Maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yanayotokea kwenye baadhi ya sehemu nchini China yameleta shinikizo kwa sekta ya ufugaji. Hivi sasa China inachinja kuku na mabata wanaofugwa kwenye maeneo ya kilomita 3 kutoka mahali panapotokewa na maradhi ya homa ya mafua ya ndege na kuwapa chanjo kuku na mabata wanaofugwa kwenye sehemu ambazo bado hazijakumbwa na maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, ili kuzuia kuenea kwa maambukizi ya maradhi hayo. Basi hivi sasa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yameleta athari gani kwa sekta ya ufugaji wa kuku na mabata? Na hatua gani zimechukuliwa na China dhidi ya maambukizi hayo ili kuhakikisha maendeleo ya sekta hiyo?
Bw. Liu Yuxiang ni mkulima wa wilaya ya Heishan mkoani Liaoning, sehemu ya kaskazini mashariki ya China. Mwaka huu amefuga kuku 1,000 wa mayai na anapata kilo zaidi ya 50 za mayai kwa siku. Katika miezi mitatu kabla ya kutokea maambukizi ya homa ya mafua ya ndege kuku wake walimletea Yuan kiasi cha 3,000. Bahati mbaya mahali anapoishi pako ndani ya umbali wa kilomita 3 kutoka mahali penye maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, hivyo kuku wake 1,000 walioko kwenye kipindi cha kutaga mayai kwa wingi, walichinjwa bila kumbakiza hata mmoja ndani ya saa 1.
Kutokana na hayo, familia ya Liu Yuxiang ilipata fidia ya Yuan elfu 10 kutoka kwa serikali.
"Nimeridhika na fidia niliyopewa. Lengo la hatua inayochukuliwa na serikali ya kuchinja kuku na mabata ni kwa ajili ya afya ya umma, tukiwa salama kabisa tutakuwa na nafasi ya kuchuma pesa. Nafikiri baadaye tukitaka kuendelea kufuga kuku, bila shaka serikali itatuunga mkono."
Serikali inatoa fidia kwa kuku na mabata wanaochinjwa, ambayo imetusaidia kupunguza hasara tunayoingia. Hivi sasa Liu Yuxiang anafuatilia sana mwelekeo wa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege. Anatarajia kuwa serikali itaweza kufanikiwa kudhibiti haraka iwezekanavyo maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, ili familia za wakulima wanaotegemea shughuli za ufugaji ziweze kuendelea kufanya shughuli za ufugaji na kupata faida kutokana na mauzo ya mayai.
Hadi tarehe 29 mwezi Novemba, matukio 29 ya maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yametokea katika mikoa 10 nchini ambapo zaidi ya milioni 20 za kuku na mabata wamechinjwa.
Hivi sasa serikali ya China imeamua kutoa chanjo kwa kuku na mabata ambao bado hawajaambukizwa virusi vya maradhi hayo. Mganga mkuu wa mifugo wa wizara ya kilimo ya China Bw. Jia Youling hivi karibuni alisema kuwa zaidi ya 60% ya kuku na mabata nchini wamepewa chanjo, inakadiriwa kwamba baada ya chanjo hizo kuanza kufanya kazi, maambukizi ya homa ya mafua ya ndege nchini yatadhibitiwa. Ili kuhakikisha ufanisi wa chanjo hizo, serikali imetoa maagizo makali kuhusu ubora wa chanjo za aina hiyo.
"Hivi karibuni wizara ya kilimo imeimarisha usimamizi kuhusu uzalishaji na usambazaji wa chanjo za kinga ya maambukizi ya ugonjwa huo, kutoa adhabu kali kwa uzalishaji na uuzaji wa chanjo za utapeli. Chanjo za homa ya mafua ya ndege zinazozalishwa nchini China zinafuata kabisa kigezo cha Shirika la Magonjwa ya Kuambukiza Duniani, OIE, ambayo ilifanya ukaguzi mara nyingi katika idara za utafiti na viwanda vya uzalishaji wa chanjo hizo, na imetoa pongezi."
Habari zinasema kuwa hivi sasa China imechagua viwanda 9 kutengeneza chanjo ya homa ya mafua ya ndege, ambavyo uzalishaji wake umefikia chanjo bilioni 16 kwa mwaka na kuweza kutosheleza mahitaji ya nchini.
Kutokana na maambukizi ya homa ya mafua ya ndege yaliyotokea kwenye baadhi ya sehemu za China, hivi sasa masoko mengi ya mazao ya kilimo yakiwemo ya Beijing yamesimamisha biashara ya kuku na mabata waliohai.
Soko la chakula cha mbuga ya malisho lililoko kwenye mji wa Huhehaote, mji mkuu unaojiendesha wa mkoa wa Mongolia ya ndani, sehemu ya kaskazini ya China ni moja ya masoko ya mazao ya kilimo ya mji huo. Katika mji huo biashara ya kuku na mabata waliohai imesimamishwa. Kwenye ukumbi wa kuuzia chakula kinachohifadhiwa kwa barafu, ingawa bado kuna wafanyabiashara wengi wanaouza nyama za kuku zilizohifadhiwa kwa barafu, ambazo zilikaguliwa na idara ya karantini, lakini nyama hizo zinauzwa kidogo tu. Mfanyabiashara mmoja wa soko hilo bibi Zhang Lixiang alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema,
"Hapo nyuma kila siku niliuza za nyama za kuku na kupata Yuan 200 au 300 hivi, lakini sasa watu wachache sana wananunua nyama za kuku."
Kuhusu hali hiyo ya watu wachache kununua nyama za kuku na mabata kutokana na kuathiriwa na maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, idara husika ya serikali pamoja na sekta za ufugaji, usindikaji na uuzaji wa rejareja zinaimarisha udhibiti wa maambukizi ya maradhi hayo na kuongeza imani ya watu ya kutumia nyama za kuku na mabata.
Ili kudhibiti ipasavyo maambukizi makubwa ya mifugo yakiwemo maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, tarehe 21 mwezi Novemba China ilitoa "Kanuni za dharura kuhusu maambukizi makubwa ya mifugo" ambazo zimeagiza utaratibu kuhusu mpango unaotakiwa kufuatwa wakati wa dharura, usimamizi, upimaji na utoaji taarifa kuhusu maambukizi ya maradhi ili kutoa dhamana kwa utaratibu katika kuzuia hatari ya maambukizi ya homa ya mafua ya ndege. Licha ya hayo, serikali ya China imetoa ruzuku za aina 9 za kusaidia maendeleo ya ufugaji wa kuku na mabata, ikiwemo ya kuchinja kuku na mabata wanaofugwa kwenye maeneo yenye maambukizi ya homa ya mafua ya ndege, kusamehe kodi za mwaka za viwanda husika, kusamehe malipo ya ukaguzi wa karantini juu ya nyama za kuku zinazosafirishwa nchi za nje na utaratibu wa taifa wa kuweka akiba ya chanjo.
Shida iliyopo hivi sasa katika udhibiti wa maambukizi ya homa ya mafua ya ndege ni kuwa familia za wakulima wa ufugaji kuku hazikuwa katika mahali pamoja, wataalamu wanaona kwamba mtindo huo wa ufugaji umeleta matatizo wakati wa kudhibiti maambukizi ya homa ya mafua ya ndege. Profesa wa kitivo cha uchumi wa kilimo cha chuo kikuu cha wananchi cha China Bw. Zeng Yinchu alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, "Kwa muda wa hivi sasa, jambo tunalopaswa kufanya ni kudhibiti barabara maambukizi ya homa ya mafua ya ndege. Lakini kutupia macho siku za baadaye tunatakiwa kubadilisha mtindo wa ufugaji kuku katika familia za wakulima, ambao ni vigumu kudhibiti maambukizi ya maradhi.
Mtaalamu huyo alisema kuwa kutokana na hali halisi kwamba katika muda mfupi ujao China haiwezi kubadilisha kabisa mtindo wa ufugaji kuku wa familia za wakulima, idara husika zinatakiwa kubuni kanuni za udhibiti wa mazingira ya ufugaji, lishe bora ya kuku na mbinu ya kuzuia maambukizi ya maradhi ya kuku, na kubuni mikakati ya kueneza teknolojia ya kisayansi ili kuboresha mazingira na teknolojia ya ufugaji na udhibiti wa maambukizi ya maradhi ya kuku.
Hivi sasa sehemu mbalimbali za China zinajitahidi kudhibiti kuenea kwa homa ya mafua ya ndege, ili kupunguza athari yake dhidi ya sekta ya ufugaji wa kuku. Baadhi ya sehemu nchini zimetoa mikopo midogo kwa familia za ufugaji na kuhimiza kampuni kununua kuku wa wakulima wafugaji, ili kuwachinja na kuuza kwa pamoja na kupunguza hasara ya wakulima wafugaji wa kuku.
Idhaa ya kiswahili 2005-12-06
|