Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-17 20:17:58    
Barua 0115

cri

Kwanza tunapenda kuwaarifu wasikilizaji wetu kuwa, kituo cha FM cha Radio China kimataifa kinachojengwa huko Nairobi Kenya karibu kitazinduliwa rasmi mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2006. Baada ya kuzinduliwa kwa kituo hicho cha FM, matangazo ya Radio China kimataifa ya lugha ya kiingereza, lugha ya Kiswahili na lugha ya kichina yatasikika kwa saa 18 kwa siku nchini Kenya. Na matangazo yetu ya lugha ya Kiswahili yatakuwa saa tatu kwa siku kwenye wimbi la FM. Kutokana na hali ilivyo ya hivi sasa ya idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa, baada ya kuzinduliwa kwa kituo cha FM, mwanzoni, matangazo yetu hayataweza kuwa na mabadiliko makubwa, lakini katika matangazo yetu tutaongeza muda wa kipindi cha salamu zenu, burudani za muziki, waandishi wetu wa habari walioko Kenya watajitahidi kuwasiliana na wasikilizaji wetu, hata kituo cha waandishi wetu wa habari huko Nairobi kitaongezewa studio ya kazi, ambapo wasikilizaji wakipenda, wataweza kupata nafasi ya kutoa maoni na mapendekezo moja kwa moja kwenye studio yetu, baada ya kukamilisha mpango, tutaweza kuwaarifu wasikilizaji wetu, hivi karibuni tumekuwa na pilikapilika za maandalizi ya matangazo yetu, na hata tumechelewa kuchapisha jarida dogo la daraja la urafiki. Hapa tunaomba radhi kwa wasikilizaji wetu, tunaomba msiwe na malalamiko, tutafanya kila kitu hatua kwa hatua. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watatuletea barua kutoa maoni na mapendekezo kuhusu namna ya kufanya matangazo ya vipindi vyetu kwenye wimbi la FM yawe ya kuvutia.

Msikilizaji wetu Joel Ngoko wa sanduku la posta 1246 Kisii Kenya anasema katika barua yake kuwa, kwanza kabisa angependa kutupa salamu zake kutoka hapo Kisii Kenya. Pili anatoa pongezi nyingi kwa kuongeza muda wa matangazo yanayopitia shirika la utangazaji la Kenya KBC. Anasema hii ni mara yake ya kwanza ya kupata fursa ya kutuandikia barua kwa muda wa miaka miwili sasa, na katika muda huo hakuwahi kushiriki kwenye shindano lolote la Radio China kimataifa kwa sababu mara nyingi yeye huwa mbali na matangazo ya radio. Na hii inatokana na kazi yake ya usanii anayoifanya. Mara nyingi yeye huwa yuko nje msituni akikusanya picha za wanyama mbalimbali na kusoma tabia za wanyama hao. Lakini wakati huu alipata wakati mzuri kwa sababu ya muda ambao uliongezwa wa kutangaza wa Radio China kimataifa, na akashiriki kwenye shindano la chemsha bongo la mwaka 2005. Na ana matumaini makubwa ya kufaulu na kupata zawadi maalum ya kutembelea China. Anasema yeye ana kiu kubwa ya kuitembelea China. Anaipenda China sana kwa sababu ya uchumi wake mzuri ambao unasifika ulimwenguni kote pamoja na viwanda vyake ambavyo vimesifika duniani kote na umaridadi wa miji yake. Pia angependa kujionea hili taifa la China ambalo lina wanyama wa aina mbalimbali.

Anasema angependa pia kutualika kutembelea Kisii Kenya ili tupate tujionee utamaduni wao, na jinsi wanavyoishi kwenye wilaya yenye milima na mabonde, chakula wanachokula na jinsi walivyo wakarimu kama watu wa China. Pia anasema huko tutaweza kujionea mbuga za wanyama wa Kenya pamoja na milima mikubwa na mito, maziwa na mabonde mazuri sana ambayo yanasifika duniani. Na hatasahau kutaja ndege ambao hupatikana katika ziwa Nakuru mkoani Bonde la Ufa.

Anasema akifaulu kupata tuzo maalum la kuitembelea China atafurahi sana kwa sababu hii ni nchi anayoipenda sana kuishi na kusomea kwa sababu ya utamaduni wake wa hali ya juu kutokana na uchumi wake mzuri. Hata ingawa muda mwingi anakuwa nje, lakini siku hizi amekuwa hakosi kusikiliza matangazo yetu. Anashukuru kwa kuongeza muda wa matangazo. Kwani mambo ni polepole. Kwa sasa hajaona kasoro yoyote kwa kazi yetu. Anaomba Jarida la daraja la urafiki lisiachwe nyuma, liendelee sambamba na matangazo ya Radio.

Anatoa pongezi nyingi kwetu kwa hatua kubwa sana tuliyofikia, haya ni maendeleo makubwa sana ambayo asingesahau kuyaunga mkono. Sasa ni wajibu wake kama shabiki wa Radio China kimataifa kujivunia maendeleo hayo ya Radio China kimataifa. Anakamilisha barua yake kwa kusema angependa kutualika ndugu zake wa Radio China kimataifa tutembelee kwao kama majirani wema.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Joel Ngoko kwa barua yake ya kutufurahisha, tunashukuru kwa pongezi zake, tutaendelea na juhudi zetu katika kuandaa vipindi mbalimbali vya kufurahisha wasikilizaji wetu. Tena tunamshukuru kwa mwaliko wake wa kutembelea Kisii, maskani yake nzuri.

Msikilizaji wetu Ambrose Ongubu wa Kitongoji cha Kanyimbo sanduku la posta 1318 Kisii Kenya anasema katika barua yake kuwa, miaka na miaka amekuwa msikilizaji sugu wa idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwenye masafa mafupi, kwa takriban miezi kenda aliyoisikiliza idhaa yetu ameridhishwa na kuridhika na vipindi vyetu vilivyojaa mafunzo na burudani chungu nzima, habari za uhakika na mawimbi yanayopasua fikra. Ndiyo maana ameamua kutuenzi ipasavyo. Yeye ambaye ni mwalimu mhitimu ana kikundi cha wanachama 37 kwa jina la Kanyimbo the sky is our limit ambacho yeye katibu wake. Wanachama wengine ni wanafunzi, wafanyabiashara, wakulima na walimu. Anasema watafurahi sana kama tutaweza kuwatumia stika za CRI, makala, kadi, na bahasha ili waweze kuwasiliana nasi kwa urahisi.

Tunashukuru sana Bwana Ambrose O. Ongubu na wanachama wa klabu yake, tutafanya kila tuwezalo kuwatumia makala au bahasha, lakini lazima wavumilie si rahisi kuwatumia kwa haraka. Ni matumaini yetu kuwa, watasikiliza vipindi vyetu kwa makini na kutoa maoni na mapendekezo yao juu ya vipindi vyetu, juu ya kituo cha FM kitakachozinduliwa hivi karibuni huko Nairobi, Kenya, hata wataweza kutuletea barua kupongeza kuzinduliwa kwa kituo hicho, kwani hili ni tukio kubwa katika historia ya ushirikiano kati ya China na Kenya, ambalo limefungua ukurasa mpya wa urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika.

Idhaa ya Kiswahili 2006-01-17