China ni nchi yenye aina nyingi za vyakula, na vyakula vinavyotokana na unga wa ngano kama vile mikate na tambi ni vyakula muhimu kwa wakazi wa mkoani Henan, katikati ya China.
Bwana Liu Shengli na familia yake kila wiki wanakula mara kadhaa tambi inayochanganywa pamoja na nyama na mboga. Akisema:
"Japokuwa hivi sasa kiwango chetu cha maisha kimeinuka, lakini tumezoea kula tambi, tunaona tambi ni chakula kitamu sana. Hata kama hatuna wakati wa kupika tambi nyumbani, wakati wa wikiendi au wakati wa sikukuu tunakula tambi kwenye mikahawa."
Wanafamilia wa Bw. Liu wanapenda kula tambi zilizopikwa pamoja na supu ya nyama ya mbuzi, chili na visibiti, Doufu, uyoga mweusi, mwani na kadhalika. Tambi hizo si kama tu zina ladha nzuri, bali pia zina lishe bora.
Karibu wakazi wote wa Henan wanapenda kula tambi zilizochanganywa na mboga na nyama. Wageni kutoka sehemu nyingine wakienda mkoani Henan hawakosi kuonja tambi hizo. Mikahawa ya tambi mkoani Henan imetapakaa kila mahali.
Zhengzhou, mji mkuu wa mkoa wa Henan unajulikana sana kwa tambi, karibu kila mtaa una mikahawa kadhaa ya tambi, hivyo ni rahisi sana kwa watu wa huko na wageni kutoka nje kula tambi za aina mbalimbali. Mkahawa wa tambi wa Xiaoji ulioko kwenye sehemu ya katikati ya mji wa Zhengzhou kila siku unajaa na wateja. Mwandishi wetu wa habari alipoingia tu mkahawani alisikia harufu nzuri ya supu ya nyama ya mbuzi. Bwana Liu Wen kutoka mkoa wa Hebei alisema:
"Tambi za hapa ni tamu sana. Nilifika hapa jana, niliambiwa na rafiki yangu kuwa tambi ya Zhengzhou ni nzuri sana, hivyo tumekuja hapa kuonja tambi hizo. "
Mpishi mkuu wa mkahawa huo Bwana Dong Zhishan alimwambia mwandishi wetu wa habari kuhusu siri ya mkahawa huo kuwavutia wateja wengi. Akisema:
"Kwenye mkahawa wetu kuna aina tatu za supu, yaani supu ya mifupa, supu ya nyama ya mbuzi, na supu ya kuku. Umaalum wa tambi zinazopikwa kwenye mkahawa huo ni, ladha nzuri ya supu, tambi zinazopikwa kama za kutafunwa, na nyama zinazoiva kabisa."
Mkazi mmoja wa Zhengzhou alisema, kula tambi si kama tu kunategemea ladha ya tambi zenyewe, bali pia kunahitaji hali yenye uchangamfu mkahawani.
Licha ya tambi hizo zinazopikwa kwa kuchanganywa na mboga na nyama, wakazi wa Henan wanaweza kupika aina nyingine nyingi za tambi kwa maumbo tofauti, kuna tambi pana, tambi nyembamba, na tambi zenye umbo la majani, ambazo zinaweza kupikwa kwa ladha yenye chumvi kidogo, chumvi nyingi, na yenye pilipili au siki.
Tambi zinazonyooshwa kwa mikono pia zinajulikana sana mkoani Henan. Mkahawa wa Yangji ni maarufu sana wa tambi zinazonyooshwa kwa mkono, tambi zinazopikwa kwenye mkahawa huo si kama tu ni laini, bali pia zinapikwa kama za kutafunwa. Jikoni mpishi anashika kinyunya, na kusukuma kwa nguvu unga uliokandwa kwenye ubao, halafu ananyoosha kwa mikono miwili unga uliokandwa, anakunja na kunyoosha tena. Akirudia vitendo hivyo kwa mara kadhaa, tambi anazotengeneza zinakuwa kama nyuzi. Mteja Bi. Zhang Li alisema:
"Mimi huwa nakuja hapa kula tambi pamoja na marafiki au jamaa zangu. Kwa kweli naishi mbali kidogo na hapa, lakini tunapenda sana tambi za hapa."
Wakazi wa Henan wanakula tambi kutokana na mabadiliko ya majira. Katika majira ya baridi wanakula tambi zinazopikwa kwa kuchanganywa na mboga na nyama au tambi zinazonyooshwa. Wakati wa joto wanapendelea zaidi tambi zilizotiwa ndani ya maji baridi baada ya kuiva, halafu zinachanganywa na viungo, vitunguu na mboga mbichi.
Kupenda kula tambi kwa wakazi wa Henan kunatokana na mkoa huo kuwa na mavuno makubwa ya ngano. Mkoa wa Henan uko katika tambarare ya katikati ya China, na ukanda wenye halijoto ya fufutende, ni mkoa unaozalisha nafaka kwa wingi, hasa ngano hivyo tambi ni chakula cha kwanza kwa wakazi wa mkoa huo, kila siku wanakula tambi mara moja, na wakazi wa huko wamevumbua upishi wa aina mbalimbali wa vyakula vinavyotokana na ngano.
Idhaa ya kiswahili 2005-12-29
|