Tokea China ilipoanza kutengeneza filamu mwaka 1905 hadi sasa imetimia miaka mia moja. Katika muda huo wa miaka mia moja?filamu zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu wa China, mabadiliko ya jamii na hisia za huzuni na furaha za watu wa China pia zimerekodiwa katika filamu. Lakini maendeleo ya filamu nchini China hayakuwa shwari kama taifa la China lilivyokuwa katika historia yake.
Filamu ya kwanza kabisa nchini China ilikuwa ni opera ya Beijing iliyopigwa mwaka 1905, muda wa filamu hiyo ni dakika kumi tu na ilipigwa katika studio ya picha ya Feng Tai mjini Beijing. Baadaye studio hiyo iliwahi kupiga filamu saba ambazo zote zilikuwa ni za opera ya Beijing. Jambo la kusikitisha ni kuwa studio hiyo ilipata ajali ya moto, filamu zilizopigwa karibu zote ziliungua.
Katika miaka ya 20 ya karne iliyopita, sanaa ya filamu nchini China ilianza kustawi na zilitokea filamu nzuri kadhaa za hadithi. Mtaalamu wa historia ya filamu wa China Bw. Li Suyuan alieleza, "Katika miaka hiyo, sanaa ya filamu nchini China bado ilikuwa haina mwelekeo mzuri, ilikuwa ni mwanzo tu wa ustawi wa filamu. Filamu katika miaka hiyo zilikuwa zinatengenezwa ili kukidhi mahitaji ya watu, aina za filamu hizo ni za kueleza maadili ya jamii, mapenzi, historia, upelelezi wa kesi na filamu za gong fu."
Mwaka 1923, filamu ya kwanza ilikuwa ni ya hadithi "Mtoto Yatima Amwokoa Babu Yake". Hii ni filamu iliyofanikiwa sana katika biashara na sanaa, ikieleza kuwa mke aliyefiwa na mumewe alifukuzwa na wakwe. Mjane huyo alimlea mtoto wake katika hali ya shida na kudharauliwa hadi mtoto wake alipokuwa mtu wa maana, baadaye mtoto huyo alimwokoa babu yake, na mjane huyo pia alijiunga na wakwe wake. Mhariri wa filamu hiyo ni mmoja wa watu wa mwanzo kwenye maendeleo ya filamu nchini China. Anaona kuwa filamu lazima ioneshe maisha halisi, na iwe na jukumu la kuwaelimisha umma na kuigeuza hali mbaya ya jamii, hii vile vile ni mila ya filamu za China hadi leo. Filamu hiyo ilioneshwa kwa miezi saba mfululizo katika miji mikubwa ya Beijing, Nanjing na Tianjin, na kuleta mapato makubwa. Tokea hapo fani ya filamu ilistawi haraka. Tokea mwaka 1922 hadi 1926 kampuni za filamu zilifikia 175, mjini Shanghai tu kulikuwa na kampuni 145.
Katika miaka ya 30 ya karne iliyopita, Japan ilianzisha vita vya kuivamia China, taifa la China lilikuwa hatarini na maisha ya Wachina yalikuwa mabaya. Katika miaka hiyo zilitokea filamu zilizoonesha maisha halisi. Bw. Li Suyuan alisema, "Filamu katika kipindi hiki zilikuwa zinaonesha maisha ya wananchi, na hasa maisha ya makabwera, na sanaa ya filamu ilikuwa ya hali ya juu zaidi, hadi sasa watu wanapenda kuangalia filamu za miaka hiyo."
"Wimbo wa Wavuvi" ni filamu iliyopigwa katika mwaka 1934, inaeleza hadithi ya familia moja ya wavuvi iliyohuzunisha, na wimbo huo ulikuwa ukiimbwa sana na Wachina. Filamu hiyo iliwahi kuoneshwa kwa siku 84 mfululizo katika jumba moja la filamu. Mwaka 1935 filamu hiyo ilipata tuzo katika tamasha la kimataifa la filamu lililofanyika Moscow, na tuzo hiyo ilikuwa ya kwanza kabisa kutolewa kwa filamu ya China.
Katika miaka ya 30 na 40, sambamba na maendeleo ya filamu, waliibuka waigiza filamu wengi nyota.
Wimbo unaoitwa "Mwimbaji wa Kike Asiye na Makazi" uliopo katika filamu ya "Malaika Barabarani" ulioimbwa na mwigizaji wa kike wa filamu Zhou Xuan unajulikana kwa Wachina wote. Filamu hiyo ilipigwa mwaka 1934, wimbo huo ulimfanya mwigizaji Zhou Xuan awe maarufu. Zhou Xuan aliigiza kwenye filamu zaidi ya 40 na kuimba nyimbo zaidi ya 100 za filamu. Kutokana na sura yake nzuri na sauti yake tamu alipendwa sana na watazamaji na kusifiwa kuwa na "sauti ya dhahabu".
Mwishoni mwa miaka ya 40 ya karne iliyopita, wasanii wa China waliopita miaka ya vita walitunga hadithi nyingi za filamu zilizoonesha maisha yalivyokuwa wakati wa miaka ya vita, hasa filamu ya "Maji ya Mto Yaelekea Mashariki". Kwa kupitia hadithi ya mume na mke waliopoteana wakati wa vita na baadaye mume aligeuza mapenzi, filamu hiyo inaeleza msiba wa Wachina.
Filamu zilizotengenezwa katika kipindi tokea mwaka 1905 hadi 1949 zinachukua nafasi muhimu katika historia ya filamu za China, na zina athari kubwa kwenye nchi za nje. Profesa aliyefanya utafiti wa historia ya filamu za China kwa miaka zaidi ya 40 Bw. Cheng Jihua alisema, "Mwaka 1983, 1986 na 1989 nilikwenda mara tatu kufundisha katika Chuo Kikuu cha Los Angeles nchini Marekani. Wanafunzi waliotoka Marekani, Uingereza, India, Japan na Malaysia waliangalia filamu za China darasani, walisema filamu za China katika kipindi cha mwanzo hazikuwa nyuma zikilinganishwa na filamu za nchi nyingine duniani."
Idhaa ya kiswahili 2005-12-19
|