Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-23 16:19:25    
Mradi wa kujenga "lambo la maji ya mama" wawanufaisha watu katika maeneo kame nchini China

cri

Ingawa upatikanaji maji safi ya kunywa na kuoga ni hali ya kawaida katika maisha ya watu wengi duniani, lakini kuna maeneo ambayo bado yanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa maji. Katika eneo lenye ukame lililoko magharibi ya China, ukosefu wa maji unaathiri vibaya afya za wakulima wa huko hususan wanawake na watoto. Mwaka 2000, mradi wa kujenga "lambo la maji ya mama" ulianza kutekelezwa katika eneo hilo. Na mpaka hivi sasa watu wapatao milioni 1 na laki 1 wamepata maji wakinufaishwa na mradi huo wa hisani, ulioanzishwa kwa ushirikiano wa Shirikisho kuu la wanawake la China na Mfuko wa maendeleo ya wanawake wa China.

Weka maji mdomoni, toa ya maji ya mdomoni weak mikononi, nawa upande wa kushoto wa uso, halafu rudia kitendo hicho na unawe upande wa kulia wa uso. Hivyo ndivyo watoto wengi hata watu wazima wanaoishi katika sehemu ya kaskazini magharibi ya China wanavyonawa nyuso zao kutokana na uhaba wa maji.

 

China ni kati ya nchi na sehemu 13 duniani zenye upungufu mkubwa wa maji kwa wastani wa watu. Na sehemu ya kaskazini magharibi ya China inakabiliwa na upungufu mkubwa zaidi wa maji. Kwa mujibu wa takwimu, kwa wastani kila mtu duniani ana mita za ujazo za maji 7,900, lakini katika eneo kame la kaskazini magharibi ya China lenye wakazi milioni 3, kiasi hicho hakizidi mita za ujazo 110.

Kijiji cha Langdonggou cha tarafa ya Wanglejing ya wilaya ya Yanchi katika mkoa unaojiendesha wa kabila la Wahui wa Ningxia, ni moja ya sehemu kame kabisa nchini China, ambapo tokea mwaka 2000 mvua imenyesha mara tano tu.

Katika kijiji hicho, msichana Li Taotao mwenye umri wa miaka 11 anasumbuliwa sana na matatizo ya maji. Bila ya maji hakuna mavuno. Kwa hiyo baba yake anapaswa kuondoka maskani kwenda kufanya kazi ya kibarua ili aweze kutunza familia. Kila siku msichana huyo akiambatana na mama yake mlemavu, wanachota maji ya chumvi kwenye kisima kilichoko mbali na kijiji, na inawabidi wachukue saa tatu kwenda na kurudi. Maji yakawa kama ni kumbukumbu zenye uchungu moyoni mwa mtoto huyo.

Alisema"Hatuna maji, hatuna maji ya kunywa, nimekata tamaa."

Mwaka 2000 Shirikisho kuu la wanawake la China na Mfuko wa maendeleo ya wanawake wa China zilishirikiana kukusanya Renminbi Yuan zaidi ya milioni 100 kutoka kwa wafadhili, na kuanza kutekeleza mradi wa kujenga "lambo la maji ya mama".

Ili kujenga lambo hilo la maji, hatua ya kwanza ni kuchimba shimo lenye ukubwa wa mita 20 hadi 30 za ujazo, halafu kujenga kwa saruji kuta zake ili kuzuia maji yasipenye ndani ya ardhi. Ardhi iliyo nje ya lambo pia hufunikwa kwa saruji na kufanya ardhi iiname kuelekea kwenye lambo, kwa hiyo maji yanamiminikia ndani ya lambo.

"Lambo la maji ya mama" hutumika kwa kukusanya maji ya mvua, na inaponyesha mvua huingia lamboni. Mlango wa lambo ni mdogo sana kwa hiyo maji yanayohifadhiwa ndani yake si rahisi kupotea kwa mjia ya mvuke. Katika maeneo yenye upungufu mkubwa wa maji, kujenga lambo la kukusanya maji ya mvua ni njia nzuri kuliko nyingine ya kupunguza tatizo la upungufu wa maji ambayo ina gharama ndogo na ufanisi mkubwa.

Lambo moja la maji lenye ukubwa wa mita 30 za ujazo linaweza kutosheleza mahitaji ya maji ya kunywa kwa watu na mifugo ya familia yenye watu kati ya watatu hadi watano. Hivi sasa mradi wa kujenga "lambo la maji ya mama" unatekelezwa katika mikoa na miji zaidi ya 10 nchini China, ambako yamejengwa malambo laki 1 ya kukusanya na kuhifadhi maji ya mvua pamoja na vifaa vidogo na vya kati zaidi ya elfu moja vya kutoa huduma ya maji.

Naibu mwenyekiti wa Shirikisho kuu la wanawake la China Bibi Mo Wenxiu alifafanua manufaa ya ujenzi wa "lambo la maji ya mama" kwa wakulima, hususan wanawake, akisema "Tulitembelea sehemu zinazotekeleza mradi huo, na tulishuhudia jinsi mradi huo unavyoboresha maisha ya wakazi na mazingira ya huko. Hapo awali watu walikuwa hawanawi nyuso zao kwa nusu mwezi, lakini sasa wanazingatia hali ya afya. Zamani magonjwa ya wanawake yaliwaathiri wanawake wengi na mazingira ya kuishi yalikuwa machafu, na sasa hayo yote yameboreshwa."

Bibi Mo Wenxiu alieleza kuwa, gharama za kujenga malambo ya maji zinachangiwa na mfuko wa hisani na serikali, ambapo wakulima wenyewe wanafanya ujenzi. Katika kijiji cha msichana Li Taotao, pesa za kujengea malambo zimepatikana na ujenzi utaanza hivi karibuni.

Kuanzia mwaka huu mradi huo wa kujenga "lambo la maji ya mama" umewekwa malengo mapya ya kuhakikisha usalama wa maji ya kunywa. Tokea mwezi Machi, operesheni ya kulinda usalama wa maji ya kunywa imeanzishwa kwa majaribio katika mikoa mitatu ya kaskazini magharibi ya China, ambapo wakulima maskini wanapewa vifaa vya kusafisha maji, na ujuzi wa usalama wa maji ya kunywa pia unaenezwa katika maeneo ya vijiji.

Ofisa wa Kituo cha udhibiti wa magonjwa cha China Bw. Tao Yong alieleza kuwa kulinda usalama wa maji ya kunywa kuna umuhimu mkubwa.

"Katika maeneo yenye watu maskini nchini China, inatokea mara kwa mara hali ambayo watu kuumwa kwa kunywa maji machafu, halafu wanakuwa maskini kutokana na magonjwa. Mfuko wa maendeleo ya wanawake wa China hautumii fedha nyingi katika kazi ya kuhakikisha usalama wa maji ya kunywa, lakini kazi hiyo inaleta ufanisi mkubwa kwa afya, uchumi na jamii katika maeneo ya vijiji."

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-23