Kuharakisha maendeleo ya sekta ya utamaduni nchini China ni suala lililozungumzwa sana katika Baraza la Mashirika la Utamaduni lililofanyika kwa siku mbili na kumalizika tarehe 8 mjini Beijing. Kwenye baraza hilo wajumbe wa nyanja mbalimbali walisema, mashirika ya utamaduni ni idara za kupata faida kubwa za kiuchumi.
Mwaka 2005, kijana mmoja wa China alitikisa dunia nzima, kijana huyo ni Li Hongyan, mkuu wa shirika la teknolojia ya mtandao wa Baidu. Hisa za shirika hilo ziliuzwa katika soko la NASDAQ nchini Marekani, kwa siku moja tu thamani ya hisa ilipanda kwa mara zaidi ya tano, shirika hilo liliwasaidia watu mia moja walionunua hisa kuwa matajiri wakawa na dola za Marekani kiasi cha milioni moja kwa usiku mmoja. Mafanikio ya Li Hongyan yamekuwa yakiwahamasisha vijana wengi kushiriki kwenye shughuli za biashara ya kiutamaduni. Serikali ya China imetambua kuwa shughuli za upashanaji habari, michezo ya kitarakimu, uchapishaji wa diski za michezo ya filamu na televisheni ni shughuli zenye faida kubwa za kiuchumi. Mwaka jana serikali ya China ilitoa sera nyingi ili kuhamasisha mitaji binafsi iwekezwe katika shughuli kama hizo.
Kwenye baraza hilo lililofanyika hivi juzi, wajumbe kutoka serikalini, nyanja za taaluma na mashirika ya utamaduni walijadiliana na kupeana mawazo kuhusu namna ya kuendeleza shughuli za biashara ya kiutamaduni nchini China, mwandaaji wa baraza hilo, mkurugenzi wa kituo cha utafiti wa maendeleo ya shughuli za biashara ya kiutamaduni Prf. Ye Lang alisema, hivi sasa shughuli hizo zimekumbwa na matatizo mengi. Alisema,
"Shughuli za biashara ya kiutamaduni bado ni jambo geni nchini China. Ingawa shughuli hizo zimepata maendeleo tokea mwaka 2002, ambapo serikali imefanya uamuzi wa kuendeleza shughuli hizo, matatizo kuhusu nadharia na sera bado hazijakamilika ambazo zinataka zijadiliwe ili upatikane ufumbuzi wa kuzikamilisha."
Mwaka 2002 serikali ya China ilitangaza wazi uamuzi wa kuendeleza shughuli za biashara ya kiutamaduni. Hapo awali, idara zote za utamaduni zilikuwa zinamilikiwa na serikali. Kuanzia Desemba mwaka 2001, China imekuwa nchi mwanachama wa WTO, kadiri China inavyotimiza ahadi zake kwa WTO, nyanja za utamaduni zimekuwa wazi kwa nchi za nje na mitaji ya kuwekeza nyanja hizo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ni sawa kusema kwamba kustawisha shughuli hizo ni chaguo lisiloepukika. Hivi sasa zaidi ya nusu ya mikoa ya China inazichukulia shughuli hizo kuwa ni sekta muhimu ya maendeleo ya uchumi.
Bw. Dan Zeng ni naibu katibu wa mkoa wa Yunnan anayeshughulikia maendeleo ya shughuli za biashara ya kiutamaduni. Mkoa wa Yunnan uko kusini magharibi mwa China, utamaduni wa huko na urithi wa utamaduni wa mji wa kale wa Lijiang unavutia maelfu kwa maelfu ya watalii. Dansi na nyimbo iliyochezwa na mwanadansi mashughuri Yang Liping na wenzake hivi sasa inaoneshwa katika nchi za nje kutoka nchi moja hadi nyingine. Bw. Dan Zeng alisema, China ina utamaduni mkubwa wa kitaifa na wa kikabila, kustawisha shughuli za biashara ya utamaduni wa kisehemu ni njia ya kustawisha maendeleo endelevu. Alisema,
"Kuendeleza shughuli za biashara ya utamaduni wa kisehemu kunategemea sana uongozi na msaada kutoka serikali. Hivi sasa tunakabiliwa na matatizo matatu: Kwanza, ufahamu kuhusu utamaduni wenyewe, kwamba utamaduni una kazi za aina mbili: moja ni itikadi na nyingine ni kuzalisha mali. Pili, mfumo wa kuendeleza shughuli hizo bado haujaanzishwa. Tatu, kuna upungufu mkubwa wa wataalamu wa kuendesha biashara ya kiutamaduni."
Bw. Dan Ceng aliona kuwa mustakbali wa shughuli za biashara ya kiutamaduni hakika utakuwa mzuri.
Mustakbali unaokadiriwa kuwa utakuwa mzuri unawavutia watu wengi binafsi kuwekeza katika shughuli hizo, lakini sheria zilizo sasa hazilingani na hali ilivyo ya maendeleo yake, ingawa kuna sheria ya kijuujuu lakini hakuna sheria yenye vipengele halisi vinavyolenga hali mbalimbali zilizopo.
Kampuni ya Shan Mao ya picha za katuni ni kampuni kubwa binafsi, mkuu wa kampuni hiyo Bw. Wu Hui alisema, shirika la utamaduni linapostawi na kufikia kwenye kiwango fulani huwa linakuwa na tatizo la fedha. Alisema,
"Ingawa kampuni yetu haijaweza kushindana na kampuni ya Marekani katika utengenezaji wa picha za katuni, lakini uwezo wake ukilinganishwa na kampuni za Japan, Korea ya Kusini, umefikia kiwango chao na hata umezidi. Mashirka ya utamaduni yana mustakbali mzuri, hivi sasa mashirika hayo hayapati msaada wa fedha kutoka serikalini, na bila ya msaada wa fedha itakuwa vigumu kwa mashirika hayo kuimarika zaidi."
Hivi sasa serikali ya China imetambua tatizo hilo na kutaka kulitatua haraka. Muda mfupi uliopita, serikali ya China iliitisha mkutano wa kujadili mageuzi kuhusu mfumo wa utamaduni, kwa hiyo tuna uhakika kuwa shughuli za biashara ya kiutamaduni nchini China zitapata maendeleo makubwa katika siku zijazo.
Idhaa ya kiswahili 2006-02-13
|