Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-16 16:49:59    
Wahitimu wa vyuo vikuu wa China wapenda kuwa maofisa wa vijijini

cri

Awali kwa mtizamo wa Wachina, wahitimu wa vyuo vikuu na msaidizi wa mkuu wa kijiji walikuwa watu wawili wasiolingana, kwa kuwa wanafunzi wengi wa vyuo vikuu walikwepa maeneo ya vijiji, wakisema maeneo hayo yanakosa mustakabali mzuri. Lakini hatua kwa hatua mtizamo wa namna hii unabadilika.

Kijiji cha Gua Jiayu kipo milimani katika kitongoji cha mji mkuu wa China, Beijing, ambapo shughuli za utalii wa mila za jadi zimeendelezwa katika miaka ya hivi karibuni.

Tukitembelea kijijini humo, tunaona kijiji cha kisasa ambacho bado kina sura ya kale, ambapo nyumba za mbao zenye umaalumu zimejengwa kwa mpangilio, na zimewekwa mashine za kuzalisha umeme kwa nguvu za jua au kwa nguvu za upepo.

Msaidizi wa mkuu wa kijiji hicho ni kijana Hu Tianwei. Baada ya kuhitimu kutoka Chuo kikuu cha uendeshaji wa bustani cha Beijing mwaka 2005, alipata nafasi ya kuwa msaidizi wa mkuu wa kijiji. Bw. Hu alifafanua uamuzi huo, alisema wilaya ya Pinggu ambayo kijiji hicho kipo imeweka mazingira mazuri kwa wahitimu wa vyuo vikuu, lakini jambo muhimu zaidi ni kuwa, anaona anaweza kufanya kazi kubwa katika kijiji.

 "Serikali ya wilaya hiyo ina sera nzuri ya kuwavutia wahitimu wa vyuo vikuu. Kijiji cha Gua Jiayu ni kizuri katika kuendeleza shughuli za utalii. Na taaluma yangu inalingana na mahitaji ya kijiji hicho. Kutokana na hali hii, niliona ningeweza kufanya kitu fulani kijijini."

Wahitimu wa vyuo vikuu walioamua kufanya kazi vijijini kama Bw. Hu Tianwei wamekuwa wakiongezeka kila mwaka katika miaka ya hivi karibuni. Ingawa bado hakuna takwimu halisi, lakini wilaya nyingi kabisa za China zimekuwa na maofisa wenye elimu ya juu. Kwa mfano mji wa Pingdingshan ulioko katikati ya mkoa wa Henan, kuna maofisa wa vijiji zaidi ya elfu 3 wenye elimu ya vyuo vikuu, ambao wanafanya kazi wilayani na vijijini kuwasaidia wakulima kujifunza ujuzi na sayansi, kuwafundisha kushiriki kwenye sekta nyingi mbali na kulima mazao ya chakula. Hali hii inawafanya wakulima wapate mavuno makubwa zaidi na mapato mengi zaidi, pia wajenge urafiki na wahitimu wa vyuo vikuu.

Profesa Wang Dewen wa Taasisi ya sayansi ya kijamii ya China akichambua hali hii, alisema vyuo vikuu vya China vimepanua wigo wa kuwaandikisha wanafunzi katika miaka ya karibuni, na kuleta ongezeko la idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu. Lakini si rahisi kwa wahitimu hao wote kupata ajira mijini. Kwa upande mwingine, ili kujiendeleza uchumi, maeneo ya vijiji yanahitaji sana watu wenye elimu ya juu. Profesa huyo alisema,

"Katika juhudi za kuendeleza uchumi, maeneo ya vijiji pia yanahitaji kuwashirikisha watu wenye uwezo mkubwa. Katika hali hii, maeneo ya vijiji yanawapatia wahitimu wa vyuo vikuu nafasi nyingi za ajira. "

Je, wahitimu wa vyuo vikuu wanaendelea vipi vijijini?

Katika kijiji cha Gua Jiayu, mhitimu wa chuo kikuu Bw. Hu Tianwei alieleza jinsi anavyoishi na kufanya kazi kijijini. Alisema alisoma taaluma ya utalii katika chuo kikuu, na anatumia taaluma yake vizuri katika kijiji hicho kinachokuza shughuli za utalii. Mwanzoni alipoanza kufanya kazi, aliwafundisha wakulima namna ya kutumia kompyuta ili watafute habari kuhusu utalii. Pia alitengeneza tovuti ya utalii ya kijiji hicho kwenye Internet.

Jitihada za Bw. Hu zilisifiwa na viongozi na watumishi wenzake. Mkuu wa kijiji cha Gua Jiayu Bw. Zhang Zhaoqi alipomtaja kijana huyo alitabasamu. Alisema , "Yeye ni mwaminifu na anafanya kazi kwa kufuata hali halisi. Katika mradi wa kukuza shughuli za utalii, aliweza kuambatanisha nadharia aliyosoma na hali halisi ya kijiji chetu. Pia alikusanya uzoefu na kasoro. Maeneo ya vijiji yanahitaji sana wahitimu wa vyuo vikuu kama yeye, na wanavijiji wanawakaribisha sana."

Katika kijiji kingine kiitwacho Bo Litai, msaidizi wa mkuu wa kijiji Bi. Song Xiaona pia ni mhitimu wa chuo kikuu. Yeye aliwafundisha wakulima ujuzi wa kompyuta. Msichana huyo alisema amechukua uamuzi wa kufanya kazi kubwa katika maeneo ya vijiji. Hivi sasa amezoea kabisa maisha ya kijijini na anajivunia kazi yake.

 "Sasa nimeimarika sana kimawazo, na nimepata maendeleo katika uwezo. Najivunia kuangalia uzuri wa kijiji chetu. Mambo madogo madogo niliyofanya siku zote yamechangia maendeleo ya kijiji, hali ambayo inanifanya nione nimepata mafanikio. Nafurahia sana kuona wanavijiji wenzangu wanakuwa na maisha mazuri."

Uchunguzi uliofanywa hivi karibuni na Chuo kikuu cha kilimo cha China unaonesha kuwa, karibu asilimia 80 ya wahitimu wa vyuo vikuu wanaofanya kazi katika maeneo ya vijiji wanaridhika na uamuzi wao wa kwenda kufanya kazi vijijini.

Wakulima ni watu wanaonufaika zaidi na uamuzi wa wahitimu hao. Katika kijiji cha Bolitai anachofanya kazi Bi. Song Xiaona, mwanakijiji Bw. Fan Defu alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa,

"Kutokana na uungaji mkono wa Xiaona, nilibadilisha sehemu ya nyumba yangu kuwa hoteli. Hoteli hiyo ilifunguliwa mwezi Septemba mwaka jana, na imewapokea wageni wengi wa nchini na kutoka nchi za nje. Mapato yangu hakika yataongezeka kuliko mapato ya kulima mazao tu. Namshukuru sana."

Nchini China serikali nyingi za mitaa zimetoa sera nafuu za kuwavutia wahitimu wa vyuo vikuu kufanya kazi vijijini. Tukichukua mfano wa Beijing, mwaka huu itazindua mpango mmoja ukiwa na lengo la vijiji vyote karibu elfu 4 vilivyo katika vitongoji vya mji wa Beijing viwe na maofisa waliohitimu vyuo vikuu katika muda wa miaka mitatu ijayo.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-16