Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-06 16:04:38    
Nchi za Afrika zatumia dawa ya kichina Artemisinin kutibu Malaria

cri

Hivi sasa dawa ya kichina aina ya Artemisinin imekuwa silaha yenye nguvu kwa waafrika kujikinga dhidi malaria. Gazeti la Times la Uingereza lilitoa makala likisema kuwa, dawa hiyo inayotengenezwa kwa mitishamba ya kichina imeokoa maisha ya mamilioni ya watu. Gazeti hilo limesema kuwa, dawa inayotengenezwa kwa Artemisinin imekuwa dawa ya kutibu malaria badala ya dawa ya jadi Quinine.

Mmea wenye dawa inayotibu malaria unaojulikana kama Sweet Wormwood au Artemisia Annua unalimwa katika mikoa ya Guangxi, Yunnan na Sichuan nchini China. Zaidi ya asilimia 80 ya Artemisinin zinazotengeneza dawa za kutibu Malaria zinatoka mji wa Chongqing, China, kiasi cha mimea ya Sweet Wormwood cha huko kimefikia tani elfu kadhaa, na sifa yake inachukua nafasi ya kwanza duniani.

Katika miaka zaidi ya 1600 iliyopita, kitabu cha tiba cha kale cha China kimeeleza njia ya kutibu malaria kwa kutumia Artemisinin. China ilianza kutumia Artemisinin katika matibabu kuanzia miaka ya 80 ya karne ya 20. Lakini kutokana na kutokuwa na wagonjwa wengi wa Malaria nchini China, Artemisinin haikutumika kwa kiasi kikubwa. Hadi kufikia mwanzoni mwa karne ya 21, Shirika la Afya Duniani WHO lilirekebisha mkakati wa kinga na tiba ya Malaria, na uwezo wa Artemisinin katika kutibu ugonjwa huo ulianza kuzingatiwa.

Harakati ya kinga na tiba ya Malaria ilianzishwa miaka ya 50 ya karne iliyopita, wakati huo DDT ilikuwa dawa muhimu ya kuua mbu. Ingawa dawa hiyo ilifanya kazi kubwa katika kuua mbu, lakini wakati huo huo ilileta uchafuzi kwa mazingira, na kuweza kusababisha maradhi mapya.

Hadi kufikia miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na matumizi ya kupita kiasi ya dawa za jadi zinazokinga Malaria, mwili wa binadamu ulianza kuzoea dawa hizo, na uwezo wa dawa hizo ulikuwa umepungua, na Malaria yaliibuka tena barani Afrika na Asia, na kuwa mwuaji mkubwa wa pili kwa binadamu baada ya Ukimwi, na kutishia maisha ya watu milioni 300. Idadi ya watu wanaokufa kwa malaria duniani ni zaidi ya milioni 3 kwa mwaka, na wengi kati ya wagonjwa hao ni watoto wenye umri chini ya miaka 5.

Hali hiyo iliwafanya wataalamu watambue umuhimu wa tiba ya malaria. Wataalamu walipendekeza kuwa, Shirika la Afya Duniani WHO linapaswa kubadilisha mikakati ya kuua mbu, na kuzuia kuenea kwa malaria kwa njia ya tiba kutokana na hali tofauti za sehemu mbalimbali. WHO ilipokea mapendekezo hayo, na wataalamu walianza kuweka mkazo wa matumizi ya Artemisinin.

Mwanzoni, wataalamu hawakupenda kutumia mitishamba kama Sweet Wormwood wakiwa na wasiwasi kwamba ni vigumu kudhibiti matumizi ya mitishamba. Lakini walibadilisha maoni yao baada ya kugundua uwezo wa Artemisinin. Mwaka 2001, sehemu ya Kwazulu nchini Afrika ilikuwa sehemu ya kwanza iliyotumia mitishamba iliyotengenezwa na Artemisinin kutibu Malaria, na kupata matokeo mazuri, na wagonjwa wengi walipona baada ya kutumia dawa hiyo kwa siku tatu mfululizo, na idadi ya watu waliokufa kutokana na ugonjwa huo ilipungua kwa asilimia 87, na kiasi kikubwa cha dawa hizo kinatoka China.

Kampuni ya dawa ya Hua Li Ke Tai ya Beijing ni kampuni iliyouza dawa ya Artemisinin mapema zaidi barani Afrika. Asilimia 97 ya wagonjwa wa Malaria walipona baada ya kutumia dawa hiyo. Pia Artemisinin inauzwa kwa bei rahisi, na inafaa wagonjwa kwenye sehemu maskini. Kutokana na takwimu za WHO, mwaka 2004 watu zaidi ya milioni 30 walitumia Artemisinin, na kiasi hicho kilifikia milioni 132 mwaka 2005.

Hivi sasa mapato ya soko la dawa ya kutibu Malaria barani Afrika ni dola za kimarekani bilioni 20 kwa mwaka. Mwaka 2004, Shirika la afya duniani WHO lilinunua tani 30 za dawa za Artemisinin kutoka Chongqing, China. Kutokana na takwimu hizo, dawa hizo bado haziwezi kutosheleza mahitaji ya soko la kimataifa. Takwimu kutoka Kampuni ya dawa ya Hua Li Ke Tai zinaonesha kuwa, mwaka 2003, nchi 10 zilitumia dawa ya Artemisinin kutibu Malaria, na kiasi hicho kiliongezeka hadi 31 mwaka 2004. Gazeti la the Economist liliripoti kuwa, hivi sasa suala linaloikabili kazi ya tiba ya Malaria ni ukosefu wa mimea ya Sweet Wormwood, na hivi sasa kiasi cha Artemisinin kinaweza kutosheleza thuluthi tu ya mahitaji yote. Katika miaka 5 hadi 10 ijayo, mapato ya biashara ya Artemisinin yatazidi dola za kimarekani bilioni 1.5 katika soko la kimataifa, lakini China ikiwa nchi inayozalisha Artemisinin kwa wingi, hivi sasa mapato yake yanayotokana na mauzo ya Artemisinin ni dola za kimarekani milioni 7 tu, kiasi ambacho ni chini ya asilimia 1 ya mapato ya jumla.

Kutokana na uwezo wa matibabu na thamani ya kibiashara ya Artemisinin, nchi mbalimbali za Ulaya na Marekani zimeanza kuharakisha hatua ya utafiti na uendelezaji wa Artemisinin. Wataalamu wa Marekani wanajaribu kutumia Artemisinin kutibu saratani. Matokeo ya uchunguzi wa mwanzo yanaonesha kuwa, Artemisinin vilevile inafanya kazi katika kuzuia saratani.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-06