Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-21 16:44:36    
Barua 0319

cri

Msikilizaji wetu Dominic Nduku Muholo wa sanduku la posta 1990, Kakamega Kenya ametuletea barua akisema, kwanza anaishukuru serikali ya China kwa uhusiano mwema na wa karibu walio nao na serikali yao ya Kenya. Hii inatokana na ufadhili wao wa mara kwa mara kwa Kenya hasa msaada wa fedha waliopata ambao serikali ya Kenya imeshaugawa kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo nchini humo.

Kuhusu kuzinduliwa kwa Radio China kimataifa FM Nairobi Kenya, Bwana Muholo anasema, imeleta mwangaza mkubwa wa China barani Afrika, pia wanamshukuru mkuu wao wa idhaa ya Kiswahili wa taifa KBC kwa ziara yake nchini China na pia kwa kutembelea Radio China kimataifa, na kuleta maelewano kati ya nchi mbili China na Kenya na kuwahakikishia kwamba atashirikiana nao kufanya kazi pamoja katika kujenga kituo cha FM cha CRI huko Nairobi Kenya.

Kituo hiki cha FM cha Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya kinasifiwa sana duniani kwa kuwa ni kituo cha kwanza cha China kujengwa barani Afrika. Bwana Muholo anasema, anapendekeza kituo kingine kijengwe katika mji wa Kisumu na pia ikiwezekana kingine kijengwe katika miji ya Ehdoret na Kakamega ili kurahisisha usikivu wa matangazo ya Radio China kimataifa katika miji hiyo, kwani katika miji hiyo kuna wasikilizaji wengi, ambao wana nafasi ya kusikiliza matangazo ya Radio za kimataifa, mojawapo ikiwa Radio China kimataifa.

Anasema, muda wa matangazo kwa lugha ya Kiswahili ni muda unaofaa kwa wasikilizaji ambao walikuwa wakikosa matangazo hayo kwa sababu ya kazi na shughuli mbalimbali. Anasema, Kituo cha FM cha Radio China kimataifa Nairobi Kenya kitawafunza mengi pamoja na kituo cha CCTV cha China kitaunganisha China na dunia nzima mbali na vituo vingine vya Radio China kimataifa vitakavyojengwa baadaye barani Afrika. Kwani wataweza kupeperusha salamu zao hewani, kufahamishwa sanaa za kale za China, utamaduni wa China na vingine vingi vinavyoihusu China.

Anasema anapenda matangazo ya lugha ya Kiswahili ya kituo cha FM cha Radio China kimataifa yaongezwe muda na yawe yakianza saa za mbele ili wasikilizaji wengi wanaotoka kazini au kwenye shughuli zao mbalimbali waweze kusikiliza. Na mwisho anapongeza uchumi wa China unaoendelea kwa haraka na kushuruku tena misaada ya China kwa nchi mbalimbali barani Afrika.

Na msikilizaji wetu Robin Sirengo ambaye barua zake huhifadhiwa na Mutanda Ayub wa sanduku la posta 172, Bungoma Kenya ametuletea barua akisema, katika barua ya mwaka mpya aliyoipokea, alielewa kuwa Radio China kimataifa itafungua kituo cha FM huko Nairobi Kenya. Kwa hiyo kwa niaba ya mashabiki wote wa Bungoma, anapenda kutoa pongezi zake kwa marafiki wao wa Radio China kimataifa kwa kuchagua Kenya kujenga kituo hiki, anasema asanteni sana na anatuombea Mungu atubariki wote na kazi tunazofanya kwa ajili ya ulimwengu mzima.

Anasema maoni yake ni kuwa, mashabiki wengi wa vituo vya FM huwa ni vijana wa rika lake, na kwa kuhakikisha hawa vijana wawe mashabiki wa kituo cha FM cha CRI, anatushauri tuwe na vipindi vingi vya burudani kama vile, muziki wa kisasa wa hapo nchini Kenya, Tanzania, Uganda na kule ng'ambo kama Amerika. Anasema pia tuwe na wafanyakazi ama watangazaji kwa lugha tamu ya kuvutia, salamu pia ziwekwe ili mashabiki wajuliane hali kila siku.

Anasema inafaa tena tuwe na njia fulani ya kutangaza jina la kituo chetu, kwa mfano yeye kama shabiki wetu mpendwa tena mzalendo ana wimbo mmoja wa rap kwa lugha ya Kiswahili na wimbo wake unaisifu Radio China kimataifa. Baada ya kufunguliwa kwa kituo hicho, anaweza kupeleka wimbo huo katika studio, ili utumiwe kutangaza jina la kituo cha FM cha Radio China kimataifa.

Tunamshukuru sana kwa barua yake na mapendekezo yake, kituo chetu cha FM kimeanzishwa rasmi huko Nairobi, Kenya, kutokana na mapendekezo ya wasikilizaji wetu wengi tutaandaa vipindi vizuri siku hadi siku, ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu, na labda katika siku zijazo tunaweza kutengeneza vizuri studio yetu kamili kwenye kituo hicho, ambapo wasikilizaji wetu watapata nafasi ya kurekodiwa kwenye studio hiyo. Vilevile tumemwajiri mwandishi mmoja wa habari ambaye ni mkazi wa Nairobi anayeitwa Ali Hassan, siku hizi anatusaidia kuandaa vipindi fulani fulani. Bila shaka wasikilizaji wetu wengi hakika wameshasikia sauti ya Bwana Ali Hassan akiwahoji wasikilizaji wetu huko Nairobi Kenya.

Bw. Anari M. Albert wa S.L.P 2995 Kisii, Kenya yeye ameanza barua yake kwa kutoa shukrani kwa watangazaji wote wa CRI pamoja na wafanyakazi wa CRI kwa ushirikiano mwema kati yao na mashabiki wote wa dunia nzima wa Radio China Kimataifa na kumaliza kazi vizuri bila tatizo katika mwaka jana.

Anatoa shukurani kwa wafanyakazi na watangazaji wote wa CRI, na anasema anatoa pongezi kwa kazi zetu nzuri sana tunazowafanyia kutoka hapa Beijing China, na anatumai kuwa tutaendelea kufanya hivyo hivyo. Bw. Anari pia anatutakia kila la heri, mafanikio mema na afya bora katika mwaka huu, na vile vile anawatakia mashabiki wote wa CRI afya bora pamoja na mzee Ngoko, watoto wote wa Bw. Ngoko, marafiki zake wote, walimu wake wote, na wanafunzi wenzake wote. Anawasalimia mwalimu Omiti wa Mokwerero, mwalimu Okello wa Mkwerero, mwalimu Besty Mitema wa Mokwerero, Bw. Thomas Outivi Otuke, pamoja na msaidizi wake Bw. John Moseti.

Pia anawatakia afya bora wazazi wake Baba Joel Mgoko na Mama Binah Anari, vile vile ndugu yake mkubwa Justine Anari, ndugu yake mdogo Abner Anari, dada yake mkubwa Zipporah Anari, dada yake mdogo Zilpah Anari, binamu zake Mogire Machuki na bibi yake Rose Mogire, pamoja na watoto wa Bw. Machuki Philip Machuki. Mwishowe anawasalimia marafiki zake pamoja na Eunice, Borca, Easter, Naom, Marriam, Shem, Evans, Vicent, Idah, Evalyine, Bukepius, Jackson, Jackline, Bi. Albert, na Patroba, anawatakia mwaka huu wenye baraka na wenye mafanikio mema na wa kipekee.

Msikilizaji wetu mwingine Bw Franklin Albert wa sanduku la posta 2995 Kisii Kenya anaanza barua yake kwa salamu nyingi kutoka hapo kwao Kisii, Kenya. Na anasema hatasahau kutoa pongezi na shukrani nyingi kwa kazi zote tulizofanya kwa mwaka 2005, na kwa hivyo yeye na wasikilizaji wengine wana matumaini kuwa tutaendelea hivyo hivyo mwaka huu, kama ilivyokuwa mwaka jana.

Anasema sababu inayomfanya atoe shukrani na pongezi hizo ni kuwa vipindi vya Radio China kimataifa vinaburudisha na kuelimisha kwa vijana kama yeye. Lakini vilevile ana swali, anataka kujua ni Kwanini hatusomi barua zao na kadi za salamu ambazo wao wanatutumia hapa Radio China Kimataifa? Anatukumbusha kuwa wao wanaitegemea sana Radio China Kimataifa, kwa hiyo ni vyema kama tutaweza kusoma barua na kadi zote za salamu tunazotumiwa na wasikilizaji wetu. Anasema anatumai kuwa tutaweza kusoma ya barua zao na kadi za salamu wanazotutumia.

Anakamilisha barua yake kwa swali, anasema hapo nyuma aliwahi kutuambia kuwa Baba yake ni mchongaji hodari, vile vile alitutumia picha zake alizochora kama simba, ndovu, nyati na ndege walioko kwenye ziwa, pundamilia, milima kama Kenya, Kilimanjaro na Hongonot na wanyama wengine hawezi kuwataja wote. Anapenda kujua kama tulivutiwa na picha hizo? Na kama zilitufurahisha basi angependa tumtumie majibu kama tunazihitaji zaidi, na pia anaomba tukiweza tumtafutie soko la picha hapa Beijing.

Tunamshukuru kwa dhati msikilizaji wetu huyo Franklin Albert kwa barua yake na picha alizowahi kututumia. Kwanza tunapenda kumwambia kwamba, tumewahi kusoma barua yake iliyotaja picha zake kwenye kipindi hiki cha sanduku la barua, na barua tunazopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu, kama wameandika vizuri na hata kama ni za kawaida, lakini zina maoni na mapendekezo zote tunasoma, na kadi za salamu tunazopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu pia tunasoma siku hadi siku, msiwe na wasiwasi. Tunaona labda baadhi ya wakati tunaposoma barua au kadi za wasikilizaji fulani, wasikilizaji hao wanakuwa kazini au kutokana na sababu fulani walikosa kusikiliza barua zao au kadi zao za salamu zikisomwa.

Na kuhusu picha zake tunaona kuwa yeye anachora vizuri, lakini tunaomba yeye atuelewe, sisi ni watangazaji na watayarishaji wa vipindi vya matangazo ya Radio, hatuwezi kumsaidia kutafuta soko la kuuza picha hizo, ama siku zijazo, wakati muda wetu wa matangazo kwenye kituo cha FM utakapoongezwa tutakapokuwa na kipindi cha matangazo ya biashara, ndipo tutakapoweza kupata nafasi ya kumsaidia kutangaza habari kuhusu picha zake. Tunaomba tafadhali atuelewe.

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-21