Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-13 15:23:36    
China yafunga kibwebwe kutokomeza ubadhilifu na kuhifadhi mazingira ya asili

cri

Kuzima taa mtu anapoondoka, kufunga maji ya bomba barabara, kutotupa maganda ya matunda na vipande vya karatasi ovyo pamoja na kuzalisha na kutumia bidhaa zenye uwezo wa kuokoa nishati vitendo hivyo vinavyohusika na uokoaji wa raslimali na hifadhi ya mazingira, vimekuwa moja ya sehemu za shughuli za uzalishaji mali na maisha ya wachina wengi. Upungufu wa raslimali, kuchafuka na kuharibiwa kwa mazingira kutokana na maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, kumewafanya wachina kufahamu kuwa kuongeza ufanisi ya matumizi ya rasilimali na kuhifadhi mazingira ya asili ni muhimu sana kwa maendeleo endelevu ya uchumi wa China, kwa upande mwingine wametambua kwamba hatua hizo zinaweza kuboresha mazingira ya maisha yao.

Bw. Ding Guopei aliwahi kufanya shughuli za kununua vitu takataka vinavyoweza kutumika tena, na kuwa na karakana moja kukarabati mota mbovu na vipuri vya mitambo katika mji wa Taizhou mkoani Zhejiang, sehemu ya kusini mashariki ya China. Shughuli zake za biashara zilipata maendeleo ya kasi katika miaka ya karibuni, hivi sasa amenunua mitambo ya kisasa ya kusafisha aluminium kwa kutumia vitu vya takataka za aluminium anazonunua. Anapata faida zaidi ya Yuan milioni 3 za Renminbi katika kutumia hewa chafu iliyotolewa katika usafishaji wa aluminium takataka peke yake.

"Kumbe, nimefahamu hata hewa chafu ni kitu kinachoweza kutumika tena."

Habari zinasema kuwa hivi sasa mkoa wa Zhejiang umekuwa kituo cha ukusanyaji wa vitu takataka za madini, karatasi, plastiki na vioo vilivyovunjika, ambavyo vinaweza kuleta faida ya Yuan zaidi ya bilioni 45 kwa mwaka.

Baadhi ya viwanda vya China hivi sasa vinazingatia kurekebisha uzalishaji wa mazao ya jadi kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kupata njia mpya ya kuongeza ufanisi wa matumizi ya raslimali na nishati. Eneo la ustawishaji wa sayansi na tekinolojia la Zhongguancun lililoko mjini Beijing linasifiwa kama "Silicon valley ya China", ambalo lina viwanda na kampuni zaidi ya elfu. Hivi sasa viwanda vingi vya eneo hilo vinafanya utafiti kuhusu bidhaa mpya zinazoweza kupunguza matumizi ya rasilimali na nishati.

Kampuni ya Shidai ni kampuni iliyoanzishwa miaka zaidi ya 20 iliyopita huko Zhongguancun. Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo bibi Wang Xiaolan alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa sababu muhimu ya kampuni ya Shidai kupata maendeleo makubwa katika eneo la Zhongguancun ni kufanya utafiti na kuzalisha bidhaa za teknolojia ya kisasa zinazohitajiwa.

"Mashine za kuchomelea zinazozalishwa na kampuni ya Shidai zinatumika katika ujenzi wa majumba zaidi ya 10 ya michezo ya Olimpiki, ukiwemo uwanja wa michezo wa taifa unaojulikana kama mradi wa kiota cha ndege. Mashine zetu zikilinganishwa na zile za aina ya zamani, zinatumia mali-ghafi kidogo na kila mashine inaweza kuokoa umeme kilowati 10,000/saa kwa mwaka."

Vyombo vya kupimia na frequency transformer zinazozalishwa na kampuni ya Shidai zimetumika sana katika sekta za uyeyushaji wa chuma cha pua na utoaji wa mafuta ya ghafi ya petroli. Bidhaa zinazozalishwa na kampuni hiyo zinapendwa na wateja wengi, kutokana na bidhaa hizo kutumia raslimali na nishati kidogo.

Kupunguza matumizi ya rasilimali na nishati na kuimarisha hifadhi ya mazingira hivi sasa ni moja ya kazi muhimu ya serikali ya China. Naibu waziri mkuu wa China Bw. Zeng Peiyan kwenye mkutano uliofanyika hivi karibuni kuhusu kuendeleza matumizi ya nishati alisema kupunguza matumizi ya nishati na kuhifadhi mazingira kumekuwa sera za kimsingi za China.

"Ili kukabiliana na hali hiyo mpya, tumetoa wazo la kuweka maendeleo ya uchumi kwenye njia ya maendeleo endelevu na yenye uwiano, kuharakisha mabadiliko ya mtindo wa ongezeko la uchumi, kuchukulia kutokomeza ubadhirifu wa raslimali kuwa sera za kimsingi za taifa, kuendeleza uchumi wa mzunguko, kuhimiza usalama katika uzalishaji mali, kuongeza ufanisi wa raslimali na kuokoa nishati kwa kiasi cha 20% kuliko mwaka 2005 katika sekta ya uzalishaji mali."

Mwaka 2004 matumizi ya mafuta ya petroli ya asili ya China yalichukua 8% ya matumizi ya mafuta ya asili duniani; Matumizi ya umeme yalichukua 10% ya duniani; Matumizi ya chuma cha pua na makaa ya mawe yote yalikuwa kiasi cha 20% ya duniani. Lakini pato la China lilikuwa 4% tu ya lile la dunia nzima, na ufanisi wa matumizi ya raslimali na nishati ulikuwa chini ya wastani wa kiwango cha duniani. Aidha, mazingira ya asili ya China yameharibiwa vibaya katika maendeleo ya uchumi.

Hivi sasa serikali ya China imeimarisha udhibiti wa ubadhirifu wa raslimali na kuunganisha ipasavyo kuinua ufanisi wa raslimali na hifadhi ya mazingira.

Tibet iko kwenye uwanda wa juu wa Qinghai na Tibet, sehemu ya kusini magharibi ya China, huko ni mahali penye mwinuko mkubwa zaidi duniani ambapo kuna mwangaza mwingi wa jua. Hivi sasa kila mahali huko kuna zana za kutumia nishati ya mwangaza wa jua. Tarafa ya Duina ni kijiji chenye shughuli za kilimo na ufugaji kwa pamoja ambayo iko kwenye mwinuko wa mita zaidi ya 4,500 kutoka kwenye usawa wa bahari. Serikali ya huko ilijenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia mwangaza wa jua miaka 3 iliyopita, wakulima na wafugaji wa huko wamenufaika kutokana na matumizi ya umeme.

Mwanakijiji wa Duina Bw. Basangciren alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alisema, "Hivi sasa tunaweza kuangalia televisheni na kutumia VCD, pia wakati tunapotengeneza samli tunatumia mashine."

Huko Tibet, si kama nishati inatumika katika uzalishaji wa umeme na kuleta mwangaza wakati wa usiku tu, bali pia inatumika katika kuleta joto, kupika na kuchemsha maji ya kuoga. Matumizi ya nishati ya mwangaza wa jua yameboresha maisha ya wakulima na wafugaji wa Tibet, na pia yamehifadhi mazingira ya asili ya Tibet.

Hivi sasa katika mikoa ya Xinjiang na Mongolia ya ndani ya China nishati ya mwangaza wa jua na upepo inatumika sana. Katika sehemu zenye milima za pembezoni vimejengwa viwanda vya uzalishaji umeme kwa kutumia nguvu ya maji. Habari zinasema kuwa katika siku za baadaye China itaimarisha matumizi ya nishati zinazoweza kutumika tena na kuyaongeza hadi kufikia 15% kutoka 7% ya hivi sasa.

Ili kubadilisha mtindo wa ongezeko la uchumi, katika baadhi ya sehemu China imeanzisha maeneo ya majaribio yenye sekta za uzalishaji mali zinazofuata mtindo wa uchumi wa mzunguko zikiwa ni pamoja na uyeyushaji madini, kemikali na vifaa vya ujenzi. Lengo la majaribio hayo ni kufanya utafiti kuhusu mtindo wa uchumi wa mzunguko, teknolojia muhimu na maeneo ya uwekezaji vitega uchumi ili kuhimiza maendeleo endelevu ya uchumi wa taifa na kupata uzoefu.

Hivi sasa wataalamu wengi wa uchumi nchini China wanafuatilia masuala ya kubana matumizi ya nishati na hifadhi ya mazingira katika kuendeleza uchumi.

Idhaa ya kiswahili 05-12-13