Katika miaka ya 80 ya karne iliyopita, Bi. Liu Xiaoqing alikuwa mwigizaji maarufu sana nchini China kutokana na uigizaji wake hodari. Lakini wakati huo alipokuwa kileleni katika uigizaji wake ghafla aliacha uchezaji wa filamu akaanza kufanya biashara, na biashara yake ilikuwa mbaya hata alitiwa gerezani kutokana na kukwepa kulipa kodi kubwa. Inawezekana kuwa alizaliwa na kipaji cha uigizaji wala sio biashara, baada ya kuachana na michezo ya filamu kwa miaka 10 amerudia tena kwenye uigizaji.
Liu Xiaoqing ana umri wa miaka 50, lakini anaonekana mwenye hamasa ya ujana, sauti na kicheko chake kinavutia kama zamani. Katika miaka 10 iliyopita, kila alipojitokeza hadharani waandishi wa habari walijiuliza: anawezaje kudumisha sura yake ya ujana? Liu Xiaoqing alijibu hivi: Kujiamini ni tabia yake.
Ni kweli kwamba Bi. Liu Xiaoqing ni mwigizaji anayejiamini. Katika nchi ya China ambayo tabia ya unyenyekevu inaheshimiwa sana, Bi. Liu Xiaoqing alisema, "Mimi ni mwigizaji hodari kabisa wa kike nchini China." Alisema hivyo hivyo hata baada ya kupita miaka 10 ya adha nyingi maishani mwake, alipozungumza na waandishi wa habari. Alisema, "Ndio, kama jambo hili likipigiwa kura nitajipigia mimi. Kwa sababu kama wewe hujiamini, basi nani atakuamini? Nimewahi kufanya kazi za aina nyingi, lakini kati ya kazi hizo inayonifaa ni kazi ya uigizaji wa filamu. Nilipata karibu aina zote za tuzo za uigizaji bora katika miaka nilipoigiza."
Bi. Liu Xiaoqing alizaliwa katika mji wa Chengdu, sehemu ya katikati ya China, wenyeji wa huko wanapenda kula pilipili, hulka yake ni kama ya pilipili ya kuongea kinaganaga bila kuficha. Mwaka 1975, kwa mara ya kwanza alipata nafasi ya kushiriki katika uchaguzi wa waigizaji kwa ajili ya filamu ya "Ukuta Mkuu katika Bahari ya Kusini". Wakati huo ulikuwa mwishoni mwa kipindi cha mapinduzi ya utamaduni nchini China ambapo filamu zilizokuwa zikitengenezwa, kwa hiyo nafasi ya kugombea uigizaji wa filamu ilikuwa ni vigumu sana kuipata, lakini uigizaji bora wa Liu Xiaoqing katika uchaguzi ulimfanya mwongozaji wa filamu hiyo amchague bila kusita sita.
Mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita, Liu Xiaoqing alichaguliwa kuwa mwigizaji katika filamu "Ua Dogo" na "Familia ya Furaha". Filamu ya kwanza ilionesha upendo kati ya kaka na ndugu yake wa kike ulivyokuwa wa kusisimua katika miaka ya vita, na ya pili ilieleza maisha ya kuchekesha katika familia moja. Uigizaji hodari wa Liu Xiaoqing uliwapa watazamaji kumbukumbu isiyosahaulika, na mpaka sasa watazamaji ambao sasa ni watu wa makamo wanakumbuka jinsi alivyokuwa katika filamu ya "Ua Dogo" iliyooneshwa miaka 20 iliyopita.
Katika mwaka 1983 na mwaka 1986 Liu Xiaoqing aliigiza katika filamu nyingi ambazo zilimpatia tuzo nyingi kutokana na uigizaji wake, kwa hiyo hata baadhi ya watu wanasema, filamu za China katika miaka ya 80 ni filamu za Liu Xiaoqing.
Mwaka 1983, Liu Xiaoqing aliandika kitabu chake cha maelezo binafsi kiitwacho "Njia Yangu". Kitabu hicho kilieleza maisha aliyopitia na safari yake ya kujitafutia mafanikio. Lakini jinsi alivyofanya juhudi binafsi na kupata mafanikio ilizungumzwa sana kwa maoni tofauti katika jamii. Baada ya kitabu hicho kuchapishwa Liu Xiaoqing alikuwa akizungumzwa sana. Alipozungumzia kitabu hicho, alisema, "Niliyoandika katika kitabu hicho ni mawazo yangu ya kweli. Mimi nina dosari nyingi, lakini dosari zenyewe si kama zilivyosemwa na nyie. Pia nina sifa nyingi, lakini sifa zangu si kama zilivyoimbwa na nyie."
Ndani ya kitabu hicho, Liu Xiaoqing kwa hisia nzito aliandika hivi, "Mwanadamu hukumbwa na matatizo, wanawake hukumbwa na matatizo mengi zaidi, na wanawake mashuhuri hukumbwa na matatizo mengi mno."
Miaka ya 80 ilikuwa miaka ya filamu za Liu Xiaoqing nchini China, na katika miaka hiyo China ilikuwa nchi iliyokuwa ikibadilika kutokana na mageuzi ya kufungua mlango kiuchumi. Wachina waliokuwa katika miaka hiyo ghafla walikabiliwa na mtindo wa aina mpya ya kimaisha na mitizamo ya aina nyingine iliyo tofauti na waliyokuwa nayo, matumaini ya maisha mapya yalikuwa yakiwachochea Wachina wote akiwemo Liu Xiaoqing kujitafutia maendeleo.
Liu Xiaoqing, mtu mwenye tabia ya unyoofu alisema, wakati huo alikuwa na tamaa kubwa ya pesa. Ili aweze kujipatia pesa nyingi, pamoja na kuendelea kucheza filamu alijitahidi kushiriki kwenye shughuli nyingi za maonesho ya michezo ya kulipwa, na wakati mwingine hata alishiriki kwenye shughuli nane katika siku moja! Katika miaka ya 90 aliacha kabisa uwanja wa filamu na kushughulikia mashirika yake zaidi ya 20 yakiwemo shirika la biashaya ya viwanja na nyumba, shirika la kutengeneza michezo ya televisheni, na kuuza kwa mnada miswada ya vitabu. Katika kipindi hicho aliwekeza na kucheza katika michezo ya televisheni zaidi ya kumi, lakini michezo hiyo ilikuwa ya kawaida kabisa. Wakati huo Liu Xiaoqing alipewa jina jingine la "Dada Tajiri wa China".
Lakini yote hayo yalikuwa kama ukungu wa asubuhi na mara ukatoweka baada ya jua kuchomoza. Mashirika yake aliyowekeza yalifilisika moja baada ya jingine, na akawa anadaiwa madeni mengi. Mwaka 2002 alitiwa gerezani kutokana na kukwepa kulipa kodi, alipitisha siku 400 jela na alipoachwa huru kwa dhamana, alidaiwa kodi karibu yuan milioni kumi.
Hata hivyo Liu Xiaoqing hakutia nanga katika safari yake ya ajabu. Baada ya kutoka gerezani alirudi tena kwenye jukwaa la michezo ya sanaa. Mwaka 2004 alichaguliwa kuwa mchezaji mkuu katika tamthilia ya "Usiku wa Mwisho wa Bw. Jin Daban", uigizaji wake katika tamthilia hiyo ulisifiwa sana na watazamaji. Katika tamthilia hiyo Liu Xiaoqing aliigiza kuwa mchezaji wa dansi aliyejichumia pesa toka alipokuwa na miaka 20 hadi 40, kwenye jukwaa Liu Xiaoqing licha ya kuimba tena alicheza dansi. Umahiri wake wa uchezaji uliwavutia watazamaji na umekubalika na jamii kama zamani. Tokea hapo alikuwa mwigizaji katika filamu nyingi.
Baada ya kupita safari ngumu Liu Xiaoqing alisema "anashukuru filamu", lakini pamoja na kusema hayo pia alisema ameelewa nini maana ya "mwigizaji filamu kuwa na shida nyingi". Alisema, "Mwigizaji filamu wa kike ana shida nyingi, ingawa anashangiliwa kwa shada la maua au kupigiwa makofi, lakini anapata hayo mara ngapi mwaka mmoja? Wakati mwingi yeye ni mpweke, anasingiziwa, anaviziwa, maisha yake hayana uhuru. Mtu anayeishi katika hali hiyo lazima awe na uvumilivu mkubwa."
Liu Xiaoqing amerudi tena kwenye jukwaa la filamu, lakini hali ilivyo leo ni kwamba, filamu za leo sio tena filamu za Liu Xiaoqing, na watazamaji wengi ni vijana ambao wanawafurahia zaidi waigizaji chipukizi. Ingawa miaka ya filamu za Liu Xiaoqing imepita, lakini safari yake ngumu inaonesha mabadiliko makubwa ya hali ya filamu nchini China katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Ni kama alivyosema kwamba matukio yake yanavutia zaidi kuliko filamu zote alizoigiza. Hata hivyo bahati yake si mbaya, kwamba aliwahi kuwapata watazamaji wengi kabisa duniani.
Idhaa ya kiswahili 2006-03-06
|