Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-27 16:03:47    
Barua 1225

cri

       Mwaka mpya 2006 unakaribia kuwadia, pia tunapenda kuwatakia furaha na kila la heri katika mwaka mpya wa 2006.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu kwa juhudi zenu kwa mwaka huu unaokwisha za kusikiliza matangazo yetu na kuendelea kuwasiliana nasi, pamoja na kutoa maoni na mapendekezo yenu mbalimbali kuunga mkono matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Mwaka huu 2005 Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa imefanya juhudi kubwa katika kuendelea kuchapa kazi kwa ajili ya kuboresha vipindi, kuchapisha jarida dogo la Daraja la Urafiki, kwenda nchi za Kenya na Tanzania kutafuta ushirikiano wa kuboresha usikivu wa matangazo yetu na kadhalika. Mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2006, kituo cha FM kinachojengwa huko Nairobi, Kenya kitazinduliwa rasmi, ambapo matangazo ya idhaa ya Kiswahili yataongezwa muda tena.

Vilevile hivi sasa tunafanya maandalizi ya kuyawezesha matangazo yetu yarushwe hewani kupitia mawimbi ya FM ya Radio Tanzania Dar es Salaam na Sauti ya Tanzania Zanzibar mwanzoni mwa mwaka 2006.Yote hayo yanaonesha kuwa kazi zetu zinastawi na kupata maendeleo. Ingawa hivi sasa nguvu na uwezo wa idhaa yetu bado si mkubwa, lakini polepole matangazo yetu yatabadilika na kuwa na sura mpya.

Msikilizaji wetu Erickson Steven Rumbagi wa Bupandagila High School sanduku la posta 125 Bariadi Shinyanga Tanzania, ametuletea barua akisema anaendelea na masomo yake kama kawaida, hata tunaweza kushangaa kuona barua kama hii kwani anahitaji kutueleza kuwa yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule ya sekondari Bupandagila.

Anasema dhamira halisi ya barua hii ni kutushukuru sana kwa kumwezesha Willson Sambu Kamba rafiki yetu wa barua kwa kumtumia barua ambayo ilikuwa na bahasha hii na nyingine ya maswali ambayo bahasha hii alimwomba ampe ili aweze kujiingiza katika safu hii ya kupata rafiki.

Anasema yeye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu ambapo mwaka 2006 anategemea kumaliza masomo yake. Kwa ufupi yeye anapenda kuwa rafiki wa Radio China kimataifa iliyoko Beijing, China. Kwani muda mrefu amekuwa akitafuta rafiki wa kalamu na hatimaye amepata anasema asante. Wakati anaandika barua hii ulikuwa umebaki muda mfupi kabla ya kufika mwezi wa 12 ili waweze kumaliza mwaka, barua yetu tutakayomjibu alikuwa hadhani kama itamfikia kwa wakati hivyo basi anatutakia heri na baraka tele katika utangazaji wetu, ili tuweze kufanikiwa katika mipango yetu.

Tunamshukuru sana Bwana Erickson Steven Rumbagi kwa barua yake ya kutusalimia, na tunamkaribisha kwa furaha kubwa awe msikilizaji wa matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kutoa maoni na mapendekezo siku zijazo.

Msikilizaji wetu Happynus Pilula ambaye barua zake huhifadhiwa na Athumani Yakusola wa sanduku la posta 772, Sumbawanga Tanzania anasema katika barua yake kuwa, dhumuni la barua yake hii limegawanyika katika sehemu mbili, ya kwanza ni shukrani na pongezi kutokana na matangazo yetu ya kila siku, na ya pili ni maoni yake binafsi.

Anapenda kuipongeza idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwa kuongeza muda wa matangazo ya kila siku jioni, anasema huu ni mwanzo wa hatua za maendeleo, anatumai kuwa mengi zaidi ya hilo yatafanyika. Pia asingependa kuwahasahau ndugu wote waliofanya vizuri kwenye chemsha bongo ya ujuzi wa miaka 55 ya China, anawapa pongezi sana, kwani safari hii walijitahidi vilivyo kuonesha ushindani zaidi kwani awamu iliyopita inaonekana kama upinzani haukuwa wa kutosha.

Na maoni yake ni kuwa mabadiliko kutokana na maoni yao yameonekana kwa kuongeza muda wa vipindi ,lakini kwa hao wasikilizaji wa Tanzania usikivu bado ni duni sana, hivyo ombi lake ni kuwa kama tulivyoahidi tuweze kulifanyia kazi mapema, kwani kutembelea tovuti mara kwa mara ni gharama sana.

Aidha kutokana na mabadiliko ya muda wa vipindi ni matumaini yake kuwa hata ratiba ya vipindi itabadilika hivyo angeomba tuweze kuwatumia kadi za ratiba ya vipindi. Siku zilizopita aliwahi kuomba kutumiwa kitabu cha kujifunza kichina, lakini mpaka sasa hajapata, kama hakijachapishwa, angependa kama wakati wa uchapishaji kurasa za kwanza kuwa na utangulizi utakaomwezesha msikilizaji kujua kuandika silabi pamoja na namba mbalimbali.

Na mwisho ni wasikilizaji wenzake, anawashauri wanapokuwa wengi katika eneo moja ni vizuri wakiungana na kuunda klabu, hii inakuwa na nguvu katika kueneza jina na sifa za idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana Bwana Happynus Pilula kwa barua yake, na kwa pongezi zake kwa mabadiliko ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa inatutia moyo, lakini pia tuna wasiwasi kwamba usikivu wa sehemu fulanifulani nchini Tanzania bado si mzuri. Kama tulivyosema, tunafanya maandalizi ya kuyawezesha matangazo yetu yarushwe hewani kupitia mawimbi ya FM ya Radio Tanzania Dar es Salaam na Sauti ya Tanzania Zanzibar mwanzoni mwa mwaka 2006, kwani Radio China kimataifa na Radio Tanzania Dar es Salaam na Sauti ya Zanzibar zimefikia makubaliano ya hatua ya mwanzo, lakini kutokana na utaratibu unaohusika, bado hatujaingia kwenye maandalizi rasmi, sasa idara husika imeshawasilisha ombi la kupata zana na vifaa hata fedha kwa idara husika ya ngazi ya juu, halafu tutakuwa na pilikapilika nyingine tena za maandalizi. Tunatarajia kutimiza lengo hili mapema iwezekanavyo.

Kuhusu kitabu cha kujifunza kichina, vipindi vya kujifunza kichina viliandaliwa na mfanyakazi aliyestaafu wa idhaa yetu, alipokuwa akiaandaa hakuandika kwa makini, na yeye amestaafu na kuondoka, vilivyotangazwa zamani hatuwezi kuvipata tena. Tumekuwa na mpango wa kuandaa vipindi vipya vya kujifunza kichina chini ya msaada wa idara husika, lengo likitimizwa, tutakuwa na kitabu rasmi, ambacho kitaweza kuchapishwa na kuwatumia wasikilizaji wetu.'

Lakini tunaona pendekezo lake kuhusu kuweka kama wakati wa uchapishaji wa kurasa za kwanza kuwa na utangulizi utakaomwezesha msikilizaji kujua kuandika silabi pamoja na namba mbalimbali, sisi tutajitahidi kuifanya ama kila tukichapisha jarida letu la Daraja la urafiki, tunaweza kuweka silabi moja moja au namba mbalimbali za kichina, ili wasikilizaji wetu wenye hamu waweze kujifunza.

Idhaa ya kiswahili 2005-12-27