wanaishi katika sehemu hiyo ya mlimani. Japokuwa Bw. Hu Yingxiang alipata elimu ya shule ya msingi tu, lakini ana akili nyingi, alitangulia kujipatia maendeleo ya kiuchumi kwa kufungua duka la kuuzia vitu vya lazima ya maisha miaka kumi iliyopita.
Lakini mwaka 1996, mafuriko yaliyotokea katika sehemu ya Wuling, yalibadilisha maisha ya Bw. Hu Yingxiang, nyumba yake ilibomolewa na mimea yote iliyokuwa shambani iliharibiwa, ni miti iliyokuwa mlimani peke yake ndiyo iliyoendelea kustawi. Kuanzia hapo Bw. Hu Yingxiang alizingatia kuendeleza chai pori tamu iliyoota mlimani kwa wingi. Akisema:
"Hali ya hewa na udongo maalum wa nyumbani kwetu unafaa kwa miti ya chai ya porini kuota, majani yake yakitafunwa ladha yake ni tamu sana na tena yanasaidia kuondoa joto na kiu."
Mti pori wa chai unaoota kwenye mlima wa Wuling una urefu wa mita mbili. Wanavijiji wa huko wanapofanya kazi mlimani hukata kiu kwa kutafuna majani ya miti ya chai ya porini. Japokuwa miti hiyo imekuwepo na wanavijiji kizazi hadi kizazi, lakini wenyeji wa huku walikuwa na ufahamu mdogo kuhusu miti hiyo.
Baada ya kupata wazo la kuendeleza miti ya chai ya porini, Bw. Hu Yingxiang alianza kuchunguza sifa ya miti hiyo, akagundua kuwa majani ya miti hiyo yanaweza kupunguza shinikizo ya damu, kuongeza uwezo wa mwili wa kujikinga, kulinda maini, kuongeza urembo na kuzuia binadamu wasizeeke haraka.
Bw. Hu Yingxiang alikopa Yuan elfu 80 kuanzisha kiwanda cha kutengeneza chai tamu inayotokana na miti ya porini. Chai hiyo inakaribishwa sana na wateja, baada ya mwaka mmoja tu alirudisha fedha zote alizokopa. Mtaalamu maarufu wa chai wa China Bwana Chen Liangbin baada ya kufanya uchunguzi kuhusu sifa za chai hiyo alisema kwa furaha kuwa:
"Chai hiyo ina ufanisi maalum katika kuongeza uwezo wa mwili wa kujikinga na kupunguza sukari kwenye damu, inaweza kuondoa joto mwilini na inaweza kuzuia maumivu ya meno."
Bw. Hu Yingxiang amefanya juhudi kubwa katika kupata ustadi wa kutengeneza chai bora na kuotesha miti bora.
Kwa kuwa miti hiyo ya chai ina sukari nyingi, ni rahisi kuharibiwa na vijidudu. Baada ya kufanya utafiti na majaribio mara nyingi Bw. Hu Yingxiang hatimaye amefaulu kupata mbinu mbili za kuotesha miti hiyo shambani, yaani kupandikiza matawi ya miti pori ya chai wakati wa majira ya mchipuko, au kuotesha miche kwa mbegu. Hivi sasa Bw. Hu Yingxiang amejenga shamba lenye hekta 6 la kuotesha miche ya miti chai. Alisema kupanda miti hiyo ya chai si kama tu kunaweza kukipatia chai kiwanda chake, bali pia kunasaidia kuzuia maporomoko ya udongo na mafuriko.
Kiwanda cha chai cha Hu Yingxiang kimeleta manufaa kwa wanakijiji. Yeye ananunua majani ya chai kutoka kwa wanakijiji, pia anawafundisha jinsi ya kuotesha na kutunza miti ya chai.
Bw. Yang Jiancheng anayeishi katika kijiji kimoja na Bw. Hu Yingxiang anafanya biashara ya majani ya chai yaliyotengenezwa kwenye kiwanda cha Bw. Hu Yingxiang. Amefungua duka maalum la kuuza chai tamu ya porini katika mji mkuu wa wilayani, alisema watu wengi wanapenda ladha tamu ya kiasili ya chai hiyo inayotokana na miti ya porini. Akisema:
"Chai tamu inayotengenezwa kutokana na miti ya porini inauzwa vizuri katika mji wa wilaya, watu wengi wanatumia chai hiyo siku zote, kutokana na sifa yake ya kurekebisha shinikizo la damu na kujenga afya. "
Bw. Hu Yingxiang amesajili nembo ya chapa ya "Dashuao" kwa chai yake. Mwezi Mei mwaka jana, chai yake ilitunukiwa medali ya dhahabu kwenye maonesho ya matokeo ya sayansi na teknolojia ya mkoa wa Hunan. Chai yake imesafirishwa hadi nchi za nje ambazo ni pamoja na Japan na Marekani. Sasa Bw. Hu Yingxiang yuko mbioni kuendeleza bidhaa nyingine za chai tamu ya porini, kama vile vinywaji vya chai tamu, na pombe ya chai.
Idhaa ya kiswahili 2005-12-01
|