Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-14 10:03:28    
Nchini China barabara zimefika kwenye sehemu zilizoko mbali na miji inayoendelea

cri

Miaka 10 iliyopita, mfanyabiashara wa mji wa Xianyang mkoa wa Shaanxi Bw. Li Xinlin alikwenda kununua mboga katika kijiji cha Mayuan, mji wa Guyuan mkoani Ningxia, kwani alisikia kuwa kijiji hicho kinazalisha figili nyekundu kwa wingi. Baada ya kutembea milimani kwa nusu saa aliona nyumba moja ya familia ya wakulima. Alinunua figili kutoka familia moja hadi nyingine, baada ya siku kadhaa aliweza kukusanya figili zinazoweza kujaa gari moja. Lakini hali ya hewa ilibadilika ghafla na kuwa mbaya, gari halikuweza kusafiri kwenye barabara za matope, hivyo mbogo nyingi zilioza kwenye gari lake.

Bw. Li Xinlin ni mfanyabiashara wa kwanza aliyekwenda kijijini humo. Wanakijiji wa kijiji hicho walianza kupanda mboga mwishoni mwa Enzi ya Qing, lakini katika karne moja iliyopita, wanakijiji wa kijiji hicho walipeleka mboga mjini kwa punda, kila mara waliweza kubeba kilo 30 hadi 40 tu za mboga, na fedha zilizopatikana kwa kuuza mbogo hizo zilitosheleza kujikimu tu.

Kama ilivyo kwa kijiji cha Mayuan, kutokana na hali duni ya barabara, vijiji vingi vilivyoko mbali na miji nchini China vimekuwa vikikabiliwa na umaskini katika muda mrefu uliopita. Lakini kuondoa umaskini si jambo rahisi, katika sehemu ya Xihaigu kiliko kijiji cha Mayuan, bado kuna watu maskini kabisa laki 2. Meya wa mji wa Guyuan Bw. Ma Fu anaona kuwa, watu wengi hawawezi kuondokana na umaskini na kujiendeleza kutokana na hali duni ya barabara.

Mwaka 2001, barabara ya kwanza yenye urefu wa kilomita 17 ilijengwa katika kijiji cha Mayuan, gari lenye uzito wa tani 10 linaweza kuingia moja kwa moja kijijini humo. Bw. Li Xinlin alisema, "hivi sasa sina budi kununua mboga kutoka familia moja hadi nyingine, naweza kumpigia simu wakala wa wakulima, na kujadili aina na sifa za mbogo, naweza kusafirisha mboga kwa gari hata kukiwa na upepo au mvua ikiwa inanyesha.

Hivi sasa kuna mabanda 700 ya kuotesha mboga kijijini humo. Katika majira ya joto na autumn, mboga zinazosafirishwa kwenda mkoa wa Henan, Gansu na Hubei zinafikia tani 50 hadi 60 kwa siku, na wastani wa mapato ya kila mkulima umefikia yuan elfu 3 kwa mwaka.

Kwa mujibu wa takwimu, hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2005, urefu wa jumla wa barabara za lami na saruji zilizojengwa vijijini umefikia kilomita laki 6.3, na barabara hizo zimefika kwenye wilaya 278 na vijiji elfu 36. Mwaka 2001 hadi mwaka 2005 ni kipindi ambacho barabara za vijijini zilipata maendeleo ya haraka na mazuri zaidi katika historia ya China. Katika miaka hiyo mitano, China ilitenga yuan bilioni 417.8 na kujenga na kutengeneza barabara zenye urefu wa kilomita laki 3 vijijini. Barabara hizo zimezisaidia sehemu hizo kuondokana na umasikini na kujipatia utajiri.

China pia inapanga kutenga yuan bilioni 1000 katika miaka mitano ijayo ili kujenga na kutengeneza barabara zenye urefu wa kilomita milioni 1.2, ili ifikapo mwaka 2010 barabara ziwe zimefika kwenye vijiji vyote vya China. Na China itatilia mkazo kuharakisha ujenzi wa barabara katika sehemu za zamani za makambi ya mapinduzi, sehemu za makabila madogo madogo, sehemu za mipakani, sehemu maskini na sehemu zinazozalisha nafaka.

Meya wa mji wa Guyuan Bw. Ma Fu alisema, kutokana na kuboreshwa kwa hali ya barabara, bila shaka mawasiliano ya watu, uchukuzi wa bidhaa na upashanaji habari utaboreshwa, na watu wa sehemu maskini wataondoa umaskini.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-13