Rais Hu Jintao wa China na Rais Faure Essozimna Gnassingbe wa Togo
Kutokana na mwaliko wa rais Hu Jintao wa China, rais Faure Essozimna Gnassingbe wa Togo amefanya ziara rasmi nchini China kuanzia tarehe 12 hadi 18 mwezi huu. Katika ziara yake nchini China kwa nyakati tofauti amefanya mazungumzo na rais Hu Jintao wa China, waziri mkuu Wen Jiabao na spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo, pia ametembelea mkoa wa Shanxi na mji wa Shanghai. Rais Faure ni mkuu wa kwanza wa nchi za Afrika kuizuru China katika mwaka huu.
Tarehe 13 alasiri, rais Hu Jintao alikuwa na mazungumzo na rais Faure katika Jumba la mikutano ya umma la Beijing, ambapo walibadilishana maoni kwa kina kuhusu uhusiano wa pande mbili na mambo yanayozihusu pande zote mbili. Kwenye mazungumzo yao, wakuu hao wawili walitathmini urafiki wa jadi kati ya China na Togo ulioanzishwa na viongozi wazee wa nchi hizo mbili, wakikubali kwa kauli moja kurithi na kuimarisha zaidi urafiki huo, na kusukuma mbele uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Togo kwenye kiwango kipya katika karne hii mpya.
Rais Hu Jintao alisema, katika miaka 34 iliyopita tangu China na Togo zianzishe uhusiano wa kibalozi, nchi hizo mbili zimepata mafanikio mazuri katika kufanya ushirikiano kwenye sekta za siasa, uchumi, kibiashara, elimu, utamaduni na afya. Togo imekuwa mshirika muhimu wa biashara wa China katika sehemu ya Afrika magharibi. Pande hizo mbili zinaelewana na kushirikiana vizuri katika mambo ya kimataifa.
Rais Faure alisema, uhusiano kati ya Togo na China unaendelea vizuri, maendeleo ya Togo katika sekta za uchumi, kilimo, elimu, na afya yanategemea maendeleo mazuri ya uhusiano huo, serikali ya Togo na wananchi wake wanaishukuru serikali ya China kwa kuipatia misaada katika miaka mingi iliyopita. Serikali ya Togo siku zote inashikilia sera ya kuwepo kwa China moja.
Rais Hu Jintao alisema, hivi sasa uhusiano kati ya China na Togo umeingia katika kipindi kipya cha maendeleo. China inapenda kuimarisha maingiliano ya kirafiki kati ya serikali, vyombo vya utungaji sheria na vyama tawala vya nchi hizo mbili, kutilia maanani kuzidisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta za kilimo, ujenzi wa miundo mbinu, mawasiliano ya simu na umeme, utamaduni, elimu, afya na uendelezaji wa nguvukazi. Kuelewana na kuungana mkono kuhusu mambo yanayohusu maslahi ya kimsingi ya kila upande, na kushirikiana vizuri katika mambo ya pande nyingi na mambo yanayohusu maslahi ya pamoja ya nchi zinazoendelea, ili kulinda amani ya dunia na kuleta maendeleo ya pamoja.
Rais Faure alisema China imepata mafanikio makubwa katika kuendeleza uchumi na jamii, na imekuwa na uzoefu mzuri wa kukuza uchumi. Togo inapenda kuimarisha mawasiliano na China, na kufanya ushirikiano wa aina mbalimbali na China katika sekta mbalimbali.
Kuhusu uhusiano kati ya China na nchi za Afrika, rais Hu Jintao alisema, kuimarisha urafiki wa jadi kati ya China na Afrika, kuzidisha mshikamano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili, na kuziunga mkono nchi za Afrika ziungane na kujistawisha kwa kujitegemea ni sera ya siku zote ya serikali ya China. Mwaka huu mkutano wa kwanza wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika utafanyika mjini Beijing, hili litakuwa ni jambo kubwa katika historia ya maendeleo ya uhusiano kati ya China na Afrika. China inapenda kutekeleza zaidi sera zake kwa Afrika kwenye msingi wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, ili kufungua kwa pamoja ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya China na Afrika.
Baada ya mazungumzo, wakuu wa nchi hizo mbili walihudhuria sherehe ya kusaini mikataba kadhaa ukiwemo mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kiteknolojia kati ya China na Togo.
Spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo alipokutana na rais Faure alisema, maingiliano na ushirikiano wa kirafiki kati ya bunge la umma la China na bunge la Togo yametoa mchango mkubwa katika kuzidisha maelewano na urafiki wa jadi kati ya nchi hizo mbili.
Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipoonana na rais Faure alisema, China na nchi za Afrika zote ni nchi zinazoendelea, kuimarisha urafiki na uhusiano wa kiuchumi kati ya China na Afrika si kama tu kunaambatana na maslahi ya pamoja ya pande hizo mbili, bali pia kuna umuhimu mkubwa wa kimkakati kwa ushirikiano kati ya kusini na kusini na kuondokana na umaskini. Japokuwa China bado ni nchi inayoendelea, lakini China itafuata ahadi yake kuendelea kutoa msaada wa kiuchumi kwa nchi za Afrika ikiwemo Togo kadiri iwezekanavyo.
Tarehe 16 rais Faure na msafara wake waliwasili mjini Shanghai. Alipokutana na naibu meya wa Shanghai Bwana Tang Jie rais Faure alieleza matumaini yake kuwa, Togo itaimarisha mawasiliano ya kiuchumi na kibiashara kati yake na China, hasa katika ushirikiano wa sekta za nguo na kilimo. Alisema lengo la ziara yake mjini Shanghai ni kutafuta ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji. Shanghai ni mji mkubwa wa kwanza wa bandari nchini China, maendeleo yake ya kiuchumi yamevutia uangalifu mkubwa duniani. Anawakaribisha wanakampuni wa China kuwekeza nchini Togo.
Idhaa ya kiswahili 2006-02-17
|