Ukienda kwenye sehemu ya kusini magharibi mwa China wanakoishi watu wa kabila la Wayi, utawaona wanawake wa kabila hilo waliovaa sketi zenye malinda hapa na pale. Wimbo mliosikia ulieleza uzuri wa wanawake waliovaa sketi zenye malinda.
Wanawake wa kabila la Wayi wanaanza kuvaa sketi zenye malinda tokea utotoni mwao. Watoto wa kike huvaa sketi nyeupe zenye malinda zilizopambwa kwa mistari miwili myeusi kwenye sehemu ya pindo, wanapoingia kwenye kipindi cha ujana hufanyiwa sherehe ya shangwe ya kubadilisha sketi. Msichana wa kabila la Wayi Bi. Shana alisema:
"Wasichana wanapofikia umri wa miaka 17 wanafanyiwa sherehe ya kubadilisha sketi. Kwenye sherehe hiyo wasichana wanabadilishwa sketi zenye malinda ambazo ni za rangi mbalimbali za nyekundu, buluu na manjano. Mitindo ya sketi pia inabadilika, zinaundwa na sehemu tatu badala ya sehemu mbili walizovaa utotoni, sehemu ya chini ni pana na inachanua zaidi. Misuko yao ya nywele na hereni pia inabadilika, wasichana vijana wanasukwa nywele zao kuwa mikia miwili inayowekwa nyuma ya masikio, badala ya mkia mmoja waliosukwa utotoni unaokaa nyuma, kufungwa kichwa chao kwa kitambaa na kuacha paji la uso wazi.
Kwenye maskani ya Bi. Shana ya wilaya inayojiendesha ya kabila la Wayi ya Liangshan, kusini magharibi mwa China, sherehe ya kubadilisha sketi ni ya shangwe kubwa kwa wanawake wa kabila la Wayi. Baada ya sherehe hiyo, watoto wa kike wa kabila la Wayi wanaingia rasmi katika kipindi kizuri cha ujana. Sketi yenye malinda ya rangi mbalimbali, kitopu cheusi chenye pindo za rangi, mavazi hayo pamoja na hereni za fedha zinamfanya msichana aonekane ni mwembamba na mrembo. Anaweza kushiriki kwenye shughuli za aina mbalimbali za jamii, kuimba nyimbo na kucheza dansi kama apendavyo, na kuwasiliana na mvulana anayempenda. Lakini Shana alisema, nyuma ya uzuri huo kuna huzuni kubwa:
"Baada ya kubadilishwa sketi, wasichana wa kabila la Wayi hawaruhusiwi kushiriki shughuli za kidini nyumbani, hii imemaanisha kama wamefukuzwa nyumbani kabla ya kuoelwa."
Watu wa kabila la Wayi wanaabudu miungu, mababu waliokufa na dunia ya maumbile, kila mwaka wanafanya shughuli za kidini nyumbani mara kadhaa. Wasichana baada ya kubadilishwa sketi wanatambuliwa kuwa wataolewa muda mfupi baadaye, wakishiriki kwenye shughuli za kidini nyumbani wataleta bahati mbaya kwa ndugu zao wa kiume, hivyo hawaruhusiwi tena kuwepo wakati shughuli hizo zinapofanyika.
Jambo muhimu kabisa katika maisha yote ya wanawake wa kabila la Wayi ni ndoa. Kiasi cha sketi zenye malinda, sifa ya sketi na ustadi wa ushonaji vyote vinatambuliwa kuonesha uhodari wa bibi arusi. Hivyo kabla ya kufunga ndoa, wasichana wa kabila la Wayi hushona sketi za aina mbalimbali zenye malinda kwa vitambaa vya sufu.
Kwa nini wanawake wa kabila la Wayi wanapenda kuvaa sketi zenye malinda? Mtaalamu wa kabila hilo Bwana Mahairigu alisimulia hadithi ya mapokeo akisema:
"Hapo zamani za kale, wanawake wa kabila la Wayi walikuwa hodari sana, waliweza kufanya kazi zote za nyumbani, hivyo waliwaoa wanaume. Wanawake wakiiga umaalum wa sura za wanyama dume kuwashinda wanyama jike kama wa tausi, kuku pori na paa, walishona sketi zenye rangi na sehemu kadhaa kwa kutumia manyoya na ngozi za wanyama kuwa mavazi ya kindoa ya waume wao. Baadaye kutokana na wanaume kupenda kula sana chakula na kung'ang'ania nyumbani kwa wanawake, kiongozi wa kike alitoa amri kuwa, kabla ya kuolewa wanawake wanapaswa kufunga kwa siku tatu, na wanaume wanapaswa kubeba wajibu zaidi wa nyumbani. Tangu hapo wanawake wa kabila la Wayi wanatengeneza sketi za manyoya zenye rangi mbalimbali kwa ajili yao wenyewe wakati wa kuolewa. Kutokana na maendeleo ya binadamu, sketi za manyoya zimebadilishwa kuwa sketi za vitambaa zenye malinda.
Bw. Mahairigu alisema hadi leo, baadhi ya wanaume wa kabila la Wayi wanavaa suruali zenye miguu mipana kama sketi, na wanawake wanafuata desturi ya kufunga kwa siku tatu kabla ya kuolewa.
Kwa sababu hali ya hewa ya sehemu ya kusini magharibi mwa China haina baridi, hivyo wanawake wa kabila la Wayi waishio vijijini wanavaa sketi mwaka mzima. Lakini wanawake wengi waishio mijini wameacha kuvaa sketi zenye malinda isipokuwa katika sikukuu muhimu za kabila la Wayi, siku za kawaida wanapenda kuvaa mavazi yenye mitindo ya kisasa.
Baada ya kuolewa, wanawake wanapaswa kuchukua majukumu mengi ya kuwalea watoto, kujishughulisha na kazi za nyumbani na mashambani mpaka wazeeke, na rangi za sketi zao pia zinabadilika kuwa ya rangi ya buluu, kijivu na nyeusi.
Mwanamke wa kabila la Wayi mwenye umri wa miaka zaidi ya 70 aliyeishi katika vipindi mbalimbali Bi. Emushama alisema, yeye anavaa sketi zenye malinda katika maisha yake yote, hadi sasa yeye anaendelea kushona sketi yeye mwenyewe. Akisema:
"Siwezi kukumbuka nimevaa sketi ngapi zenye malinda. Hivi sasa nina sketi 4 zenye mistari na milia ya rangi ya kijivu na nyeusi. Pia nimejishonea sketi nitakayoivaa wakati nikifa. Sketi hiyo ina rangi nyeupe yenye pindo nyeusi, inafanana na sketi nilizovaa nilipokuwa mtoto."
Rangi ya sketi zenye malinda inaeleza maisha kamili ya wanawake wa kabila la Wayi, yaani kuanzia rangi nyeupe ya utotoni, rangi mbalimbali za maisha ya ujana, hadi rangi ya kijivu na nyeusi.
Idhaa ya Kiswahili 2006-02-06
|