Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-09 20:13:01    
Mwanamke anayefuatilia mitindo ya kisasa

cri

Mzee Bao Qian ni mwanamke anayefuatilia mitindo ya kisasa. Yeye ni mkazi wa mji wa Hangzhou, mkoani Zhejiang, mashariki mwa China. Bibi Bao Qian mwenye umri wa miaka 73 anajua kutumia kompyuta, kuongea lugha ya Kiingerea na kuendesha magari. Amini usiamini, mzee huyo alianza kujifunza hayo yote baada ya umri wa miaka 60. Elimu hizo zimechangia kubadilisha hali ya maisha yake na kumletea raha kubwa.

Hangzhou ni mji maarufu sana nchini China ambao unajulikana kwa kuwa na ziwa moja la kupendeza liitwalo "Xihu". Mzee Bao Qian anaishi karibu na ziwa hilo. Mwanamke huyo si mrefu wala mnene, akiongea na watu husema kwa haraka na ufasaha na anaonekana ni mzee mwenye akili nyingi. Ni vigumu kuamini kuwa ana miaka zaidi ya 70 bila ya kutizama uso wake.

Huang Zhou ni mji wa utalii, unasifiwa kama pepo ya duniani kutokana na mandhari nzuri na mazao mengi. Mzee Bao Qian anajiona ni mwenye bahati kuwa mkazi wa mji huo.

"Tunajiburudisha katika mandhari inayopendezwa ya Hangzhou pamoja na sifa zake mbalimbali. Nafurahia sana hali hii. Wageni wengi wanasema, wakazi wa Hangzhou ni wenye bahati. Moyoni mwangu najiuliza mara kwa mara kuwa, 'Je, unaipenda Hangzhou?' Najibu ndiyo. Lakini halitoshi. Nikiwa mkazi wa mji huu, inanibidi nichangie uzuri wake."

Kabla ya kustaafu Bibi Bao Qian alikuwa anatunga hadithi. Anaona kuwa, mbali na ziwa Xihu, hariri na chai maarufu aina ya Longjing, Hangzhou ina mambo mengine mengi yanayowavutia watu. Kwa hiyo miaka mitano iliyopita, alitunga mpango kuwa, katika muda wa mwaka mmoja atakuwa anatembelea ama sehemu moja ya utalii ama familia moja kila siku, na kuandika makala kuhusu mambo hayo. Anatumai kuwa watu watapata sura kamili ya mji wa Hangzhou kutokana na makala zake.

Mlimbikizo wa makala hizo umepewa kichwa kisemacho "Kutembeatembea mjini Hangzhou katika siku 365". Makala hizo zimetangazwa kwenye mtandao wa Internet na kuwavutia wasomaji wengi.

Miaka 13 iliyopita wakati Bibi Bao Qian alipokuwa na umri wa miaka 60, alianza kujifunza kutumia kompyuta kutokana kupenda utungaji na uandishi wa makala. Wakati huo huo kompyuta zilikuwa zinaanza kuingia katika maisha ya Wachina, ambapo mzee huyo alikuwa na hamu ya kutumia nyenzo hiyo ya kisasa. Baada ya kusoma kwa bidii kwa kipindi fulani, Bibi Bao Qian alipata ustadi wa kuandika maneno ya Kichina kwenye kompyuta na mbinu za kuhariri makala, kiasi ambacho aliwafundisha wakazi wenzake masomo ya komputa bila malipo.

"Nikipata ustadi ningependa kuutumia. Naona kuwafundisha wakazi wenzangu ni jambo zuri, kwa hiyo niliwaandalia semina ya mafunzo ya kompyuta. Mpaka sasa imeshapita miaka mitatu na zimefanyika semina 5. Na waliohudhuria ni pamoja na mzee mwenye umri wa miaka 78 na kijana mwenye umri wa miaka 20. "

Alipokuwa na umri wa miaka 65, Bibi Bao Qian alifunga safari kwenda London kutokana na mwaliko wa mpwa wake anayefanya kazi nchini Uingereza. Alikuwa hafahamu lugha ya Kiingereza, akajiona kama mtu ambaye hajui kuongea wala kusikia, hali ambayo ilimpa taabu kubwa katika kuwasiliana na wenyeji. Aliporudi kutoka Uingereza, Bibi Bao Qian alianza kujifunza Kiingereza. Sasa anaweza kuongea sentensi za Kiingereza zinazotumika sana katika maisha ya kila siku.

Katika mji wa Hangzhou, kuna wazee wachache wenye umri zaidi ya miaka 60 wanaojifunza kuendesha magari. Bibi Bao Qian alipokuwa na umri wa miaka 69 alifanya uamuzi mkubwa wa kujifunza kuendesha magari. Siku chache tu kabla hajatimiza umri wa miaka 70, mzee huyo alipewa leseni kuendesha magari, jambo ambalo lilimfanya awe mzee pekee mwenye umri zaidi ya miaka 70 ambaye bado anaendesha magari katika mji wa Hangzhou. Bibi Bao Qian alianza kuburudishwa na kuendesha magari.

Kabla ya kufunga safari, alipiga simu ili kukodi gari na dereva kutoka kampuni ya kutoa huduma hiyo, dereva huyo anamsaidia kushughulikia hali ya dharura. Bibi Bao Qian aliandika makala kuhusu safari zake za kuendesha magari na makala hizo zilichapishwa kwenye magazeti ya huko ili wakazi wengine waburudike kwa pamoja.

Bw. Qian Keng ni dereva ambaye alishirikiana mara kwa mara na Bibi Bao Qian katika safari ya kuendesha magari, na wamejenga urafiki. Bw. Qian anamsifu sana Bibi Bao kwa ustadi wake wa kuendesha magari na desturi yake ya kuonesha mwenye furaha siku zote.

"Kusema kweli, sasa anaendesha magari vizuri, alijifunza kwa makini. Kila alipokuwa na matatizo, aliyachambua mpaka yaeleweke kabisa. Ametimiza umri wa miaka 73 mwaka huu, hata hivyo anaonekana kama kijana, kiasi kwamba sijisikii kama nawasiliana na mzee. Hakuna ugumu hata kidogo. "

Bibi Bao Qian ni mzee anayefuatilia mitindo ya kisasa. Anatumia simu za mkononi kwa kumpigia simu na kumtumia ujumbe mke wa mwanaye, pia anamtumia barua pepe mjukuu wake katika mtandao wa Internet. Anajitathmini kuwa, anapaswa kwenda sambamba na mitindo ya sasa.

"Naona tunaishi katika enzi za kisasa. Kama hamna ustadi wa kisasa, hususan kwa wazee, tunaachwa na enzi hii."

Bibi Bao Qian pia anajihusisha na huduma za jamii. Katika eneo la makazi anapoishi, yeye ni mtu anayejitolea mwenye umri mkubwa zaidi kuliko wengine. Mbali na kutoa mafunzo ya kompyuta bure, amefungua namba ya simu ya huduma ya Bibi Bao. Jumanne ni siku ya kutoa huduma, ambapo simu hiyo inasikika ikiita mara kwa mara. Wakazi wenzake wanapokabiliwa na matatizo, ama matatizo kati ya mke na mume au matatizo ya milango na madirisha, wanapenda kutafuta msaada kwa Bibi Bao. Ili kumsifu, mji wa Hangzhou ulimpa sifa ya mtu anayejitolea kueneza sayansi na teknolojia, na wakazi wenzake pia walimchagua kuwa mtu anayechangia maendeleo ya eneo la makazi.

Mzee Bao Qian ana watoto watatu wa kiume, ambao wanapenda kuona maisha ya mama yao yanayojaa furaha. Mtoto wake wa pili Bw. Meng Yang alisema, "Mama yangu anapendelea mambo ya kisasa. Anatilia maanani maisha yenye sifa nzuri na furaha kubwa zaidi kuliko kuishi kwa miaka mingi. Katika umri wake huo mkubwa, anajitahidi kujifunza mambo mapya na kupata mafanikio, tunafurahi sana."

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-09