Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-07 14:28:08    
Barua 0205

cri

Wasikilizaji wapendwa, Kituo cha FM cha Radio China kimataifa kimezinduliwa rasmi tarehe 28 Januari huko Nairobi Kenya, kuanzia siku hiyo matangazo ya Radio China kimataifa kwa lugha ya kiingereza, Kiswahili na kichina yanasikika kwa saa 19 kwa siku kwenye 91.9 FM huko Nairobi Kenya.

Kama alivyosema Mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian, "kuzinduliwa kwa Kituo cha FM cha CRI huko Nairobi, Kenya , hili ni jambo linalostahili kupongezwa kwa Radio China kimataifa na wasikilizaji wake wote".

Kwa kupitia matangazo yetu, marafiki zetu si kama tu mtaweza kuelewa kwa wakati hali kuhusu ujenzi wa uchumi wa China, maendeleo ya jamii na maisha ya utamaduni nchini China, bali pia mtaweza kufahamishwa kuhusu mawasiliano ya kirafiki kati ya China na Kenya na nchi nyingine za Afrika pamoja na matukio makubwa yanayotokea katika sehemu mbalimbali duniani. Na tunawakaribisha wasikilizaji wetu wasalimiane na jamaa na marafiki kwa kupitia matangazo yetu.

Mkurugenzi mkuu Wang Gengnian alisema, ingawa China na Kenya ziko mbali, lakini rafiki wa jadi na mawasiliano ya kiuchumi na kiutamaduni kati ya wananchi wa nchi zetu mbili yalianza tangu enzi na dahari. Mapema miaka 600 iliyopita, mwanamaji maarufu wa China Zheng He aliongoza kikosi cha merikebu kuwasili Kenya na utamaduni wa China na bidhaa za China pamoja na urafiki wa dhati wa wananchi wa China kwa wananchi wa Kenya.

Mkurugenzi mkuu wa CRI Bwana Wang Gennian alisema, katika miaka ya hivi karibuni, viongozi wa China na Kenya wanatembeleana mara kwa mara. Mwezi Agosti mwaka jana rais Mwai Kibaki wa Kenya alifanya ziara nchini China, ziara yake hiyo imeongeza zaidi maingiliano na ushirikiano kati ya China na Kenya kwenye sekta za siasa, uchumi, utamaduni na elimu, ambapo pande hizi mbili zilithibitisha mradi wa kuanzisha matangazo kwenye mitabandi 91.9 ya wimbi la FM ambalo limezinduliwa tarehe 28 Januari kuwa mradi wa ushirikiano kati ya serikali za China na Kenya.

Hivyo anasema, "sisi tutafanya juhudi kubwa kadiri kwa iwezekanavyo, ili kuandaa vizuri vipindi vyetu kwenye wimbi la FM ili kukidhi matakwa ya wasikilizaji wetu, na kuyafanya matangazo kwenye wimbi hilo kuwa dirisha la wasikilizaji wetu kuifahamu vizuri China, na kuwa daraja la kuongeza maelewano na urafiki kati ya wananchi wa China na Kenya.

Msikilizaji wetu Mogire Machuki wa sanduku la posta 646 Kisii Kenya ametuletea barua pepe akitoa pongezi za dhati kwa Radio China kimataifa kuzindua Kituo cha 91.9 FM huko Nairobi Kenya, anasema hongera sana Radio China kimataifa kwa mafanikio yake hayo.

Na msikilizaji wetu Adson Gamba pia anasema katika barua yake pepe kuwa, anapenda kuungana na wasikilizaji wenzake wa Radio China kimataifa na watangazaji wote wa radio hiyo katika kuadhimisha sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China kwa kalenda ya kilimo ya China, pia anatoa pongezi zake za dhati kwa juhudi za Radio China kimataifa zilizofanywa mwaka 2005-06.hadi kufikia kilele cha ufunguzi wa kituo cha fm 91.9 nchini Kenya tarehe 28 Januari.

Anasema ni matumaini yake makubwa kuwa Radio China kimataifa itazidi kuboresha matangazo yake kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na kuleta ufanisi kama matokeo mazuri kwa wasikilizaji wake. Katika kuadhimisha sikukuu ya mwaka mpya napenda kuwasalimia wafuatao; Mbaruku msabaha na Ali Ghasan wa Falme za Kiarabu, Beatris Mgeni wa Mbeya Tanzania, Gulam Haji Karim wa Zanzibar, Lavi Mamboleo wa Arusha Tanzania, Kilulu Kulwa wa Shinyanga Tanzania, Godfrey Mwanyama , Mtoto Happiness Julius na Franz Manko Ngogo walioko Tanzania. Ujumbe wake unasema, anawatakia maisha marefu mwaka 2006.

Na msikilizaji wetu Franz Manko Ngogo wa klabu ya wasikilizaji ya Kemogemba sanduku la posta 71 Tarime Mara Tanzania anasema katika barua pepe aliyotutumia kuwa, Ndugu wa CRI Idhaa ya Kiswahili nawapa mkono wa heri kwa kufungua kituo cha FM hapo Nairobi Kenya. Anasema yeye ni msikilizaji wa siku nyingi na amefurahishwa na harakati za muda mrefu na ushirikiano mzuri uliopo kati ya serikali mbili za China na Kenya. Hayo na mengi ambayo Radio China kimataifa imewafanyia wasikilizaji wake hakika hatayasahau na yuko nasi bega kwa bega kuuendeleza urafiki kati yangu na Radio China kimataifa. Anasema ama kwa upande wa klabu yake ya Kemogemba wao wako kigongo na Radio China Kimataifa kila leo ndio moto wetu. Anamaliza kwa kusema idumu CRI.

Tunawashukuru sana wasikilizaji wetu hao waliotuletea pongezi kwa kuzinduliwa kwa Kituo cha FM cha Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya. Ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu wengi watatuletea maoni na mapendekezo, ili tuandae vizuri vipindi vyetu.

Kutokana na ahadi yetu, leo tunapenda kutoa maswali mawili kuhusu matangazo yetu kwenye 91.9 FM Nairobi Kenya, maswali hayo ni:

1. Je, Matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China kimataifa kwenye 91.9 FM huko Nairobi Kenya yalianzia lini?

2. Mnaweza kutaja maneno machache aliyozungumza mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa katika pongezi zake kwa kuzinduliwa kwa kituo cha FM huko Nairobi Kenya?

Kama mmesikiliza kwa makini leo katika kipindi hiki cha sanduku la barua, kweli tumerudia maneno yake aliyosema siku ya kuzinduliwa kwa kituo cha FM cha CRI.

Wiki ijayo tutaendelea kutoa maswali mawili, wasikilizaji wetu watakaosikiliza kwa wiki 3 mfululizo kipindi hiki na kujibu vizuri maswali yetu, watapewa zawadi ndogondogo katika siku za baadaye.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-07