Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-14 15:29:08    
Barua 0314 JINSI CHUO KIKUU CHA KENYATTA NCHINI KENYA KINAVYOJITAHIDI KUIMARISHA LUGHA YA KISWAHILI

cri

Lugha ya Kiswahili inazidi kukua kila uchao na hivyo kuwalazima wahadhiri, watalaam, wanafunzi na wapenzi wote wa lugha hii kufanya juu chini kuona kuwa Kiswahili kamwe hakibaki nyuma ela kinakwenda na wakati.

Ni kwa misingi hii basi ndiposa Chuo Kikuu cha Kenyatta, cha pili kwa ukubwa nchini Kenya, kilipoamua kuzindua idara ya Kiswahili na lugha za Kiafrika. Kabla ya kuzinduliwa kwa idara hii ni kuwa kulikuwa na idara moja kubwa iliyokuwa ikijumuisha maswala kadha ikiwemo lugha za Kiingereza, Kiswahili, Fasihi na lugha za kigeni.

Lakini wahadhiri wa Kiswahili wakafanya mbinu na hapo kubuni idara yao tofauti, ambayo kwa sasa yajulikana kama idara ya Kiswahili na lugha za ki-afarika.

Kulingana na mmojawapo wa wahadhiri wa idara hii Bw. Mutegi Mokubwa, ni kuwa hii ndio idara kubwa zaidi katika vyuo vyote kote ulimwenguni. Bw. Mutegi asema kuwa idara hii ina jumla ya wahadhiri 23 na wanafunzi wapatao 1500 na ingali ikikua kila leo.

Lakini nini hasa ndicho kilichokuwa chimbuko na lengo la idara hii?

Asema Bw. Mutegi kuwa idara hii ilibuniwa hasa zaidi kwa misingi kuwa Kiswahili ni somo la lazima katika viwango vya shule za msingi na upili.

"Baada ya Kiswahili kuwekwa kama somo la lazima katika mfumo wa elimu nchini Kenya katika viwango vya shule za msingi na sekondari, tuliona kuwa idara hii itawafaa sana si wanafunzi tu, bali pia kuwapa mafunzo kabambe walimu ambao wangewafunza wanafunzi hao," akasema mhadhiri huyo.

Juhudi nyengine za idara hii zimebainika kwa kuwa wanachangia pakubwa katika maswala ya kukikuza Kiswahili katika mikutano ya kimataifa, shughuli za tafsiri na ukalimani.

Asema Bw. Mutegi kuwa ili kuwafikia kikamilifu Wakenya wote, msemaji anahitaji pakubwa lugha kama chombo cha mawasiliano, ndiposa hata vyombo vya habari, hasa zaidi vya kimataifa kama vile idhaa za Kiswahili za Redio China Kimataifa, BBC, VOA, Deutsche Welle na nyenginezo, vinafanya kila hali kuona kuwa vinatangaza kwa Kiswahili.

"Zipo lugha za kienyeji na kigeni, lakini kwa minajili ya kuufikisha ujumbe kwa mlengwa bila matatizo yoyote, inabidi msemaji kutumia Kiswahili. Hii imetokana na hali kuwa Kiswahili ni lugha ya taifa nchini Kenya, sikwambii inavyotumika kwa mapana na marefu katika mataifa ya Tanzania, Uganda, Burundi, Rwanda, Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, maeneo ya maziwa makuu na kwengineko kote barani Afrika.

Juhudi za idara hii zimeanza kuonekana pia kupitia kuanzishwa kwa vyuo vikuu vya Kiswahili katika mataifa ya Asia ikiwemo Uchina, bara la Uropa na Marekani.

Asema mhadhiri huyu kuwa majuzi katika mkutano wa mawaziri wa Utamaduni kutoka bara la Afrika, walikubaliana kwa kauli moja kuwa Kiswahili kiwe lugha rasmi ya mawasiliano katika vikao vya mataifa haya.

Baadaye katika mkutano wa marais wa bara hili uliofuatia, ikaamulika pia kwa kauli moja kuwa Kiswahili ndio lugha rasmi ambayo kwamba itakuwa ikitumika katika mikao hiyo.

"Hii ni ishara kuwa katika muda wa kama mwongo mmoja hivi ujao, Kiswahili kitaanza kutumika kama lugha rasmi katika mikutano ya Umoja wa Mataifa. Hii imechochewa pakubwa na Umoja wa Afrika kuwasilisha kwa Umoja wa Mataifa, pendekezo la Kiswahili kutumika kama mojawapo wa lugha rasmi katika makongamo ya umoja huo." Akaongozea Bw. Mokubwa.

Kwa sasa idara hii ya Kiswahili na lugha za Ki-afrika ya Chuo kikuu cha Kenyatta, imeweka mikakati ya kupanua mafunzo ya Kiswahili ili kuwafaidi zaidi watafsiri na wakalimanai katika shughuli mbalimbali za kitaifa na kimataifa, ikiwemo mahakamani na katika nyanja nyenginene za mawasiliano na shughuli za serikali na ofisini.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-14