Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-27 16:31:03    
Maisha ya utamaduni wa aina mbalimbali katika sehemu za makazi mjini Beijing

cri

Kadiri maisha yanavyokuwa bora ndivyo watu wanavyohitaji zaidi maisha ya utamaduni. Hivi sasa shughuli za aina mbalimbali za utamaduni zinafanyika moto moto katika sehemu za makazi mjini Beijing. Kila siku asubuhi na mapema, wazee karibu mia moja wanakusanyika kwenye uwanja wa sehemu ya makazi ya Haite kucheza dansi. Wazee hao ingawa wamekuwa na mvi lakini kila mmoja wao anaonekana mkakamavu. Hao ni wachezaji wa kundi la dansi katika sehemu ya Haite.

Mama Ye Daoxia ni mwanzilishi wa kundi hilo, kabla ya kustaafu alikuwa anapenda dansi, mwaka 2000 aliwashirikisha wazee na kuanzisha kundi la dansi katika sehemu yao ya makazi ili kuimarisha afya zao. Kwa kuzingatia hali ya wazee alitunga aina ya uchezaji inayowafaa na ambayo ni rahisi kwao kucheza. Hivi sasa kundi hilo limekuwa kubwa kutoka watu zaidi ya kumi hapo mwanzo hadi watu karibu mia moja wa sasa. Mama Ye Daoxia alisema, "Mtu mwenye umri wa miaka 50 hivi akiwa mvivu atazeeka haraka na ni rahisi kupata ugonjwa. Mtu huzeeka kuanzia miguu, kwa hiyo kufanya mazoezi ni muhimu kwa afya."

Kundi hili licha ya kushiriki katika maonesho ya michezo ya sanaa katika sehemu yao ya makazi, pia mara nyingi linawakilisha sehemu yao kushiriki katika michezo nje ya sehemu yao, na kila mara linashiriki kwenye shughuli za michezo ya wazee ya Beijing. Katika sehemu ya makazi ya Haite pia kuna kundi la opera ya Kibeijing. Mliyosikia ni sehemu ya opera ya Kibeijing iliyoimbwa na mkazi Wang Lianfen. Mama Wang Lianfen ana miaka 62, ni mmoja wa wachezaji zaidi ya 20 wa kundi la opera ya Kibeijing, kila Jumamosi kundi hilo hukusanyika na kufanya mazoezi na kusaidiana kiusanii kwa muda wa saa tatu, na mara nyingine wanawaalika wachezaji mashuhuri wa opera ya Kibeijing kuwafundisha. Kwa furaha mama Wang aliwaambia waandishi wa habari akisema, "Sisi sio wasanii, lakini tunafurahia maisha yetu ya utamaduni baada ya kustaafu. Tunakaa pamoja, tunajiburudisha pamoja na katika sikukuu za taifa tunapatiwa nafasi za kuonesha michezo yetu katika sehemu nyingine mjini Beijing."

Bendi hiyo ya rock'n' roll iliundwa na vijana wanne wa sehemu yao ya makazi ya Xiluo, kila mmoja ana kazi yake ofisini, wamejiunga pamoja kutokana na upendo wao wa muziki wa rock'n' roll. Katika siku za mapumziko au sikukuu za taifa bendi hiyo hufanya maonesho kuwaburudisha wakazi. Hapo mwanzo waliofurahia muziki wao walikuwa vijana tu na wazee waliduwaa, lakini sasa, wazee wengi wanapenda muziki wao na kuupigia makofi. Mkurugenzi wa kamati ya wakazi Bi. Meng Qi alisema, "Naona bendi hiyo ni nzuri sana, kwamba licha ya kuwafurahisha vijana, nayo pia inaleta uchangamfu katika sehemu yetu ya makazi."

Katika sehemu ya makazi ya Xiluo pia limeanzishwa darasa la somo la Kiingereza, mwalimu wa Kiingereza alialikwa kutoka shule iliyo karibu na sehemu ya makazi. Hivi sasa kuna wanafunzi zaidi ya 600. Mkazi Xie Shuyan ana umri wa miaka 51, tokea darasa la Kiingereza lianze hajawahi kukosa masomo yake. Hivi sasa anaweza kuongea Kiingereza na wageni kama kawaida. Mama Xie alisema, "Nia yangu ya kujifunza Kiingereza ni kutaka kutoa huduma fulani kwa wageni katika michezo ya Olimpiki mwaka 2008 mjini Beijing, na kuwafanya wajisikie kama wako nyumbani kwao."

Katika sehemu nyingine ya makazi ya Qingqing kuna majumba 27 ya ghorofa na wakazi karibu 2,000. katika sehemu hiyo kuna nyumba za michezo, maktaba na nyumba za kusomea, na kuna uwanja wa shughuli za utamaduni wenye eneo la mita za mraba elfu 20.

Mjini Beijing kuna sehemu nyingi za makazi kama hizo ambazo kwa kufanya shughuli mbalimbali kustawisha maisha ya utamaduni ya wakazi.

Idhaa ya kiswahili 2006-02-27