Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-20 21:22:28    
Kutembelea makazi ya watu

cri
Makazi ya Watu

China ni nchi kubwa yenye sehemu tofauti na utamaduni tofauti. Kutokana na hali hiyo makazi ya watu pia yanatofautiana.

Katika sehemu wanazokaa watu wa kabila la Han, makazi ya watu hujengwa kwa nyumba za chini zenye nyua za mraba, mfano wa ujenzi huo ni makazi yaliyopo mjini Beijing. Nyumba za chini zenye nyua za mraba mjini Beijing zimegawanyika kuwa ua wa mbele na ua wa nyuma. Nyumba iliyopo katikati ua wa mbele na ua wa nyuma ni ya heshima kabisa, ni mahali pa kufanyia sherehe za familia, na kupokelea wageni wa heshima. Nyumba zote pembeni mwa ua wa mbele na ua wa nyuma zinaelekea katikati ya ua na zinaunganishwa kwa ujia wenye paa. Kuishi katika nyumba kama hizi ni starehe na kwa sababu ya kuishi pamoja katika nyumba hizo uhusiano wa jamaa ni wa karibu sana. Nyumba za aina hiyo zipo katika sehemu za kaskazini, na kaskazini mashariki za China.

Nyumba za Ghorofa za Udongo

Majumba ya ghorofa ya aina hiyo yanajengwa zaidi katika sehemu za kusini za China, umbo la nyumba linakuwa la duara, mraba au la yai, mithili ya ngome. Katikati ya jumba hilo ni kiwanja ambacho kuna kisima na ghala la nafaka. Milango ya nyumba ikifungwa kwa ajili ya kuzuia wezi au katika siku za vita, watu wanaoishi ndani ya nyumba hiyo wanaweza kukaa humo bila wasiwasi wa kukosa maji wala chakula kwa miezi kadhaa. Kwa kawaida nyumba kama hizo huwa na ghorofa tatu au nne.

Nyumba za ghorofa za udongo zinajengwa kwa mchanganyiko wa udongo, kokoto, mchanga na mbao, katika siku za majira ya baridi, ndani nyumba kunakuwa na joto, na katika siku za majira ya joto ndani ya nyumba kuwa na baridi, na tena ni madhubuti hata likitokea tetemeko la ardhi.

Makazi ya Watu wa Makabila Madogo Madogo

Makazi ya watu wa makabila madogo madogo pia yako aina nyingi. Makazi ya kabila la Uygur mkoani Xinjiang, kaskazini magharibi mwa China, yanajengwa kwa paa lililo bapa, kuta za udongo na ghorofa moja au mbili, na kuna ua mbele ya nyumba; Makazi ya kabila la Watibet yanajengwa kama ngome, kuta za mawe kwa nje na mbao kwa ndani na paa lililo bapa; Watu wa kabila la Wamongolia ni wafugaji, wanaishi katika mahema ambayo ni rahisi kuyahamisha kufuata malisho ya mifugo; Watu wa makabila madogo madogo katika sehemu ya kusini magharibi mwa China wanaishi katika nyumba zilizojengwa milimani karibu na maji, ghorofani wanaishi watu, na chini inaishi mifugo au kutunza vitu mbalimbali. Majumba hayo hujengwa kwa mianzi na kusimamishwa kwa nguzo bila kuwa na msingi ardhini.

Mapango na Makazi katika Miji ya Kale Kaskazini mwa China

China ni nchi kubwa yenye makabila mengi, kwa hiyo makazi pia ni ya aina nyingi. Makazi katika sehemu za mwanzo na katikati ya Mto Huanghe, mengi zaidi ni ya mapango, makazi hayo yako katika mikoa ya Shan'xi, Gansu, Henan na Shanxi. Wakazi wa sehemu hizo wanachimba mapango kwenye milima ya udongo na familia moja huwa na mapango kadhaa yanayounganishwa kwa ndani. Kwa ndani mapango hujengwa kwa matofali. Mapango hayo hayashiki moto, yanazuia kelele, na huwa na baridi wakati wa majira ya joto na joto katika majira ya baridi, na hayatumii ardhi ya kilimo.

Nchini China kuna miji ya kale ambayo mpaka sasa bado iko vilevile. Ndani ya miji hiyo kuna makazi mengi ya kale. Kati ya miji hiyo, mji wa Pingyao, mkoani Shanxi, kaskazini mwa China, na mji wa Lijing, mkoani Yunan kusini mwa China, imeorodheshwa katika kumbukumbu za urithi wa dunia mwaka 1998.

Idhaa ya Kiswahili 2006-02-20