Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2005-12-28 20:11:07    
Matibabu ya jadi na dawa za mitishamba za kichina zafanya kazi muhimu kwenye sehemu za vijijini nchini China

cri

matibabu ya jadi na dawa za mitishamba za kichina zenye historia ya zaidi ya miaka 5000, ni sehemu muhimu ya utamaduni wa jadi wa China na zinapendwa na kuaminiwa na wachina. Ingawa hivi sasa matibabu ya kisasa yamekuwa mkondo mkuu katika sekta ya matibabu, lakini kutokana na matibabu ya jadi ya kichina kuwa na mbinu nyingi, ufanisi mkubwa na bei nafuu, bado ni sehemu muhimu ya matibabu nchini China. Katika kipindi cha leo, tutawaelezea kuhusu hali ya matibabu ya jadi na matumizi ya dawa za mitishamba za kichina kwenye sehemu za vijijini mkoani Sichuan,China.

Bi. Yu Mingying ni mkulima wa kijiji cha Yongsheng kilichoko kwenye mji wa Dujiangyan mkoani Sichuan. Katika miaka mitano iliyopita, alipatwa na ugonjwa sugu wa nyongo. Katika miaka ya hivi karibuni, ameendelea kutumia dawa za mitishamba, na gharama ya dawa hizo ni yuan mia moja tu kwa mwaka, lakini ufanisi wa matibabu hayo umekuwa mzuri sana. Alisema:

"siku kadhaa zilizopita, nilikuwa na mafua na ugonjwa wa nyongo ukarudi. Na nilitumia dawa za mitishamba mara moja, mwili ulipoanza kuwa na maumivu, na nimeanza kupona tena. Nikipatwa na ugonjwa, kwa kawaida nitatumia dawa za mitishamba."

Katika zahanati ya kijiji cha Yutang kilicho karibu na kijiji cha Yongsheng, mwandishi wetu wa habari aligundua kuwa wagonjwa wengi wanaokwenda kwenye zahanati hiyo wanachagua madaktari wa matibabu ya jadi. Mwenyeji wa kijiji hicho Bi. Luo Bing alisema:

"dawa za mitishamba zina ufanisi mkubwa, madhara madogo na bei yake ni nafuu. Hivyo sisi sote tunapenda kutumia dawa hizo."

Uchunguzi uliofanyika unaonesha kuwa, kwenye sehemu za vijijini, wastani wa gharama za matibabu ya kichina kwa kila mtu ni yuan za Renminbi 6 hadi 8, ikiwa ni chini kwa asilimia 20 hadi 30 kuliko gharama za matibabu ya kisasa. Hivi sasa vituo vya huduma za afya vya vijiji zaidi ya 140 katika mji wa Dujiangyan vimeweka idara za matibabu ya jadi. Kuenea kwa huduma za matibabu ya jadi kunafanya wastani wa gharama za matibabu kwa kila mtu mjini humo zipungue mwaka baada ya mwaka, hali hiyo inapunguza mzigo wa kiuchumi kwa wagonjwa, hasa wagonjwa wa vijijini.

Bw. Yang Yong ni mmoja wa madaktari wa vijijini wa mji huo, zahanati yake yenye wafanyakazi watatu inawajibika kutoa huduma za matibabu ya kimsingi kwa vijiji vitatu vilivyoko karibu. Alisema:

"hapa kuna vijiji vitatu na wakazi zaidi ya 5500. tunapendelea dawa za mitishamba ya kichina. Na kwa wastani, matibabu ya jadi na dawa za mitishamba ya kichina yanachukua asilimia 40 katika huduma zote."

Kutokana na matibabu ya jadi na dawa za mitishamba ya kichina kupendwa na wakulima, katika miaka ya karibuni, mkoa wa Sichuan umeweka mkazo katika kujenga mfumo wa huduma za matibabu ya mitishamba wenye ngazi tatu za vijiji, tarafa na wilaya. Asilimia 80 ya wilaya za mkoa huo zimekuwa na hospitali za matibabu ya jadi, asilimia 90 ya vituo vya huduma za afya vya vijiji vina idara za matibabu ya jadi, sehemu za kuchukua dawa za mitishamba ya kichina na vyumba vya matibabu ya akyupancha. Hivi sasa huduma za matibabu ya jadi zinachukua zaidi ya asilimia 30 ya jumla ya huduma za matibabu kwenye sehemu za vijijini mkoani Sichuan.

Mkoa wa Sichuan pia unaweka mkazo katika kuandaa wataalamu wa matibabu ya kichina. Kuanzia mwaka 1998, mkoa huo umeandaa wataalamu zaidi ya 1200 wa matibabu ya kichina na kutoa mafunzo kwa madaktari wa vijijini, mpaka sasa madaktari zaidi ya elfu 10 wamepata shahada za sekondari ya juu ya matibabu ya kichina. Aidha, mkoa huo pia unaeneza ufundi wa matibabu ya kichina kama akyupancha na kusinga kwa ajili ya kuzuia na kutibu kwa gharama ndogo magonjwa ya kawaida yanayotokea mara kwa mara vijijini, hatua hiyo imkuwa na mafanikio.

Mkurugenzi wa idara ya usimamizi wa matibabu ya kichina na dawa za mitishamba ya kichina ya mkoa wa Sichuan Bw. Yang Dianying alisema, mkoa wa Sichuan umetatua kwa kiasi fulani suala kuhusu wakulima ambao hawawezi kumudu gharama kubwa za matibabu na kuhakikisha afya za wakulima kwa njia ya kuimarisha huduma za matibabu ya kichina kwenye sehemu za vijijini mkoani humo. Alisema:

"kueneza matibabu ya kichina na dawa za mitishamba ya China kwenye sehemu za vijijini kunapunguza mzigo kwa wakulima. Tunaona kama tukiweza kutibiwa magonjwa ya kawaida papo hapo kijijini, basi hatutasubiri kupata matibabu mpaka magonjwa madogo yaendelee kuwa magonjwa makubwa. Kama ikiwa hivyo, lazima tulipe gharama kubwa za matibabu."

Hali ya mkoa wa Sichuan ni ya kawaida. Katika mikoa mingi nchini China, hasa katika mikoa ya magharibi ya kati yenye idadi kubwa ya wakazi wa sehemu za vijijini, matibabu ya kichina na dawa za mitishamba ya China yanaendelea kufanya kazi kubwa zaidi. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2004, kuna hospitali 1500 za matibabu ya kichina za wilaya kote nchini China. Hospitali hizo zinaendelea kupanua huduma zake na baadhi ya idara maalum za matibabu ya kichina zimekuwa chaguo la kwanza kwa wakulima wa huko. Asilimia 75 ya vituo vya afya vya vijiji na tarafa nchini China vimeweka idara za matibabu ya kichina, na idara nyingi kati ya hizo zinapokea asilimia 30 ya wagonjwa wote wanaokwenda kwenye vituo hivyo. Aidha, mikoa ya Zhejiang, Henan, Sichuan na Gansu pia imeweka vigezo vya ujenzi wa idara ya matibabu ya kichina kwenye vituo vya afya vya vijiji na tarafa.

Ili kuhimiza zaidi maendeleo ya shughuli za matibabu ya kichina na dawa za mitishamba ya China kwenye sehemu za vijijini, serikali kuu ya China imetenga yuan za Renminbi milioni 100 kurekebisha miundombinu ya hospitali za matibabu ya kichina za wilaya maskini, wilaya zinazojiendesha za makabila madogomadogo, na wilaya za mipakani kwenye mikoa 7 ya magharibi ya kati. Katika miaka mitatu hadi mitano ijayo, serikali kuu itaendelea kuongeza fedha kuboresha miundombinu na vifaa vya hospitali za matibabu ya kichina kwenye sehemu hizo.