Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani, Shule ya Msingi ya Alaro, sanduku la posta 61 Ophoro, Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu na kututakia amani na mafanikio katika kazi yetu ya kuwapasha wasikilizaji wetu habari motomoto. Anasema yeye huko Kenya hajambo na mzima kabisa.
Anasema angependa kutoa shukurani zake kwetu kutokana na nyoyo zetu za kujali na kutilia maanani barua zote tunazozipokea. Kutokana na sababu hiyo tuliweza kumwandikia barua na kumtumia jarida lililojaa mengi ya kujifunza, huku likimpa fursa ya kuziona picha zetu pamoja na ile ya mkuu wa Radio China Kimataifa. Anashukuru na anaomba Mungu aikuze Radio China kimataifa ili ifikie upeo wa juu kabisa.
Anasema yeye ni mwalimu katika shule ya msingi, ambako anafundisha somo la kiswahili. Na hivyo basi anapenda sana idhaa nyingi za Kiswahili. Anasema siku moja katika hali ya kutafuta idhaa yoyote ya Kiswahili, mbali na KBC; aliweza kupata Radio China Kimataifa kwa mara ya kwanza. Alifurahi na kugundua kuwa alikuwa amekosa na kupitwa na mengi hasa kuhusu Elimu na Afya, Chemsha Bongo, ambayo imemwezesha kujua kuwa kisiwa cha Taiwan ni "kisiwa cha hazina cha China", Daraja la Urafiki, kipindi ambacho ni kama daraja kwake, kwani ameweza kujua au kusikia mengi kuhusu China.
Anamaliza barua yake kwa kusema angependa kututaka tusilegeze uzi hata kidogo na tuendelee kuwavutia wasikilizaji wengi wapya kama yeye na wengineo kwa kuboresha vipindi vyetu vya kila siku na kutoa chemsha bongo ambayo kwao wasikilizaji watapata "viinua mgongo", kwani chanda chema huvikwa pete!
Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani kwa barua yake ya kwanza ya kututia moyo, kwani tunaona matangazo yetu yanasikilizwa na kupendwa na wasikilizaji wetu wengi, yeye ni mwalimu wa kiswahili, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza kwa makini matangazo yetu ili kutoa maoni na mapendekezo yake kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.
Msikilizaji wetu Samuel Cosmas wa sanduku la posta 513 Tabora Tanzania ametuletea barua akisema kuwa yeye ni kijana wa Tanzania anayesoma katika shule ya sekondari. Anasema amebahatika kukutana na matangazo mengi kuhusu Radio China kimataifa, lakini hakuweza kujua undani sana wa radio hii, pia amejaribu kusikiliza matangazo yetu kwenye tovuti ya www.cri.cn, ambapo alitokea kuyapenda sana matangazo na utulivu wa radio kwa ujumla. Sasa anachoomba ni kujiunga kuwa mwanachama msikilizaji wa Radio China kimataifa na pia anachoomba ni kuendelea kumtumia barua na matangazo zaidi kuhusu radio yetu. Yeye ataendelea kusikiliza na kama atakuwa na maoni atatuandikia barua.
Tunamkaribisha kwa mikono miwili msikilizaji wetu huyo mpya Samuel Cosmas, tunamtaka aendelee kusikiliza vipindi vyetu na kutembelea kwenye tuvuti yetu ya mtandao wa internet ambayo anuani yake ni www.cri.cn, akiwa na maoni na mapendekezo asisite kutuandikia barua ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.
Msikilizaji wetu Mbarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai U.A.E anasema katiba barua yake kuwa, lilikuwa ni jambo la kufurahisha sana kuwaona mheshimiwa rais Hu Jintao wa Jamhuri ya watu wa China na makamu wake Bw. Zeng Qinghong walipokuwa wakitazama kwa furaha kubwa kurushwa kwa chombo cha pili cha China cha safari za anga ya juu kilichobeba wanaanga wawili Fei na Nie, chenye jina la Shenzhou No.6 asubuhi ya tarehe 12 Oktoba mwaka 2005 mjini Beijing katika kituo cha udhibiti wa satlaiti cha Beijing.
Miaka miwili tu tangu China ilipofanikiwa kurusha chombo chake cha kwanza cha safari ya anga ya juu kilichombeba mwananga shujaa Yang Liwei na kufanya safari ya kuizunguka dunia kwa saa 21, jambo ambalo lilifungua ukurasa mpya kwa China na kuandika historia iliyoiweka China kuwa ni taifa la tatu baada ya Marekani na Urusi ya zamani kufaulu katika sekta hiyo hapa duniani. Bila shaka yoyote kufaulu kwa wanaanga Fei na Nie katika safari ya anga ya juu ndani ya chombo cha Shenzhou No.6 kunadhihirisha wazi jinsi gani taifa la China lilivyopevuka na kukomaa katika elimu ya kisayansi na kiteknolojia hapa duniani, pamoja na umahiri wake wa kwenda sambamba kimaendeleo na mataifa mengine makubwa yaliyoendelea duniani.
Anasema yeye binafsi amevutiwa mno na mafanikio hayo ya China kurusha chombo cha pili cha safari za anga ya juu kilichobeba wanaanga wawili na kutua ardhini salama salimini baada ya kumaliza safari yao hiyo.
Anasema ni matumaini yake makubwa kuwa China haitasita kujiendeleza zaidi katika tenolojia hiyo siku za mbele na anatarajia kuwa huenda angalau siku moja itatokezea China itaweza kuzisaidia nchi nyingine zinazoendelea kama vile barani Afrika au Amerika ya kusini kufikia hatua kama hiyo.
Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mbarouk Msabah kwa barua yake ambayo hutuelezea maoni yake baada ya kusikiliza habari mbalimbali kutoka kwa Radio China kimataifa, kweli moyo wake wa kusikiliza kwa makini matangazo yetu, hutuhimiza kuandaa vizuri zaidi vipindi vyetu mbalimbali ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu na kuwawezesha wasikilizaji wetu wengi waweze kuijua zaidi China. Hapa tunamtakia kila la heri katika mwaka mpya 2006.
Msikilizaji wetu Ernest W. Mukimba wa sanduku la posta 2099 Bungoma Kenya anasema katika barua yake kuwa, anavipenda vipindi cha Radio China kimataifa, na anafurahi huku akitabasamu na kuwashukuru wote wanaohusika. Anasema matangazo ya Radio China kimataifa yanaelimisha mengi kote duniani, kwani yeye binafsi ameelimika kwa mengi kupitia radio China kimataifa. Pia anasema kupitia Radio China kimataifa watu mbalimbali wanaweza kujuliana hali, yaani kuwasiliana kwa kupitia salamu.
Anasema yeye matangazo ya Radio China kimataifa anayasikia kupitia idhaa ya kiswahili ya KBC. Pia amefahamishwa mengi kuhusu vipindi hivyo na Ayub Mutanda Shariff. Ila anawaomba wahusika wa Radio China kimataifa kama ikiwezekana wakati wa kuchapisha jarida la daraja la urafiki, ni vizuri likiwepo somo la kujifunza kichina ili wasomaji waweze kujua kuandika kichina.
Tunamshukuru msikilizaji wetu Ernest W.Mukimba kwa barua yake pamoja na maoni na mapendekezo yake, ikiwezekana tutafanya juhudi za kuwasadia wasikilizaji wetu kujifunza kichina na kuandika kichina, lakini kweli hii ni kazi ngumu.
Idhaa ya Kiswahili 2006-01-10
|