Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-24 19:47:46    
Uhusiano kati ya China na Kenya waonesha hali nzuri ya maendeleo

cri

Mwaka 2005 ulikuwa mwaka ulioleta maendeleo mapya kwenye uhusiano wa kirafiki na ushirikiano kati ya China na Kenya. Mawasiliano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika sekta za siasa, uchumi na biashara, utamaduni, elimu, utalii na habari umetokea hali ya kustawi. Serikali mpya ya Kenya inafuata sera ya nje ya kuelekea sehemu ya mashariki, na kutilia maanani kukuza uhusiano kati yake na China.

Balozi wa China nchini Kenya Bwana Guo Chongli hivi karibuni alipotaja maendeleo ya uhusiano kati ya China na Kenya alisema, katika miaka miwili ya karibuni, uhusiano wa nchi hizo mbili umepata maendeleo makubwa, tangu rais Mwai Kibaki ashike madaraka ya nchi hiyo mwaka 2003, serikali za China na Kenya zimesaini makubaliano 12 kuhusu mambo ya uchumi, biashara, safari za ndege, utalii, afya, ukaguzi wa bidhaa wa forodhani, elimu ya mambo ya kale, na nishati. Makubaliano hayo yalikuwa yamezidi yale yaliyosainiwa kati ya nchi hizo mbili katika miaka 40 iliyopita.

Katika miaka miwili iliyopita maofisa wengi wa ngazi ya juu wa nchi hizo mbili walitembeleana, wakiwemo rais Mwai Kibaki wa Kenya, waziri wa mambo ya nje wa Kenya Bwana Chirau Ali Mwakwere, spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo na naibu waziri mkuu wa China Bwana Zeng Peiyan na wengineo. Karibu nusu ya mawaziri wa Kenya walialikwa kuitembelea China.

Balozi Guo alitaja hasa maendeleo ya uchumi na biashara kati ya China na Kenya katika miaka miwili ya karibuni. Akisema:

"Nilipokuja Kenya zaidi ya miaka miwili iliyopita, ingawa China na Kenya zilikuwa na ushirikiano katika sekta nyingi, lakini thamani ya biashara kati ya nchi hizo mbili ilikuwa dola za kimarekani milioni 180 tu kwa mwaka. Na ilipofika mwishoni mwa mwaka jana, kiasi hicho kilifikia dola za kimarekani milioni 460, kikiongezeka kwa maradufu."

Katika kipindi hicho, uwekezaji wa makampuni ya China nchini Kenya pia umeongezeka kwa haraka. Mwezi Mei mwaka jana, kampuni moja ya Beijing iliwekeza dola za kimarekani milioni 3 kuanzisha kiwanda cha kutengeneza nguzo za saruji za waya wa umeme na simu nchini Kenya, huu ni mradi mkubwa kabisa uliowekezwa na kampuni ya China nchini Kenya hadi sasa. Isitoshe, kampuni ya Huawei na kampuni ya mawasiliano ya simu ya Zhongxing ya China kwa nyakati tofauti zilipata mikataba ya kushirikiana na upande wa Kenya katika ujenzi wa mtandao wa mawasiliano ya simu ya vijijini na kote nchini Kenya.

Katika sekta za utalii na elimu, nchi hizo mbili pia zimepata maendeleo makubwa katika miaka miwili ya hivi karibuni. Mwezi Desemba mwaka 2004, makubaliano ya ushirikiano wa utalii wa pande mbili kati ya China na Kenya yalianza kutekelezwa rasmi, Kenya ilikuwa nchi inayoweza kuwapokea watalii kutoka China. Kuanzia hapo idadi ya watalii wa China waliokwenda kutalii nchini Kenya imeongezeka kwa haraka. Jambo hili si kama tu limezidisha ufahamu wa watu wa China kuhusu mambo ya Kenya, bali pia limehimiza kustawi kwa utalii wa Kenya na uchumi wake kwa ujumla.

Licha ya kuwa na kituo cha kufundisha lugha ya Kichina katika chuo kikuu cha Egaton cha Kenya, chuo cha Confucius cha chuo kikuu cha Nairobi kilianzishwa mwezi Septemba mwaka jana.

Mwelekeo mzuri wa uhusiano kati ya China na Kenya umeweka mazingira mazuri kwa ushirikiano wa nchi hizo mbili katika sekta mbalimbali. Radio China Kimataifa imetoa mchango mkubwa katika kuzidisha maelewano na urafiki kati ya watu wa nchi hizo mbili. Kama Balozi Guo Chongli alivyosema, kuzinduliwa kwa kituo cha FM cha Radio China Kimataifa Nairobi Kenya kumewafungulia dirisha watu wa Kenya kuifahamu China.

Waziri wa habari wa Kenya Bwana Mutahi Kagwe muda si mrefu uliopita alipokutana na mkurugenzi mkuu wa Radio China Kimataifa Bwana Wang Gengnian alipongeza sana uhusiano kati ya China na Kenya. Akisema:

"Tunafurahia uhusiano kati ya Kenya na China, huu ni uhusiano wa kunufaishana. Wizara ya habari ya Kenya inaridhishwa sana na ushirikiano kati yetu na upande wa China, hasa tunafurahia kuzinduliwa kwa kituo cha FM cha Radio China Kimataifa nchini Kenya."

Bw. Kagwe alisema, serikali ya Kenya inatilia maanani uhusiano kati yake na China, wakati wizara ya habari ya Kenya ilipopokea ombi la China la kuanzisha kituo cha FM nchini Kenya, kwa kweli mitabendi za FM zilikuwa tayari zimekwisha, ni kampuni ya utangazaji ya Kenya ilikubali kuipa Radio China Kimataifa mitabendi yake. Kwa sababu uhusiano kati ya Kenya na China ni uhusiano wa kunufaishana wa muda mrefu.

Bw. Kagwe alisema tarehe 23 mwezi Januari mwaka 2006, China na Kenya zilisaini makubaliano mawili kuhusu China kuipa Kenya mikopo nafuu kwa mradi wa kujenga mtandao wa mawasiliano ya simu wa vijijini, na mradi wa kuboresha mfumo wa kusambaza umeme wa Kenya. Alisema miradi hiyo miwili bila shaka itahimiza ongezeko la uchumi wa Kenya na maendeleo yake ya kijamii kutoka pande zote.

Bw. Kagwe alisema kwa kichekesho:

"Hivi sasa shughuli za biashara na utalii ni shughuli zinazoendelezwa kwa haraka zaidi kati ya nchi zetu mbili. Tunatumai kuiuzia China chai na kahawa kwa wingi zaidi. Ikiwa kila mchina atakunywa kikombe kimoja cha kahawa ya Kenya, basi kahawa inayozalishwa nchini Kenya itakuwa na soko kubwa la kutosha."

Serikali ya China pia inatilia maanani kukuza uhusiano wa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati yake na Kenya, kuyahimiza makampuni yenye nguvu kuwekeza nchini Kenya. Imefahamika kuwa, kuanzia tarehe 3 hadi 18 mwezi huu, shirikisho la wafanyabiashara wa China na Afrika lilituma ujumbe nchini Kenya kutafuta miradi ya uwekezaji. Na idara ya kuhimiza uwekezaji ya Kenya ilikuwa imeandaa kongamano la miradi ya uwekezaji ili kuwasaidia watu wa ujumbe huo wa China kutafuta miradi mwafaka ya kuwekeza.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-24