Tarehe 27 mwezi Novemba, mawaziri wa elimu wa China na nchi 17 za Afrika walihudhuria mkutano wa Baraza la Mwaka 2005 la Mawaziri wa Elimu wa China na Afrika uliofanyika hapa Beijing. Kwenye mkutano huo, mawaziri hao walisaini Taarifa ya Beijing, na kukubaliana kuhusu kuimarisha ushirikiano na maingiliano ya elimu kati ya pande hizo mbili.
Katibu wa kudumu wa wizara ya elimu ya Kenya Bw. George Godia, aliiwakilisha Kenya kuhudhuria mkutano huo. Baada ya Mkutano huo, mwandishi wetu wa habari alipata fursa ya kufanya mahojiano na Bw. Godia. Yafuatayo ni mahojiano hayo.
CRI: Bw. Godia, tunajua Kenya na China zina uhusiano mzuri, na zinafanya ushirikiano katika nyanja mbalimbali, ningependa kujua ushirikiano kwenye mambo ya elimu kati ya nchi hizo mbili kwa sasa ukoje?
Bw Godia: Katika Upande wa kisiasa, nafuraha kuona kuwa waziri wa China alitembelea nchini Kenya, na mheshimiwa rais Kibaki pia alifanya ziara nchini China mwaka huu, kutembeleana kwa viongozi wa nchi hizo mbili kuna umuhimu kwa uhusiano wa nchi hizo mbili, na kwa upande wa teknolojia, kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa leo, maofisa wa elimu wa nchi hizo mbili watatembeleana zaidi, ili kuhimiza maendeleo ya elimu ya nchi mbili.
CRI: Bw. Godia, kama tunavyojua, serikali za Kenya na China zinachukua hatua mbalimbali ili kuimarisha ushirikiano wa elimu kati yao, kwa mfano, serikali ya Kenya ilianzisha misaada mbalimbali ya masomo, yaani Scholarship, ili kuwasaidia wanafunzi wa Kenya kusoma katika nchi za nje, ikiwemo China. Ningependa kujua ni utaratibu gani mnaotumia kutoa hizo Scholarship kwa wanafunzi, na mbali na hilo, Kenya inaendeleza vipi ushirikiano wa elimu kati yake na China?
Bw. Godia: hivi sasa, China imeipatia Kenya Scholarship 10, lakini kutokana na mahitaji mengi ya wanafunzi, katika mkutano wa leo tumekibaliana kuongeza Scholarship hizo hadi 20 kutoka 10 kwa mwaka, na leo pia tulijadili ushirikiano kati ya Kenya na China, kwa mfano, kupelekeana wanafunzi na walimu.
CRI: Katika muda ambao umekuwepo hapa China, umepata habari zozote kuhusu wanafunzi wa Kenya wanaosoma hapa? Tafadhali tuelezee kidogo hali yao ya maisha na masomo.
Bw. Godia: Nimeongea na balozi wetu nchini China, na nimeambiwa kuwa hakuna matatizo kwao, na kitu muhimu kwa sasa ni kujaribu kuongeza Scholarship. Pia wakati nilipotembelea Chuo Kikuu cha Beijing, nimewakuta wanafunzi wa Kenya wanaosoma huko wanasoma vizuri, na nimeambiwa kuwa masomo waliyoyapata hapa ni ya maana.
CRI: Bw. Godia, nimeambiwa kuwa hii ni mara yako ya kwanza kuja hapa China, katika ziara yako hii umepata picha gani kuhusu China na watu wake?
Bw. Godia: Hii ni mara yangu ya kwanza kuja hapa China, nilitembelea sehemu za kihistoria na kutazama Opera, tunakaribishwa vizuri, tunatunzwa vizuri, nimeona kuwa China ni nchi ambayo watu wake ni wenye heshima, viongozi wanaheshimiwa na vijana ni wa heshima, hali hii inaonesha kwamba masoma ya hapa China yanatilia maanani kuhimiza utamaduni, na utamaduni ni kitu muhimu kwa nchi moja.
CRI: Asante, Bw. Godia.
Idhaa ya Kiswahili 2005-12-02
|