Kabila la Waman ni miongoni mwa makabila madogomadogo nchini China. Waman wengi wanaishi katika eneo la kaskazini la China, hasa mkoa wa Liaoning uliopo kaskazini mashariki ya China. Katika historia, kabila hilo linajulikana kama kabila linalobebwa na farasi, kwa vile watu wa kabila hilo walikuwa ni hodari katika kupanda farasi na kutumia upinde na mishale. Kutokana na umaalumu huo, Waman pia walikuwa na ufundi wa hali ya juu wa kutengeneza pinde na mishale. Lakini siku nenda siku rudi, watu wanaofahamu ufundi huo wanapungua na kuwa wachache sana.
Katika mtaa mmoja uliopo mashariki ya mji wa Beijing, kuna karakana moja ya kutengeneza upinde inayojulikana kwa jina la Ju Yuan Hao, ambako kuna vitu mbalimbali vya kutengenezea pinde na mishale pamoja na pinde zenye ukubwa tofauti zilizotundikwa ukutani. Mtu mmoja wa makamo mwenye ndevu alikuwa anatengeneza upinde mkubwa. Huyu ni mwenye karakana hiyo Bw. Yang Fuxi wa kabila la Wamam.
Bw. Yang alituambia kuwa, katika miaka 100 iliyopita makumi kadhaa ya karakana za kutengeneza pinde na mishale zilitapakaa katika mtaa mmoja huko Beijing, watu wa kabila la Waman walikuwa wanatembelea karakana hizo mara kwa mara na kununua vitu hivyo. Baadaye matumizi ya pinde na mishale yalipungua, kwa hiyo mbali na karakana iliyoendeshwa na familia ya Bw. Yang, karakana nyingine zaidi ya 40 zilifungwa.
Alipokuwa anasoma katika shule ya sekondari, Bw. Yang Fuxi alikuwa na ndoto ya kurithi ufundi wa familia yake. Anasema, "Nilipokuwa na umri wa miaka 14 na 15, nilifikiri kuwa mimi pia nitatengeneza pinde na mishale katika siku za baadaye."
Lakini mvulana huyo alishindwa kutimiza ndoto yake mwanzoni alipoanza kazi. Alifanya kazi katika kiwanda na halafu alikuwa dereva wa teksi. Hadi kufikia mwaka 1998, hali ya afya ya baba yake ilianza kuwa mbaya, Bw. Yang alitambua kuwa, kama asingejifunza kutoka kwa baba yake ufundi wa kutengeneza pinde wa mtindo wa kabila la Waman, labda ufundi huo utapotea. Kwa hiyo aliacha kazi ya udereva na kuanza maisha ya ufundi.
Mwanzoni, mke wake Bibi Tian Zhanhua hakufurahia uamuzi huo. Anasema,"Nilikuwa nataka asiache kazi ya udereva. Kwa vile mwanzoni alipoingia katika shughuli za pinde, mustakabali wa shughuli hizo ulikuwa si mzuri na biashara ilikuwa si nzuri, ambapo maisha ya familia yalikuwa yanategemea mshahara wangu peke yake, pia ilinibidi kulipa kodi za karakana na kununua vifaa vya kutengenezea pinde. Tulitumia akiba yote ya familia katika shughuli za kutengeneza pinde na mishale."
Lakini hatua kwa hatua Bibi Tian aliguswa na moyo wa mume wake wa kujitia katika shughuli za kutengeneza pinde na mishale, na aliamua kumsaidia kununua vifaa vya kutengenezea.
Kutokana na kufundishwa na baba yake, haikuchukua muda mrefu Bw. Yang Fuxi alifahamu ufundi wa kutengeneza pinde, na pinde zake ziliuzwa kwa bei nzuri katika masoko. Alifafanua kuwa, utengenezaji wa pinde za jadi unachukua muda mrefu sana. Inamchukua miezi minne hivi kwa kutengeneza pinde zaidi ya 10. Ndiyo maana kutoka mwaka 1998 alipoanza kujifunza ufundi huo mpaka hivi sasa, ametengeneza pinde karibu 300 tu.
Kutokana na umaalumu wa ufundi huo, pinde zake za mtindo wa kabila la Waman zinawavutia watu wengi wanaopenda pinde na mishale. Mbali na wanaohifadhi pinde, pia kuna watu ambao wanakwenda kwa Bw. Yang kujadili ufundi wa kutengeneza pinde. Watu wengi wanaopenda pinde zake wanajitetea kuwa, wanavutiwa na utamaduni wa kabila la Waman unaohifadhiwa ndani ya ufundi huo wa jadi.
Bw. Bai Kewei kutoka kabila la Wamongolia amenunua pinde kadhaa zilizotengenezwa na Bw. Yang Fuxi. Alisema pinde za mtindo wa kabila la Waman zinaonesha sifa za ukubwa na upana, pamoja na moyo wa uongozi wa kabila hilo. Watu wa makabila hayo mawili ya Waman na Wamongolia wote wanakaa katika eneo la kaskazini ya China, na wote wanajulikana kwa ustadi wa kupanda farasi na kutumia pinde na mishale. Hata hivyo mionogni mwa watu wa kabila la Wamongolia, watu wanaofahamu kutengeneza pinde na mishale wamebaki wachache sana.
"Bw. Yang amerithi ufundi wa jadi wa kutengeneza pinde za mtindo wa kabila la Waman. Naona hili ni jambo zuri kwake kurudisha ufundi huo wa jadi."
Hivi sasa watu wengi wameonesha nia ya kujifunza kwa Bw. Yang Fuxi, hata hivyo ameweka vigezo mbalimbali. Kwa maoni yake, masharti ya kwanza ni wanafunzi kutambua sifa za utamaduni na sanaa za ufundi huo, licha ya kuuchukulia kama ni njia ya kujipatia fedha.
Bw. Yang ana mtoto mmoja wa kiume, ambaye mwaka huu atashiriki kwenye mtihani wa kujiunga chuo kikuu. Kijana huyo hakueleza rasmi nia ya kumrithi baba yake ufundi huo, ambapo Bw. Yang alisema hataki kumlazimisha bali anatumai kuwa atachagua mwenyewe njia anayopenda. Hivi sasa Bw. Yang bado hajapata mwanafunzi anayefaa kumrithi ufundi wa kutengeneza pinde, lakini hana wasiwasi.
"Kwa hakika nitampata mrithi atakayefaa, nina imani kubwa. Kwa kuwa nina umri wa zaidi ya miaka 40 tu, nina wakati wa kutosha. Iwapo naona kijana fulani atakayefaa, awe anaitwa Li au anaitwa Zhang, nitamfundisha ufundi wote."
Mwaka huu ufundi wa kutengeneza pinde za jadi za mtindo wa kabila la Waman umewekwa kwenye orodha ya urithi wa kiutamaduni iliyopendekezwa na kuwasilishwa na China kwa Umoja wa Mataifa. Taasisi ya utafiti wa sanaa ya China ilimpa sifa ya mtafiti na kumpa fursa ya kuonesha ufundi wake na kumpatia hali mwafaka ya kutengeneza pinde. Bw. Yang alieleza kuwa, ataandika makala na kuweka rekodi za kunakili ufundi huo wa jadi.
Idhaa ya kiswahili 2006-03-16
|