Uchunguzi unaonesha kuwa shida ya kupata matibabu kutokana na malipo makubwa ni tatizo linalofuatiliwa sana na wananchi wa China, ambalo pia ni tatizo lililozungumzwa sana kwenye mkutano wa Baraza la Mashauriano ya Kisiasa la China unaoendelea kufanyika sasa mjini Beijing. Mjumbe wa baraza hilo Bi. Edibay aliyetoka Mkoa wa Xinjiang aliwaambia waandishi wa habari kuwa, kuhusu utatuzi wa tatizo hilo Mkoa wa Xinjiang umepata ufumbuzi fulani.
Bi. Edibay ni daktari mstaafu wa mapafu, katika muda wake wa miaka 30 ya kazi anaelewa fika kwamba tatizo la matibabu linahusiana moja kwa moja na maisha ya watu, hasa kwa watu wasiokuwa na kipato cha uhakika na kuishi kwa kutegemea dhamana ya kijamii, watu hao wana wasiwasi wa kupata ugonjwa kwa sababu ya kushindwa kulipa malipo ya matibabu. Bi. Edibay alisema, "hospitali za kuwasaidia watu maskini" zilizoanzishwa miaka ya karibuni mkoani Xinjiang, zimesaidia utatuzi wa tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.
Hospitali za kusaidia watu maskini zinatoa huduma kwa watu wasio na uwezo katika miji na vijiji na kutoa huduma za matibabu ya kimsingi. Bajeti ya hospitali hizo inatolewa na serikali. Ili kupunguza malipo ya matibabu, serikali imeweka kikomo cha malipo. Tuchukue mfano wa hospitali iliyoanzishwa tarehe mosi Agosti mwaka 2003: Malipo ya sindano, kutundikiwa maji na ukaguzi wa aina mbalimbali jumla ni nusu tu ya malipo ya hospitali ya kawaida. Malipo ya dawa ni 3% tu ya bei ya dawa zilizonunuliwa na hospitali; malipo ya kitanda cha wodi, uokoaji wa dharura, huduma za uuguzi na upasuaji ni nusu ya malipo ya hospitali ya kawaida. Kwa wastani malipo ya matibabu katika hospitali za kuwasaidia watu maskini ni yuan 40 hadi 50, na malipo ya kitanda ni yuan elfu moja na mia nane, malipo hayo ni chini sana ikilinganishwa na malipo katika hospitali za kawaida. Hivi sasa mkoani Xinjiang kumeanzishwa hospitali hizo zaidi ya 40 na zimeanzisha zahanati kwenye ngazi ya wilaya.
Bi. Edibay alieleza serikali na idara za afya zinatenga fedha kwa ajili ya majengo ya hospitali na kununua zana za matibabu. Watu wenye kipato cha chini wanaweza kunufaika na sera za fursa maalumu kwa kitambulisho cha dhamana ya jamii kilichotolewa na kamati ya sehemu ya makazi. Bi. Edibay alitoa mfano: mgonjwa wa kijiwe cha nyongo, akitibiwa katika hospitali ya ngazi ya kwanza anapaswa kulipa yuan elfu sita, lakini akitibiwa katika hospitali ya kuwasaidia watu maskini analipa yuan elfu mbili tu, na kati ya yuan elfu mbili hizo mgonjwa analipa 5% hadi 10% tu, sehemu nyingine analipiwa na idara ya mambo ya raia.
Pamoja na hayo, wagonjwa wanaolazwa hospitali wanalipiwa chakula chenye kigezo kisichopungua yuan 12 kwa siku. Bi. Edibay alisema kuanzishwa kwa hospitali hizo kumetatua tatizo la malipo makubwa linalowakumba wananchi, na ni mchango kwa ajili ya utulivu na upatanifu wa jamii mkoani Xinjiang.
Imefahamika kuwa hivi sasa hospitali hizo pia zina matatizo, moja ya matatizo hayo ni kwamba vitanda vya hospitali havijatumiwa vya kutosha, kwa sababu watu bado hawana imani na uwezo wa hospitali hizo. Ili kutatua tatizo hilo Bi. Edibay alipendekeza kuharakisha kuchanganya uwezo wa hospitali kubwa na ndogo. Alieleza hospitali kubwa zinapaswa kuanzisha zahanati zao kwenye sehemu za makazi, madaktari wa hospitali kubwa waende kufundisha katika zahanati na kushika zamu ya matibabu, kufanya hivyo kutawafahamisha raia kwamba katika zahanati za sehemu za makazi pia kuna wataalamu, wagonjwa hawatakuwa na wasiwasi wa kutibiwa huko na kwa malipo madogo.
Bi. Edibay alisema, mkoani Xinjiang kuna madaktari wengi hodari na hospitali nyingi kubwa, ambazo zinapaswa kusaidia zahanati za sehemu za makazi ili kuinua uwezo wa zahanati na kuwapa imani ya wagonjwa na zahanati hizo.
Ugonjwa wa kawaida unatibiwa katika zahanati za sehemu za makazi na ugonjwa usio wa kawaida utibiwe katika hospitali kubwa, hivyo msongamano wa wagonjwa wengi katika hospitali kubwa unaweza kupungua, malipo madogo ya matibabu yanaweza kuondoa hali ya wagonjwa maskini kujitafutia ovyo matibabu na wagonjwa hawatachelewesha matibabu kwa kuhofia malipo makubwa.
Idhaa ya Kiswahili 2006-03-22
|