Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-02-28 15:21:20    
Barua 0226

cri
Leo kwanza tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa Bwana Wang Gengnian na msafara wake wamefika Nairobi Kenya tarehe 25, na wanatazamiwa kushiriki kwenye sherehe ya kuzinduliwa rasmi kwa kituo cha FM cha Radio China kimataifa tarehe 28 huko Nairobi Kenya, ambapo pia watakutana na wasikilizaji wetu walioko huko Nairobi. Tukipata habari kuhusu ziara hiyo ya mkurugenzi mkuu wa Radio China kimataifa tutawafahamsisha.

Sasa tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Ali Hamisi Kimani wa sanduku la posta 61-40224, Othoro Kenya ametuletea shairi lake lisemalo Heko Radio China Kimataifa. Shairi lake hilo linasema:

Radio CRI Kiswahili, hongera kwa matangazo murua

Kila pembe ya dunia, husikika kwa yakini

FM, masafa poa, husikika kote ulimwenguni

Ni kosa au ni haki, kuipongeza maradufu?

Idhaa ya Kiswahili hoyee, watangazaji shupavu hoyee

Miaka zaidi ya arobaini, idhaa kuitimiza asilani

Uhusiano bora kuhimiza, CRI radio na Afrika

Ni kosa au ni haki, kuipongeza maradufu?

Wengine msiudhike, leo ninauliza

Wala msibabaike, haki yetu wasikilizaji natetea

Swali langu lisikike, msidhani nakosea

Ni kosa au ni haki, kuipongeza maradufu?

Kiswahili kukikuza maridhawa, uchina bara na Taiwan kisiwani

Idumu Radio CRI, mengi mapya kutupasha,

Afya njema Mola mpe, Mkuu wa idhaa Bwana Wang Gengnian

Ni kosa au ni haki, kuipongeza maradufu?

Msikilizaji wetu Mogire O. Machuki wa kijiji cha Nyankware sanduku la posta 646 Kisii Kenya ametuletea barua akisema, ana furaha kutuarifu kuwa wiki iliyopita alikuwa jijini Nairobi, ambako alivutiwa na matangazo ya CRI yanayosikika kwenye 91.9 FM. Bila shaka yeye kama mpenzi wa Radio China Kimataifa alihamasishwa sana na mpangilio wa vipindi kadhaa vingine, ambavyo havisikiki kwenye matangazo yetu ya masafa mafupi na yale yanayosikia kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC.

Aidha alivutiwa na kuwepo kipindi cha moja kwa moja cha wasikilizaji ambapo wanapata fursa ya kutoa maoni juu ya maswali mbalimbali yanayowakera moyoni. Shukrani za dhati kwa CRI, anasema kama kuna uwezekano anaomba wimbi hili lipanuliwe zaidi ili liwafikie wakenya wote kama ikiwezekana na sio tu watu wa Nairobi peke yake.

Kwa maoni yake ni kuwa kuzinduliwa kwa wimbi la 91.9 FM kwa njia moja au nyingine itatoa fursa thabiti kwa wakenya kufahamu kwa kina hali ya utamaduni wa China. Ni nadra kupata au kuelewa hali ya utamaduni wa nchi fulani pasipo na hali nzuri ya masikilizano kati ya mataifa husika.

Anasema ana imani kuwa 91.9 FM itaboresha hali ya urafiki kati ya China na Kenya kwa kiasi kikubwa sana. Je, ni kituo gani kitabeba jukumu la kuwaarifu wasikilizaji kwa njia iliyo ya ufasaha utamaduni unaovutia wa kichina kama sio CRI yenyewe? Anasema wao wasikilizaji wa kituo hiki, watakienzi na kukithamini kwa vyovyote daima, na 91.9 FM idumu daima na izidi kutambaa kote kila pembe ya Kenya

Bwana Machuki anasema, anatarajia kukutana na ujumbe maalum wa Radio China kimataifa huko Nairobi mwishoni mwa mwezi huu iwapo atachaguliwa kutunikiwa zawadi kwenye chemsha bongo kuhusu usikivu wa matangazo ya 91.9 FM ya CRI.Pia anatuambia kuwa, huko Kisii Kenya wanaendelea kufuatilia vipindi na matangazo ya Radio China kimataifa kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC. Kuzinduliwa kwa kituo hiki tarehe 28 Januari mwaka 2006 sambamba na sikukuu ya mwaka mpya wa jadi wa China, inamaanisha kuwa Radio China kimataifa imepiga hatua na kuwa shirika la kwanza la utangazaji kutoka Bara la Asia kumiliki kituo cha FM nchini Kenya. Kuchaguliwa kwa Nairobi kama ufunguaji mlango wa vituo vingine vya FM kwenye mataifa mengine, ni jambo ambalo wakenya wanapaswa kujivunia.

Anasema Mkuu wa Radio China kimataifa alisema kwenye hotuba yake kuwa, taifa la Kenya hivi sasa ni kivutio kwa watalii wa China hasa ukizingatia historia ya miaka 600 ya mchina Zheng He. Zheng He ni mchina maarufu wa Karne ya 16 aliyeongoza merikebu ambazo ziliwahi kufanya ziara mara kadhaa kwenye pwani ya Kenya. Historia imedhihirisha kwanza kwenye pwani ya Kenya kunapatikana jamii moja ambayo asili yake ni ya China. Uhusiano kati ya China na Kenya ni wa zaidi ya miaka 40, na thibitisho ni kwamba karibu asilimia 40 na zaidi ya bidhaa wanazotumia hapo Kenya zinatokana na China.

Anasema wazo la kufungua kituo cha FM ni hatua bora na hii inamaanisha zaidi ya wakenya milioni mbili watafuatilia matangazo bila tatizo la usikivu. Hii ni changamoto kwa watu wote. Kwa wale ambao wako nje ya Nairobi bado wameridhika na matangazo ya CRI ambayo husikika kupitia shirika la utangazaji la Kenya KBC. Hii ni ishara kwamba Radio China kimataifa inawajali wasikilizaji wake wa mbali na karibu.

Anasema China ni taifa ambalo lina na historia ya miaka mingi, historia ambayo ni ya kuvutia, historia ambayo si rahisi kuisikia kwenye vyombo vingine vya habari. Utamaduni wa China daima ni wa kuvutia sambamba na sera za utawala wa serikali kuu ya China, ambapo kituo cha 91.9 FM Nairobi kitakuwa daraja muhimu la kutekeleza haya yote. Anasema ni wapi utapata kuburudika na muziki taratibu na wa jadi wa kichina kama sio Radio China kimataifa? Pia anasema kwenye tovuti yetu alipata fursa ya kusoma hotuba mbalimbali za viongozi wa ngazi za juu kutoka Radio China kimataifa na zaidi. Lakini Bwana Machuki anasema, bado hatujafahamisha kwa undani historia halisi ya kituo hiki, kiko eneo gani la Nairobi? Na je, kuna uwezekano wa kuyawezesha matangazo hayo kutanda Kenya nzima?

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Machuki kwa barua yake na maoni yake, kuhusu kituo cha FM cha CRI, tunapenda kumwambia kuwa, kituo hiki kilijengwa kutokana na ushirikiano kati ya CRI na shirika la utangazaji la Kenya KBC, ndiyo shirika hilo lililoipatia Radio China kimataifa wimbi la FM kwenye mawimbi yake ya matangazo, hivyo tunaweza kusema kituo chetu cha FM kiko karibu na shirika la utangazaji la KBC. Na matangazo ya FM kwa kawaida ni matangazo ya mijini, ambayo yanasikika kwenye eneo dogo kwa usikivu mzuri, hivyo bado matangazo ya Radio China kimataifa kwenye 91.9 FM huko Nairobi Kenya hayajaweza kutanda Kenya nzima.

Msikilizaji wetu Dennis H. Gondwe wa sanduku la posta 1545 Mwanza Tanzania ametuletea barua akisema, yeye ni msikilizaji wetu sugu na wa siku nyingi sana wa idhaa yetu ya Kiswahili, ingawa kwa sasa ana zaidi ya miaka mitatu hajasikiliza matangazo yetu baada ya kukatika ghafla, na tokea hapo hakutupata tena. Hadi sasa hawezi kutupata na hata hajui tunapatikana kwenye masafa gani na muda gani.

Anapenda kutupongeza sana kwa kufungua kituo cha FM cha Nairobi Kenya, anasema hongera kwa kufikisha huduma hii karibu na wananchi wa Afrika mashariki. Anasema amesikia kuwa tumeanzisha jarida dogo la Daraja la urafiki pamoja na mengine anaomba tumtumie na matoleo mengine ya jarida hilo.

Tunamshukuru kwa dhati kwa pongezi zake, kweli tunasikitika kuwa usikivu wa matangazo yetu katika sehemu aliko si mzuri, siku hizi tunafanya juhudi za kuboresha usikivu wa matangazo yetu popote wasikilizaji wetu walipo, ni matumaini yetu kuwa wasikilizaji wetu watuelewe na kutuvumilia kwa muda, tuna imani kuwa tutaweza kutoa huduma nzuri kwa wasikilizaji wetu wote.

Msikilizaji weu Richard Chenibei Mateka wa sanduku la posta 65 Kapkateny Kenya anasema katika barua yake kuwa, anashukuru kwa upendo na maendeleo na uhusiano kati ya China na Kenya, anasema yeye na wasikilizaji wengine wataendeleza uhusiano huo kwa dhati. Naye anasema amepokea barua iliyomvutia sana baada ya kusikia kuwa Radio China kimataifa imezindua rasmi kituo cha FM huko Nairobi Kenya. Hayo yote aliongea kupitia maoni yake ya barua ya mwaka 1995, hata hivyo polepole ndio mwendo na sasa wakati utekelezaji umewadia na mafanikio ni kwa wakenya na Radio China kimataifa.

Anasema wanachama na wasikilizaji wa Radio China kimataifa kama yeye aliyejiunga na uanachama miaka 15 iliyopita, hata kabla matangazo ya Radio China kimataifa haijaanza kusikika kupitia KBC hadi sasa mawimbi ya FM, wameweza kujionea kuboreshwa kwa vipindi na usikivu wa matangazo ya CRI. Anasema ndoto yake kubwa ni kuona kuwa, baada ya kuzinduliwa kwa kituo hicho cha FM, bidhaa za China zinaweza kutangazwa kupitia kituo hicho.

Msikilizaji wetu huyo Richard Chenibei Mateka pia anasema, Radio China kimataifa ilianza polepole lakini sasa mafanikio yameonekana wazi ikishirikiana na Radio KBC na sasa pia inatangaza kwenye mawimbi ya FM huko Nairobi Kenya kuanzia mwaka wa 2006, ambapo huenda wasikilizaji watakuwa na uwezo wa kuongea kupitia kituo hiki cha FM, huu ni ufunguo pia wa nafasi za kazi kwa watu wa huko, wataendelea kupata ujuzi na mafanikio ya maendeleo ya wachina na watapata ujuzi na mbinu za biashara pia.

Anasema tovuti ya Kiswahili ya Radio China kimataifa pia ni moja ya mafanikio ya kuona matukio ulimwenguni na mpangilio wa vipindi ya CRI. Kutoa jarida dogo la daraja la urafiki, pia ni moja ya mafanikio ya Radio China kimataifa. Vivutio vya utalii kama vile utamaduni, sanaa, uchumi na biashara, elimu, afya na vyakula vya kiafrika na kichina ni mfano bora wa ushrikiano kati ya China na Kenya.

Anasema yeye hafanyi kazi ya serikali ya Kenya bali anashirikiana na wachina katika shughuli za utalii na kuwapokea watalii kutoka China na kuwafahamisha hali ya Kenya, ili wanaotembelea Kenya wawe huru katika shughuli za utalii.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu Richard Chenibei Mateka kwa barua zake ambazo zimetuambia hali ya shughuli zake za kuwapokea watalii wa China nchini Kenya, na tunamshukuru kwa usikilizaji wake wa makini wa matangazo yetu, ni matumaini yetu kuwa atakuwa na mawasiliano barabara nasi, anaweza kutujulisha maendeleo ya shughuli za utalii nchini Kenya

Idhaa ya kiswahili 2006-02-28