Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-01-18 16:28:44    
Maisha ya kijana mmoja wa kawaida yawafanya wananchi wa China wazingatie jukumu lao kwa jamii

cri

Siku hizi kijana mmoja aitwaye Hong Zhanhui amefuatiliwa sana na wananchi wa China. Katika kampeni ya kuwachagua watu 10 wa China waliowavutia watu zaidi katika mwaka 2005, kijana huyo alichaguliwa kwa kura nyingi zaidi. Maisha ya kijana huyo yamewafanya wananchi wa China wajadili kwa kina jukumu lao kwa jamii. Kijana huyo anayewavutia watu moyo alifanya nini, kwa nini maisha yake yanaweza kuishangaza jamii nzima na kuwafanya watu wazingatie jukumu lao kwa jamii?

Hong Zhanhui ni kijana wa kawaida anayeishi mkoani Henan, katikati ya China. Hivi sasa anasoma katika chuo kikuu, anafuatiliwa na watu wengi kutokana na maisha yake yenye taabu kubwa zaidi tofauti na watu wengine. Alipokuwa na umri wa miaka 12, baba yake aliyepatwa na ugonjwa wa akili alimchukua dada yake mdogo akamtupa na kusababisha kifo cha dada yake mmoja mdogo, hata alimpiga mama yake na kumjeruhi. Tangu hapo, mama yake aliondoka nyumbani. Wakati familia yake ilipokumbwa na msiba mkubwa, baba wa kijana Hong Zhanhui alimwokota mtoto mchanga wa kiume aliyetupwa, familia hiyo maskini ikakabiliwa na matatizo makubwa zaidi ya kiuchumi.

Kutokana na kukabiliwa na taabu kubwa namna hii, kijana Hong hakurudi nyuma, peke yake alibeba mzigo wa maisha ya familia. Alifanya kazi za vibarua na kufanya biashara ya rejareja; dada yake mdogo hakuna mtu aliyemtunza, hivyo alimchukua na kwenda naye kwenye chuo alichosoma, na kumwambia acheze nje ya darasa. Baada ya masomo alipaswa kumtunza baba yake aliyekuwa mgonjwa, aliishi kwa kufanya hivyo kila siku kwa miaka 12, hata hivyo masomo yake hayakuathiriwa hata kidogo, na mwaka jana alifanikiwa kupita mtihani na kusoma katika chuo kikuu. Mwezi mmoja uliopita, makala moja isemayo: "Mwanafunzi anaposoma katika chuo kikuu huku anamtunza dada yake mdogo" ilipochapishwa kwenye magazeti. Habari kuhusu maisha ya kijana Hong Zhanhui ikaenea kwa haraka kote nchini China.

Katika miaka 12 iliyopita kijana Hong alibeba majukumu mengi ambayo hakustahili kuyabeba. Lakini moyo wake wa kubeba majukumu umewavutia sana wachina wengi. Mtumishi wa serikali mjini Beijing Bwana Li Jingjie alisema:

Kijana Hong alifanya mambo mengi ambayo watu wengi hawawezi kuyafanya katika hali yenye taabu kubwa kabisa, hii ni thamani kubwa ya moyo wake. Moyo wake huo unastahiki kuigwa na kuheshimiwa na watu.

Kijana Hong hakujivuna kutokana na kusifiwa na watu, aliwaambia watu kuwa wasingevutiwa tu na moyo wake, bali wanapaswa kuchukua hatua halisi ili kuboresha maisha. Alisema:

Naona kila mtu ana upendo moyoni na anahisi jukumu lake kwa jamii, familia na yeye mwenyewe, huenda ni kutokana na sababu fulani upendo huo na jukumu aliloona vimefunikwa. Baada ya kufahamu maisha yangu, watu wengi wamegundua tena upendo huo na jukumu hilo. Natumai kuwa watu wote watachukua hatua halisi badala ya kuvutiwa tu.

Kijana Hong Zhanhui anaheshimiwa na wanafunzi wa China wanaosoma katika vyuo vikuu kwa vitendo vyake, hata amekuwa mfano wa kuigwa kwa watu wengi katika vitendo vya maadili. Watu hao wanaona kuwa, wamejifunza mambo mengi kutoka kwa kijana Hong, kutokana na vitendo vya kijana Hong wameona vitendo halisi, moyo mwema na sifa nzuri aliyo nayo, na maisha ya kijana Hong yanawahimiza vijana wa zama tulizo nazo wawe watu wanaosaidia jamii. Mwanafunzi anayesoma katika chuo kikuu cha ualimu cha Beijing Bi.Zheng Xiaoli alisema:

Hong Zhanhui alisema watu wakivutiwa na vitendo vyake wanapaswa kufanya vitendo halisi ili kuboresha maisha ya jamii yetu. Naona maneno hayo aliyosema Hong Zhanhui ni mazuri sana yanayogusa hisia zangu zaidi. Kweli kama tunavutiwa naye moyoni bila kutekeleza aliyosema, hakuna maana hata kidogo. Tunapaswa kufanya vitendo halisi vya kumsaidia Hong Zhanhui, pia kuwasaidia watu wengi wanaohitaji misaada kama Hong. Tunapaswa kueneza upendo wetu kwa watu wote wa jamii.

Kutokana na kufuatiliwa na watu wengi katika jamii, kijana Hong Zhanhui alichaguliwa kuwa mmoja kati ya watu 10 waliowavutia watu zaidi katika mwaka 2005. Bwana Lu Xiaochuan ambaye alikuwa mjumbe wa kamati ya uchaguzi wa watu 10 waliowavutia watu zaidi ambaye pia ni mkurugenzi wa taasisi ya habari ya China alisema, kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wakati uchumi ulipoendelea kwa kasi, walijitokeza watu kadha wa kadha waliotilia maanani tu maendeleo ya uchumi na kupuuza jukumu la jamii. Kuchaguliwa kwa kijana Hong Zhanhui kuna umuhimu mkubwa kwa China ya hivi sasa. Akisema:

Wakati wowote watu huweza kukutana na taabu na majukumu, wanaweza kushinda taabu au la, au wanaweza kubeba jukumu au la, hii ni nguvu inayohitajiwa rohoni mwa wachina kwa hivi leo.

Maisha ya kijana Hong Zhanhui yameonesha kuwa bado kuna matatizo na dosari katika utaratibu wa utoaji misaada na huduma za jamii nchini China. Mkurugenzi wa taasisi ya utafiti wa habari ya China Bwana Lu Xiaochuan anaona kuwa, katika siku zijazo serikali ya China inapokamilisha utaratibu wa huduma za jamii, watu wanaokaa katika hali yenye matatizo ya kiuchumi pia wanapaswa kujifunza kutoka kwa kijana Hong Zhanhui juu ya moyo wake wa kujikakamua, kujitegemea na kujiheshimu, ili kufanya juhudi za kushinda taabu na kujikwamua kiuchumi.

Baada ya kutangazwa kwa maisha ya kijana Hong Zhanhui na vitendo alivyofanya, watu wengi wa China walitoa misaada kwa njia mbalimbali, lakini kijana Hong alirudisha pesa nyingi alizosaidiwa na watu, juu ya pesa zile alizosaidiwa ambazo hajui ni nani walimsaidia, kijana Hong ameamua kuanzisha mfuko mmoja ili kuwasaidia watu wengine wanaohitaji zaidi misaada.

Idhaa ya kiswahili 2006-01-18