Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-09 17:00:49    
China na nchi za Afrika zatafiti njia mpya ya ushirikiano katika nyanja ya elimu

cri

Tarehe 27 Novemba mwaka huu mkutano wa mawaziri wa elimu wa China na Afrika ulifanyika hapa Beijing. Mawaziri wa elimu kutoka nchi 18 za China na Afrika walibadilishana maoni, na kujadiliana kuhusu jinsi ya kustawisha elimu katika nchi zinazoendelea, na kutafiti njia mpya ya ushirikiano wa elimu kati ya pande hizo mbili. Waziri wa elimu na utamaduni wa Tanzania Bwana Joseph Mungai alisema:

"Mkutano huu umelenga kutazama sura mpya ya ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika. Imeonesha kwamba uongozi wa China na uongozi wa nchi za Afrika umeona haja ya kuwepo kwa ushirikiano mkubwa zaidi kati ya China na Afrika katika nyanja ya elimu. Huu ni mtizamo mpya kwa sababu huko nyuma miaka iliyopita, ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika ulikuwa zaidi katika maendeleo ya kiuchumi, ilitazama kwamba namna ya kuzisaidia nchi za Afrika ni kuzisaidia katika viwanda, mawasiliano na maendeleo ya kilimo.

Lakini mtizamo mpya na wa kisasa zaidi ni kwamba ushirikiano ukuzwe katika eneo la elimu. Sasa maendeleo ya elimu ni maendeleo ya kuongeza uwezo wa watu kufanya maendeleo kukuza uwezo wa raslimali ya nguvukazi. Huo ni msingi mzuri na nguzo ya kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Kwa miaka mingi tulikuwa tunaamini kwamba msingi au uti wa mgongo wa maendeleo ya nchi zetu ilikuwa ni kilimo, lakini kwa kweli tumegundua kuwa ili tuwe na maendeleo yanayodumu na yanayoleta maendeleo makubwa zaidi, mwanzo wake lazima ni kuwaendeleza watu wenye kufanya maendeleo."

Bw. Mungai alisema sera ya elimu ya Tanzania ni elimu ya msingi kwa watoto wote, na angalau nusu ya watoto wasome shule ya sekondari ifikapo mwaka 2010. Lakini kutokana na matatizo ya kiuchumi, Tanzania imekumbwa na upungufu mkubwa wa miundo mbinu ambayo ni pamoja na shule, madarasa, maabara na walimu. Anatumai kuwa China itaweza kuisaidia Tanzania katika miundo mbinu. Akisema:

"Kwanza China kwa miaka mingi imekuwa ikitusaidia katika maendeleo ya elimu kwa kutoa fursa kwa watu wetu kuja kusoma katika vyuo vikuu vya China. Lakini sasa tumeanza mazungumzo mapya, yaani Afrika tunahitaji elimu siyo ya msingi peke yake, pia tunahitaji elimu ya sekondari ipanuliwe iwafikie watoto wote. Uwezo wetu wa kiuchumi wa kuweka miundo mbinu inayohitajika ni mdogo. Hivyo tunatumai kuwa China itatusaidia katika kujenga maabara na kutusaidia kuwaandaa walimu wa ngazi mbalimbali.

"Katika maonesho yaliyofunguliwa siku hiyo nimeona vifaa vya maabara vinavyotengenezwa hapa China vinaweza kutosheleza kabisa mahitaji yetu. Sasa tunazungumzia kuhusu China kutusaidia kwa njia zipi. Ama itupe msaada ama kuweka katika mipango mbalimbali ya kukopeshana. Lakini nimeona China ina uwezo mkubwa sana kiteknolojia na kiufundi kuweza kutusaidia katika mahitaji yetu ya elimu."

Idhaa ya kiswahili 2005-12-09