Wageni wengi wanaokuja kuitembelea China wanavutiwa sana na utamaduni wake unaong'ara ambao umetia mizizi katika ardhi yake tangu enzi na dahari. Kijana mmoja kutoka Bangladesh Bw.Mahmud Hossain Taufiqe ni miongoni mwa wageni hao. Alikuja China kuendelea na masomo yake miaka minane iliyopita, sasa anaiona China kama ni maskani yake ya pili.
Mwandishi wetu wa habari alimkuta Bw. Taufige katika Chuo Kikuu cha Qinghua kilichopo Beijing. Kijana huyo kutoka Bangladesh anayeongea Kichina vizuri, alieleza jinsi anavyoipenda China na utamaduni wake. Alisema, "China ni nchi yenye utamaduni wa muda mrefu. Nikiwa mpenzi wa sanaa na utamaduni, napendelea kuishi katika nchi kama China. Nafurahi zaidi kuishi hapa nchini China. Nilirudi nyumbani mara moja, lakini nilikaa kwa muda usiozidi mwezi mmoja tu, nikakumbuka kurudi nchini China. Niliporudi China, naliona kama nimerudi nyumbani."
Tokea mwezi Septemba mwaka 1998, Bw. Taufige alianza kusoma sanaa ya kauri katika Chuo Kikuu cha Dhaka nchini Bangladesh. Kutokana kupendekezwa na mwalimu wake, alikuja China ambayo ni nchi inayozalisha vitu vya kauri kwa wingi kabisa, kuendelea na masomo yake ya sanaa ya kauri katika Chuo Kikuu cha Qinghua, ambacho ni maarufu nchini China. Baada ya kuhitimu, alifanikiwa kupita mtihani na kuendelea na masomo ya sanaa ya vioo. Kwa hiyo, akawa Mbangladesh wa kwanza wa kusomea sanaa ya vioo katika chuo kikuu hicho. Mwezi Julai mwaka 2005, Bw. Taufige aliandaa maonesho ya kazi zake za vioo, na hayo yalikuwa ni maonesho ya kwanza kuandaliwa na mwanafunzi wa kigeni katika Chuo Kikuu cha Qinghua.
Katika maonesho hayo, balozi wa Bangladesh nchini China Bw. Masud Manna alimsifu sana kijana huyo kwa mafanikio yake. (sauti 2) "Nafurahi sana kuona msanii kijana wa Bangladesh anafanikiwa kuandaa maonesho ya kazi zake katika nchi ya kigeni. Kwa maoni yangu, maonesho ya namna hii yamewatia moyo sana wanafunzi wa kigeni wanaosomea sanaa. Na siku za baadaye tungependa kutoa msaada unaolingana na uwezo wetu kwa harakati za aina hii."
Mbali na taaluma yake, Bw. Taufige anapenda kujua mambo yote yanayohusu utamaduni wa Kichina, na amepata maendeleo. Katika mwaka wa kwanza alipoanza masomo katika Chuo Kikuu cha Qinghua, kwa mara ya kwanza alipata ujuzi kuhusu maandiko ya Kichina na uchoraji picha wa kijadi wa China, akavutiwa sana na sanaa hiyo. Tokea hapo anafanya mazoezi ya maandishi ya Kichina na uchoraji picha wa kijadi wa China takriban kila siku, aidha aliwalipa walimu wa vyuo vikuu vya sanaa ili wamfundishe ustadi wa uchoraji picha wa kijadi.
Mwezi Septemba mwaka 2005, lilifanyika shindano linaloshirikisha wageni la maandiko ya Kichina na uchoraji picha katika mji wa Huzhou mkoani Zhejiang ulioko mashariki ya China. Wageni zaidi ya 100 wanaoishi nchini China, ama wanaofanya kazi au kusoma, walishiriki kwenye shindano hilo. Bw. Taufige alishika nafasi ya pili. Katika shindano hilo, alichora picha kwa mtindo wa Kichina ya mplamu wa Kichina, ambao ni maua maalumu yanayochanua wakati wa siku za baridi. Watathmini waliisifu sana picha hiyo kwamba, inaonesha tabia ya maua ya mplamu wa Kichina ya kuweza kuvumilia hali ya baridi.
Mbali na uchoraji picha wa Kichina, Bw. Taufige pia anavutiwa sana na sanaa za aina mbalimbali za kijadi za Kichina, kama vile 'Xiang Sheng' kwa Kichina, hii ni ngonjera ya kuchekesha, kiasi ambacho alijifunza kutoka kwa msanii maarufu wa 'Xiang Sheng' Mzee Ding Guangquan. Mzee huyo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, kijana huyo ni mwanafunzi mwenye bidii ambaye anapenda kumwuliza mwalimu kila anapokuwa na masuali. Mzee Ding anampenda sana mwanafunzi huyo na Bw. Taufige kwa upande wake, amezoea kumwita mzee Ding "Baba wa Kichina".
Vyombo vya habari vya China vimefuatilia jinsi Bw. Taufige anavyosoma nchini China na kuvutiwa na utamaduni wa Kichina. Jina lake limetajwa katika televisheni, radio na magazeti mbalimbali ya China. Mvulana huyo kutoka Bangladesh pia amepata mafanikio katika kuandika makala za Kichina. Mwaka 2004 shirika moja la uchapishaji la China lilikuwa mpango wa kuchapisha vitabu kuhusu maisha ya wageni nchini China, kutokana na mwaliko wa shirika hilo Bw. Taufige alishirikiana na msichana wa China Bibi An An kuandika kitabu cha kwanza miongoni mwa vitabu hivyo. Kitabu hicho kinachoitwa "Mimi ni nyota katika nchi ya kauri" kinahusu maisha ya Bw. Taufige katika Chuo Kikuu cha Qinghua. Kwenye kitabu chake, anaeleza jinsi anavyovutiwa na utamaduni wa jadi wa Kichina, hususan sanaa ya utengenezaji wa vitu vya kauri.
Mwandishi mshiriki wa kitabu hicho Bibi An An alipomtaja kijana huyo wa Bangladesh, alisema, (sauti 4) "Ana tabia nzuri sana, anafurahia kuwasaidia wengine. Kusema kweli, yeye ni mtu mwema."
Taufige alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, anajiona ni mtu mwenye bahati nzuri kwa kuwa aliweza kuja China, kujifunza utamaduni wa Kichina, naye anapenda sana China ambayo utamaduni umeenea katika kila sehemu yake. Alisema hivi sasa anajitahidi kuingia katika maisha ya Wachina wa kawaida ili apate uelewa zaidi juu ya utamaduni wa China.
(sauti 5) "Nilipokuja China, jambo la kwanza nililofanya lilikuwa ni kuwa na marafiki Wachina. Nakatambua kwamba, Wachina wana ukarimu mkubwa, na wanafurahi kuwa na marafiki wa kigeni. Pia natazama vipindi vya televisheni za Kichina. Kuna vituo vingi, naweza kuchagua na kupata mambo mengi kuhusu utamaduni wa China. Hatua ya tatu ni kutembelea sehemu mbalimbali. Natembelea nje ya Beijing, ambapo nashuhudia maisha ya wenyeji pamoja na mila na desturi za sehemu hizo, jambo ambalo linanisaidia kuelewa utamaduni wa China."
Bw. Taufige alisema atatumia muda mrefu kwa kusoma na kuishi nchini China, pia atatembelea sehemu mbalimbali na kupata marafiki wengi wa China. Kwa kuwa, ni kufanya hivyo tu, ndipo atakapoweza kuelewa vizuri China, watu wake na utamaduni wake.
Idhaa ya Kiswahili 2006-02-16
|