Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-16 18:44:47    
Hali ya maisha kwenye gereza la wanawake la Beijing

cri

Gereza la wanawake la Beijing lipo katika kitongoji cha mji huo, Daxing. Hilo ni gereza pekee katika mji huo kwa ajili ya wafungwa wanawake, ambapo wafungwa zaidi ya 900 waliothibitishwa kuwa na makosa na kuhukumiwa na mahakama adhabu ya vifungo mbalimbali.

Kwa maoni ya watu wengi kabisa, maisha katika gereza la wanawake ni ya siri, au ni ya kutisha. Lakini kwa mtazamo wa wafungwa wenyewe, maisha kwenye gereza hilo ni rahisi na matulivu. Hata baadhi yao wanaona furaha na matumaini gerezani.

Bi. Zhu Baocao, mfungwa wa gereza hilo ambaye alihukumiwa kifungo cha miaka 6 kwa kosa la kudokoa pesa za umma miaka minne iliyopita, alisema "Mwanzoni nilipofika hapa, mama yangu alipata nafasi ya kuongea nami kwa njia ya simu. Akiwa na wasiwasi mkubwa, aliniuliza nilipewa chakula cha kutosha na kama wafungwa wengine na maofisa wa gereza walinipiga?"

Bi. Zhu aliongeza kusema, "Kusema kweli, maisha ya gerezani si mabaya kama wengine wanavyofikiri. Nimekuwa naishi hapa kwa zaidi ya miaka minne. Kila asubuhi, tunakula vipande vya dough za kukaangwa au mikate ya Kichina. Chakula cha mchana ni pamoja na sahani moja ya mboga na nyingine ya nyama na wali. Wakati wa jioni, tunapewa mboga na mikate ya Kichina. "

Pia alisema, hakupigwa hata mara moja na wengine, na wakati aliposikia baridi, maofisa wa gereza walimtunza sana.

Bi. Zhu alisema, "Hata hivyo mwanzoni nilipokuja hapa nilikuwa katika hali ya kufa moyo. Nilihitimu kutoka kwa chuo kikuu kizuri na nilipata nafasi ya uhasibu katika kampuni moja kubwa ya kiserikali. Katika siku zilizopita nilikuwa na maisha mazuri. Niliposikia kuhumu mahakamani, nilidhani kuwa maisha yangu yameharibika kabisa."

Aliendelea kusema, "Maofisa wa gereza walikuwa wanazungumza nami mara kwa mara, na waliwaalika wanasaikolojia kunitibu. Siku nenda siku rudi, nilikuwa naanza kuwa na matumaini na kuwa mtulivu, na kujitia katika shughuli za uandishi. Makala zangu zilichapishwa mara kwa mara kwenye gazeti la gereza letu liitwalo "safari mpya". Pia gerezani nilijifunza ufundi wa kushona nguo, ufundi wa umeme na kazi ya kukata nywele na nikapata vyeti vinne vya kiufundi."

Katika gereza la wanawake la Beijing lililoanzishwa mwaka 1999, asilimia 41 ya wafungwa walikuwa na makosa ya kiuchumi, kama alivyo Bi. Zhu. Asilimia 25 wamefungwa kutokana na uhalifu wa jinai, kama vile kuua na kupora, na wafungwa asilimia 7.9 walifanya uhalifu wa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Miongoni mwa wafungwa hao, aslimia 24.8 walihitimu kutoka vyuo vikuu.

Bi. Li Ruihua ni mkuu wa gereza, alisema gereza hilo lina vifaa vya kisasa vya matibabu pamoja na madaktari na wauguzi wenye sifa, kwa hivyo kila mfungwa anaweza kufanyiwa uchunguzi wa afya kila baada ya kipindi fulani na kuna rekodi ya afya ya kila mfungwa.

Mkuu huyo wa gereza alisema sio tu wafungwa wenye mafua wanatibiwa kwa wakati, bali na wale wanaougua saratani pia wanatunzwa vizuri ndani ya gereza.

Kwa maoni yake, kuwafundisha wafungwa kazi za kiufundi ni miongoni mwa mambo muhimu sana, kwa sababu watakapoondoka jela, wataweza kujitegemea na kuhudumia jamii.

Ndiyo maana, gereza la wanawake la Beijing linawapatia wafungwa mafundisho ya kazi mbalimbali za kiufundi, yakiwemo teknolojia za kompyuta, sanaa ya kupanga maua, kukata nywele, uhandisi wa umeme na sanaa ya uchongaji.

Zhao Xiaojie ni mfungwa aliyefanya kazi Forbidden City, kasri la zamani la kifalme. Anawafundisha wafungwa wenzake sanaa ya uchongaji, hivi sasa ana wanafunzi 20. Alisema, "Kuwafundisha wengine sanaa ya uchongaji kunaniletea furaha na kunisaidia kupitisha muda wangu gerezani."

Bi. Zhao alijipamba na kuonekana kuwa ni mrembo. Alisema, "Tunaruhusiwa kujipamba siku za wikendi na siku za kukutana na familia zetu. Katika kila chumba cha wafungwa katika gereza hilo, kuna kioo kimoja."

Wafungwa wanaweza kuongea na watu wa familia zao mara moja kwa mwezi. Mfungwa mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Nie alisema, "Kila mwezi tunapewa Renminbi Yuan 6 hadi 8, zikiwa pesa za kununua vitu vidogovidogo. Kama hazitoshi, naomba familia yangu kuweka pesa nyingine kwenye kadi ya benki ambayo inatumika pia katika soko ndani ya gereza. Kwa hiyo maisha ya hapa si mabaya."

Wafungwa wanakaa katika maeneo tofauti ya gereza kutokana na vipindi mbalimbali vya vifungo vyao. Na katika kila eneo, kuna maktaba moja, chumba kimoja cha kukutana, chumba cha kutoa matibabu ya kisaikolojia na chumba cha burudani.

Wafungwa wanaweza kwenda kwenye chumba cha burudani kucheza karata au chesi katika siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili. Katika chumba hicho, wanaongea bila marufuku, baadhi ya wakati wanazungumzia familia zao na wakati mwingine mada zinahusu maisha yao ya siku zilizopita. Chumba cha matibabu ya kisaikolojia ni kwa ajili ya wafungwa wenye matatizo ya kufa moyo ambao wanapewa matibabu wakisaidiwa na wanasaikolojia au askari jela.

Bi. Liu Yan aliyekuwa mtumishi wa Benki ya kilimo ya Beijing alihukumiwa kifungo cha maisha kutokana na uhalifu wa udokozi. Alisema, "Matibabu ya kisaikolojia yalikuwa muhimu sana kwetu. Hali halisi ni kwamba, mwanzoni wafungwa wengi waliokuja gerezani walikuwa na viwango tofauti vya huzuni. Na baadhi ya wafungwa walikumbwa na balaa nyumbani wakati wakiwa vifungoni. "

Aliongeza kusema, "Mama yangu alifariki dunia, sababu kubwa ni kushindwa kukabiliana na ukweli wa mambo kuwa, binti yake alikuwa mfungwa, na huenda ni mfungwa wa maisha. Nilihuzunika sana niliposikia habari ya kufariki kwake. Ni matibabu ya kisaikolojia ndiyo yalinisaidia kuondokana na huzuni. "

Mkuu wa gereza Bi. Li alisema wanasaikolojia kadhaa wanakwenda kufanya kazi kwenye gereza hilo baada ya kazi, ambao wanawasaidia wafungwa kupambana na matatizo ya kisaikolojia. Kwa maoni yake, matibabu ya kisaikolojia pia ni muhimu katika kusimamia gereza.

Wizara ya sheria ya China imeyaagiza magereza zaidi ya 700 nchini kuanzisha matibabu ya kisaikolojia kwa wafungwa ili waishi na afya njema gerezani.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-16