Kuonesha filamu zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kitibet ni jambo linalowafurahisha watu wa Tibet. Bibi Zholma kutoka kabila hilo alieleza kuwa anafurahia filamu hizo kwa kuwa, anapata sura ya dunia iliyo nje ya maskani yake na ujuzi unaomsaidia katika shughuli za kilimo.
Alisema, "Tunaweza kutazama filamu mara moja kwa mwezi. Ninaona mambo mengi mapya kwenye filamu hizo. Napenda sana filamu zinazotoa elimu ya kilimo. Ni rahisi kwetu kuelewa ufundi unaofundishwa kwenye filamu zikiwa na picha na sauti."
Bi. Zholma aliongeza kusema, alipata ujuzi wa kupanda mboga ndani ya vibanda vya kuhifadhi ujoto katika siku za baridi. Mbali na kutumia mwenyewe pia anauza baadhi ya mboga katika mji wa Lhasa na amechuma pesa nyingi.
Ni kweli kama alivyoeleza Bi. Zholma, hivi sasa filamu zimekuwa ni njia muhimu kwa wakulima na wafugaji wa kabila la Watibet kujipatia habari kutoka nje na ujuzi. Hasa filamu za elimu zilizotafsiriwa kwa lugha ya Kitibet zinaonesha maisha ya wakulima na wafugaji, zikiwasaidia sana katika kubadilisha mtizamo, kuboresha ufundi na kuinua kiwango cha maisha.
Wakulima na wafugaji wa Tibet wanaweza kutazama filamu kila baada ya kipindi fulani, hii inatokana na uamuzi wa serikali ya China wa kupeleka filamu vijijini. Tokea mwishoni mwa miaka ya 90 ya karne iliyopita, serikali ya China ilianzisha mpango mmoja uitwao "2131", unaolenga kuwawezesha wakulima wa vijiji vyote vya China wataweza kutazama filamu moja kwa mwezi hadi ifikapo mwanzoni mwa karne ya 21. Eneo la kilimo na mifugo lenye ukubwa wa kilomita milioni 1 na laki 2 za mraba mkoani Tibet ulipewa kipaumbele kwenye mpango huo.
Mpango huo ulianza zoezi hilo kutekelezwa mkoani Tibet mwaka 1998. Kwa kuwa wakulima na wafugaji wa kabila la Watibet wanafahamu lugha ya Kitibet tu, kazi ya kutafsiri lugha ya Kihan kwa Kitibet imeimarishwa. Meneja wa Kampuni ya filamu ya mkoa unaojiendesha wa Tibet Bw. Phagba Chozin alieleza,
"Ili kuhakikisha idadi ya filamu, idara ya kutafsiri ya kampuni yetu iliimarishwa. Tuliongeza kuwaajiri wakalimani na waigizaji wa filamu. Kutokana na maombi ya wakulima na wafugaji, tulitafsiri filamu nyingi za elimu zinazotoa ujuzi wa kilimo na ufugaji."
Meneja huyo aliongeza kuwa katika miaka ya hivi karibuni, walitafsiri filamu zaidi ya elfu moja kwa lugha ya Kitibet, zikiwa ni pamoja na filamu za hadithi na filamu za elimu.
Katika juhudi za kuwapatia wanavijiji filamu, vituo vya kuonesha filamu vilijengwa katika wilaya zote, na wafanyakazi wa vituo hivyo walipewa mafunzo ya kuonesha filamu. Sasa kuna vituo karibu 500 vya namna hii mkoani Tibet.
Mkoa wa Tibet upo katika uwanda wa juu, una eneo kubwa na milima mingi inayofunikwa na theluji. Kwa hiyo safari za kuonesha filamu zinachukua siku kadhaa kwa magari kabla ya kuwasili vijijini. Bw. Nyima Tsering ni mkuu wa kituo cha kuonesha filamu cha wilaya ya Dagze iliyopo kwenye kitongoji cha kaskazini cha Lhasa.
Alisema, "Vijiji vingi vya wilaya hii vipo mbali sana. Tunakwenda vijijini kwa magari. Hata hivyo katika baadhi ya vijiji hakuna barabara. Tunawabebesha ng'ombe au farasi wachukue vifaa vya kuonesha filamu ili wanavijiji waweze kutazama filamu za sasa zilizotafsiriwa. Kila mara tunaonesha filamu moja ya elimu na nyinigne ya hadithi katika kijiji kimoja."
Filamu ni kama uhondo wa utamaduni unaochangia maisha ya wakulima na wafugaji ambao makazi yao yupo katika uwanda wa juu. Kila ifikapo siku ya kuonesha filamu, watu wanamiminikia vijijini ama kwa farasi, ama kwa kutembea au kwa motokaa. Bw. Nyima Tsering alisema hawezi kuhesabu idadi ya vijiji alivyokwenda na filamu alizoonesha katika miaka iliyopita. Lakini hawezi kusahau kuwa, katika kila kijiji wakulima na wafugaji wanafurahia kutazama filamu na kuwang'ang'ania. Siku nyingine filamu yenyewe ikiisha, lakini wanavijiji walitaka kuitazama kwa mara nyingine tena, na wao wanaionesha tena.
Watu wa kabila la Watibet ni waumini wa dini ya Kibudha ya Kitibet, na kuna mahekalu mengi mkoani Tibet. Bw. Nyima Tsering alisema, kwa mahekalu yenye watawa zaidi ya 30 wanaonesha filamu pia katika mahekalu hayo.
Kutokana na hali duni ya kimaumbile ya Tibet na ugumu wa maisha ya wakulima na wafugaji, filamu zote zinazooneshwa kwa wakulima, wafugaji na watawa zinatolewa na serikali bila malipo. Meneja wa Kampuni ya filamu ya Mkoa unaojiendesha wa Tibet Bw. Phagba Chozin alieleza kuwa, katika miaka ya hivi karibuni, serikali imegharamia Renminbi Yuan makumi na mamilioni kununua vifaa vya kuonesha filamu, kutoa mafunzo kwa wafanyakazi na kutenga fedha katika kuendeleza shughuli za filamu mkoani Tibet. Hivi sasa, karibu kila kituo cha kuonesha filamu kina gari moja, na hali hii inawafanya wafanyakazi wapeleke vifaa na filamu vijijini kwa urahisi.
Alisema, "Sasa kati ya wilaya 73 mkoani Tibet, wakulima na wafugaji wa wilaya 69 wanaweza kutazama filamu mara moja kwa mwezi. Na siku za baadaye, tutatafrisi filamu nyingi zaidi na kuwafundisha wafanyakazi wengi zaidi wa kuonesha filamu, pia tutaboresha hali ya vituo vya kuonesha filamu, ili wakulima na wafugaji waburudishwe na filamu nyingi."
Idhaa ya kiswahili 2006-03-02
|