Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-06 15:43:10    
Barua 1206

cri
Msikilizaji wetu Stephen Magoye Kumalija, wa Kiliwi shule ya msingi, Mwamashimba Division, P.O.Box 1421 Mwanza, Tanzania anasema katika barua yake kuwa, ni matumaini yake kuwa wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa kutoka mjini Beijing China hatujambo, hali yake ni nzuri na anaendelea kuitegea sikio Radio China Kimataifa inayowatangazia kutoka mjini Beijing nchini Jamhuri ya watu wa China.

Anasema anapenda kutumia fursa hii kutoa pole kwa marafiki zake wa China kutokana na janga baya kabisa la kimbunga lilitokea huko kusini mashariki mwa nchi ya China pamoja na kisiwani Taiwan kikiwa ni miliki ya umma wa China. Pia anatoa pole kutokana na maafa ya mvua kubwa sana iliyotokea miezi michache iliyopita ikiambatana na upepo mkali, na kuleta madhara kwenye kisiwa cha Taiwani pamoja na miji mbalimbali ya Jamhuri ya Watu wa China kama vile Shanghai. Anasema, poleni sana marafiki zangu, kwani dunia ndivyo ilivyo. Na anatutakia kila la kheri wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa, ufanisi na baraka tele.

Tunamshukuru kwa dhati kwa barua yake ya kutuletea salamu.

Msikilizaji wetu Isaac Nikitah Barasah (Macharia), Sanduku la Posta 1129, Bungoma, Kenya anasema katika barua yake kuwa, anayo furaha isiyo na kifani akiandika waraka huu akitumai kuwa sisi ni bukheri wa afya, na tunaendelea kuchapa kazi bila kusita. Hata hivyo, anatoa wingi wa shukurani kwa barua pamoja na nakala ya maswali ya chemsha bongo ambayo tulimtumia.

Anasema ilikuwa kama ni heshima kubwa sana kwake kupewa fursa ya kushiriki, kuwasiliana na hata kutuma salamu kwa wapendwa bila malipo yoyote. Hapo Kenya pasipokuwa na kununua kadi za salamu pamoja na kulipa kiasi fulani cha pesa, hakuna salamu wala mawasiliano. Hana budi kusema Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa ni idhaa ya kipekee.

Anasema yeye husikiliza idhaa hii kwa makini sana, anayo matumaini ya kutembelea China kama ataibuka mshindi kwa shindano la chemsha bongo. Ingawa yeye ni msikilizaji mgeni lakini anawashukuru sana wasikilizaji kama Mutanda Ayub Sharrif ambao walimfanya ajiunge na idhaa hii ya Radio China kimataifa.

Anasema heko wafanyakazi na watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, anatuomba tuendelee kuimarisha tovuti yetu kwa kila nchi ulimwenguni. Na kama kukiwa na nafasi anaomba tusisahau kutembelea Bungoma Kenya ambapo mashabiki kama Bwana Mutanda Ayub Sharif, Joyce, Hellen na Dan wana hamu kubwa ya kutuona ana kwa ana. Pia anawaomba mashabiki wa kila nchi waunde vyama ili waweze kufanya kazi na kuwasiliana pamoja kwani umoja ni nguvu.

Anasema, yeye ni kijana Mkenya mwenye umri wa miaka 22. Bado ana nguvu za kufanya kazi na kuwasiliana nasi bila uvivu wowote. Yuko nasi pamoja hapo Bungoma Kenya kutoka awali mpaka akheri, ili kuiboresha idhaa yetu ya Radio China Kimataifa. Anatutakia Maulana awe nasi ili tuendelee kuchapa kazi kwa moyo wote.

Msikilizaji wetu Mbaraka Mohammed Abucheri wa sanduku la posta 792 Kakamega, Kenya kwenye barua yake anataka tukpokee salamu zake, akitarajia kuwa hapa Beijing sote ni. Yeye huko Kakamega ni mzima wa afya njema, akiendelea na shughuli za ujenzi wa taifa lake la Kenya, bila kusahau kusikiliza vipindi na habari kochokocho zinazowafikia kwa njia mwafaka kutoka Radio China Kimataifa. Yeye hana budi kutushukuru na kutupongeza kwa ufanisi wetu hasa katika mwaka wa 2005, kwanza utayarishaji na utangazaji wa vipindi mbalimbali.

Anasema kwa hakika tumefanya juhudi na kazi kubwa na nzuri mno ya kuwaletea vipindi murua vya kutosheleza mahitaji ya wasikilizaji kote duniani, pili katika mwaka 2005 wasikilizaji wetu walitumiwa zawadi nzuri na wasimamizi wa idhaa waliweza kuchapishwa jarida liitwalo "Daraja la urafiki" ambalo lilitoa makala na habari zenye kuaminika na kuelimisha kwa wasomaji na wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa, haya ni mafanikio muhimu. Pia anasema mafanikio mengine ni kwa wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wa Afrika Mashariki, hasa wa hapo nchini Kenya walitunukiwa zawadi na heshima kubwa ya kuongezewa muda wa matangazo ya vipindi vinavyopitia shirika la utangazaji la Kenya KBC kwa saa moja badala ya nusu saa ya siku zilizopita.

Kutokana na hayo anapenda kutoa shukurani zake za dhati kwa wasimamizi wa Radio China Kimataifa na wale wa idhaa ya taifa ya KBC kwa hatua hii bora na mwafaka. Anaomba ushirikiano huu kati ya Radio China Kimataifa na idhaa ya taifa KBC udumishwe na kuimarishwa zaidi kwa manufaa ya wasikilizaji, kwa kufanywa mawasiliano na ziara za mara kwa mara ili kuboresha utoaji huduma na matangazo ya vipindi vya kuvutia na kuelimisha.

Anaamini kwamba kupitia majadiliano na ziara za wakurugenzi wa mashirika haya mawili, kutakuwa na mafanikio na kujenga uhusiano mzuri kati ya raia wa mataifa haya mawili yaani taifa la China na Kenya, hivyo kufungua njia pana ya kubadilishana mawazo na kufanya biashara ili kuboresha uchumi wa mataifa haya. Pia anasema anapendekeza kuwa washindi wa chemsha bongo wa kuanzia mwaka 2006, 2007 na 2008 wapewe nafasi kuja nchini China kushuhudia michezo ya olimpiki itakayofanyika mwaka 2008. Hatua hii nafikiri itatoa changamoto kwa wasikilizaji wa Radio China Kimataifa kufanya juhudi kama mchwa na nyuki ili kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo kwa wingi, hivyo kuimarisha usikilizaji kote duniani.

Pendekezo lake lingine ni kuhusu washindi wa nafasi ya kwanza, pili na tatu. Anasema itakuwa vizuri kama hao watafikiriwa kwa kudhaminiwa kimasomo, kibiashara, kiufundi badala ya kupewa nafasi ya kuzuru China. Anasema anaamini kuwa mapendekezo yake yatachukuliwa kwa wema na kwa umuhimu mkubwa, ili yasaidie kuboresha matangazo ya Radio China..

Tunamshukuru sana kwa barua yake na ushauri wake

Msikilizaji wetu Stephen M. Kumalija sanduku la posta 1421 Mwanza Tanzania anasema katika barua yake kuwa, anapenda kutumia fursa hii akitupongeza wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa hususan idhaa ya Kiswahili kwa kazi nzuri tunazofanya hapa mjini Beijing China, kwa kuwaletea habari nzuri na nyeti kutoka kote duniani.

Pia anapenda kutumia fursa hii kutushukuru zawadi tulizomtumia pamoja na kadi zilizotokana na ushindi wake kwa kujipatia nafasi ya tatu kutokana na mashindano ya chemsha bongo kuhusu miaka hamsini na tano ya China mpya. Vilevile anapenda kutushukuru kutokana na imani yetu kuwa ataendelea kufuatilia matangazo yenu na tovuti yenu ya Kiswahili kwenye mtandao wa wakati halisi, yaani internet, na pia kwa kunijulisha kuwa mtafanya juhudi za kutafuta fursa mbalimbali ili wasikilizaji wenu bora kama mimi tatuweza kutimiza matumaini yetu ya kuitembelea China hususan Radio China Kimataifa. Anamaliza barua yake kwa kutuambia kuwa ametutumia picha yake ndogo ili tuiweke kwenye mtandao wa internet na kuchapishwa kwenye gazeti la daraja la urafiki kwenye toleo lijalo..

Msikilizaji wetu Patrick Masika Okabo ambaye barua zake huhifadhiwa Lurende Market sanduku la posta 194, Bungoma Kenya Pokea kwanza anasema tupokee salamu za furaha kutoka kwake. Pia anasema anapenda kutumia fursa hii kushukuru kukubaliwa kuwa mmoja wa wanachama wa Radio China Kimataifa. Anasema amesoma jarida la daraja la urafiki na limemfurahisha sana anasema atafurahi kama akiendelea kupata jarida hilo. Na mwisho anasema anatutakia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa heri ya mwaka mpya ujao.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-06