Tarehe 12, Januari, serikali ya China ilitoa waraka wa sera ya China kwa Afrika, ambao unaeleza malengo ya sera za China kwa Afrika, kuweka mipango kuhusu ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta mbalimbali katika siku za usoni, na kuhimiza uhusiano kati ya China na Afrika kupata maendeleo yenye utulivu na ya muda mrefu. Waraka huo umekaribishwa na nchi mbalimbali za Afrika.
Balozi wa Angola nchini China Bw. Joao Manuel Bernardo alisema, waraka wa sera ya China kwa Afrika ni waraka unaostahili kuaminika, na unaotia nguvu na ujasiri kwa nchi za Afrika.
Bw. Bernardo alisema, "Waafrika wanaweza kuamini kuwa, China ni rafiki wa dhati kwa watu wa Afrika, na Afrika itaweza kupata maendeleo kutokana na misaada ya China."
Bw. Bernardo alieleza kuwa, waraka huo umesisitiza kuwa, misaada inayotolewa na China haina masharti, hivyo inaaminiwa na nchi za Afrika.
Baada ya vita vya ukombozi wa taifa vilivyodumu kwa miaka 14 na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka 27 nchini Angola, hivi sasa nchi hiyo inahitaji kufanya ukarabati mkubwa wa uchumi. Bw. Bernardo alisema, mwaka 2003 China na Angola zilisaini Makubaliano ya jumla ya mikopo ya upande unaosafirisha bidhaa nje, na China imetoa fedha zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wa uchumi wa Angola.
Alieleza kuwa mashirika ya China yanafanya uwekezaji nchini Angola siyo kunyang'anya maliasili au "Ukoloni mambo leo" kama baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za magharibi vinavyosema. Alisema China itaendeleza maliasili za Angola huku ikileta maendeleo ya nchi hiyo na kuwafanya wananchi wake waweze kutumia maliasili za kimaumbile, na ushirikiano wa namna hiyo unanufaisha pande zote mbili.
Mashirika ya China yanashiriki kwenye ukarabati wa uchumi nchini Angola katika sekta mbalimbali zikiwemo mafuta, kilimo, maji kunywa, uvuvi, mfumo wa umeme, upashanaji habari, ujenzi wa barabara, reli, hospitali, ujenzi wa shule na miundo mbinu.
Bw. Bernardo alisema kuna uwezekano kwamba China haiwezi kupata faida kubwa katika sekta hizo, lakini uwekezaji huo wa China unatoa misaada mikubwa kwa Angola inayokabiliwa na matatizo makubwa.
Bw. Bernardo alieleza kuwa uwekezaji wa mashirika ya China umevunja ukiritimba wa nchi za magharibi nchini Angola, na kuleta ushindani na kutia uhai kwa uchumi wa Angola. Alisema bidhaa na huduma za China zina bei chini, muda wa ujenzi ni mfupi, tena una sifa nzuri ambao unawaletea wananchi wa Angola fursa za ajira.
Alisema "Nchini Angola, mashirika ya China hayachukuliwi kama ni tishio, bali yanasifiwa na wananchi wa Angola kutokana na bei chini, sifa nzuri na kasi kubwa."
Bw. Bernardo alisema wananchi wa China waliwapa uungaji mkono mkubwa wananchi wa Angola katika mapambano ya nchi hiyo ya kujipatia uhuru kwa muda mrefu. Hivi sasa hakuna mashaka yoyote kuwa China itatoa misaada wakati Angola inapofanya ukarabati.
Bw. Bernardo alisema uhusiano kati ya China na Afrika ni wa kunufaisha, na uwekezaji wa China nchini Angola unanufaisha pande zote mbili. Alisema maendeleo ya China siyo tishio kwa dunia wala Afrika, na maendeleo ya China yamefanya waafrika waamini kuwa nchi zote zikiwemo nchi za Afrika zina fursa ya kupata maendeleo na ustawi.
Mwanadiplomasia mwingne wa Afrika ambaye ni balozi wa Tunisia nchini China Bw. Muhammed Basri alisema, waraka wa sera ya China kwa Afrika utasaidia kuimarisha na kupanua ushirikiano wa kirafiki kati ya China na nchi za Afrika.
Balozi Basri hivi karibuni alisema, amepata toleo la kiingereza na kifaransa la waraka huo, na amesoma kwa makini mambo halisi ya waraka huo.
Bw. Basri alisema China inatilia maanani kukuza uhusiano kati yake na nchi za Afrika katika muda mrefu uliopita, na imekuwa ikishikilia kuwa nchi zote kubwa au ndogo zinapaswa kuheshimiana, na kutoingiliana mambo ya ndani. Waraka huo ni kumbukumbu ya sera za China kwa Afrika katika muda mrefu uliopita, vilevile ni kanuni ya utekelezaji ya kukuza urafiki na ushirikiano kati ya China na Afrika katika kipindi kipya.
Bw. Basri alisema, ingawa China na Tunisia ziko mbali sana, lakini urafiki kati ya nchi hizo mbili unapunguza umbali huo. Katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa nchi hizo mbili wamekuwa wakiwasiliana, na ushirikiano wa kiuchumi umekuwa ukiongezeka. Wafanyabiashara wa China wanaowekeza vitega uchumi nchini Tunisia wamekuwa wakiongezeka, kwa upande mwingine, Tunisia vilevile ina mradi wa utengenezaji wa dawa za kilimo nchini China. Tangu China ilipokubali Tunisia kuwa nchi inayowapokea watalii kutoka China, ubalozi wa Tunisia nchini China ulianzisha ofisi ya utalii, ili kutoa huduma kwa watalii wa nchi hizo mbili.
Bw. Basri ambaye amekuwapo China kwa karibu mwaka mmoja anafahamu kiarabu, kifaransa na kifaransa. Alisema hivi sasa anajifunza kichina, na anatumaini kuwa atatoa mchango mkubwa zaidi katika kukuza uhusiano kati ya China na Tunisia.
|