Mkurugenzi wa kituo cha maendeleo ya afya cha shirika la afya duniani WHO huko Kobe nchini Japan Dr. Frederic Clazer tarehe 20 alisema huko Shanghai, China kuwa, kutokana na utandawazi wa uchumi duniani, maendeleo ya haraka ya utandawazi wa miji yamekuwa tishio baya kwa afya ya binadamu, lakini binadamu bado hawako tayari kukabiliana na tishio hilo.
Dr. Clazer alisema kuwa, hivi sasa karibu nusu ya watu duniani wanaishi mijini, lakini baada ya miaka 30, wengi wa watu duniani wataishi mijini, na kasi ya utandawazi wa miji itakuwa kubwa kabisa barani Afrika na Asia. Utandawazi wa kasi wa miji unasababisha kuwepo kwa sehemu nyingi za makazi zenye idadi kubwa ya watu na zisizopangwa vizuri. Dr. Clazer amekadiria kuwa, hivi sasa watu bilioni 3 wanaishi kwenye sehemu za mijini duniani, na kati ya watu hao, watu wapatao bilioni 1 wanaishi kwenye makazi ya watu maskini. Pia alisema kuwa, katika baadhi ya nchi, hali ya afya ya watu maskini mijini ni mbaya zaidi hata kuliko watu maskini vijijini. Aidha, pengo kati ya maskini na matajiri mijini bado linapanuka, na idadi ya watu maskini bado inaongezeka na hali yao imekuwa mbaya zaidi.
Kutokana na ongezeko la sehemu za makazi ya watu maskini na mazingira kuwa mabaya zaidi, baadhi ya miji imekuwa chanzo cha maambukizi ya magonjwa. Katika miji mingi, hewa, maji na ardhi zimechafuliwa vibaya, na miundo mbinu hafifu ya afya na ya kushughulikia takataka, upungufu wa maji safi ya kunywa ni vyanzo vikubwa vya mlipuko wa magonjwa. Aidha, hali ya hatari ya afya inayosababishwa na msongamano wa magari, na ajali za barabarani pia zinaongezeka. Dr. Clazer alisema, kula sana chakula cha haraka na kutofanya mazoezi ya kutosha ya kujenga mwili pia kunaweka athari mbaya kwa afya ya watu.
Dr. Clazer alisema kuwa, matumizi makubwa ya nishati mijini yamesababisha hali ya wasiwasi ya upungufu wa nishati duniani, na pia yameleta tishio kwa afya ya binadamu. Alisema kuwa, maendeleo yasiyo endelevu na matumizi ya ovyo ya nishati yameharibu mazingira na kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa.
Ingawa athari iliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya ya binadamu bado haijulikani, lakini inajulikana kuwa mabadiliko hayo bado yatakuwa ya haraka zaidi, na tishio la afya lisilotabilika siku hizi limeanza kutokea.
Bw. Clazer alisema kuwa, shirika la afya duniani WHO liliona kuwa, matokeo ya ongezeko la joto duniani litazidi kuwa makubwa siku hadi siku, na kuamini kuwa binadamu bado wana muda wa kutosha kukabiliana na hali mbaya, na hata kuzuia mazingira yasiendelee kuwa mabaya zaidi. Lakini matukio yaliyotokea hivi karibuni yameonesha kuwa, mabadiliko ya kimazingira yameleta athari kubwa mbaya. Matukio hayo ni pamoja na baadhi ya miji kukumbwa na joto kali, kimbunga, mafuriko na maporomoko ya ardhi.
Utandawazi wa uchumi duniani pia ni chanzo muhimu kwa afya ya binadamu. Dr. Clazer alisema kuwa, utandawazi umerahisisha maambukizi ya virusi katika nchi mbalimbali, na miji itakuwa chanzo cha mlipuko wa magonjwa katika nchi nzima. Katika miaka ya hivi karibuni, binadamu walikumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa SARS, na hivi sasa wanakabiliana na mlipuko wa homa ya mafua ya ndege.
|