Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-27 15:07:06    
Kazi ya kuhifadhi vitu vya kale nchini China imepata mafanikio makubwa

cri

Siku chache zilizopita, serikali ya China ilitangaza kuwa kuanzia mwaka huu, kila J'mosi ya pili katika mwezi wa Juni ni "Siku ya Urithi wa Utamaduni" nchini China. Naibu mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Vitu vya Kale Bw. Zhang Bai alisema, kazi ya kuhifadhi vitu vya kale ni jukumu la wananchi wote. Kutokana na maendeleo ya uchumi na ujenzi wa miundombinu kote nchini China, shughuli za kuchimbua vitu vya kale zimekuwa nyingi, na mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na msaada wa serikali. Alisema, "Hivi sasa kuna shughuli nyingi za kuhifadhi vitu vya kale nchini China, hasa katika eneo la mradi mkubwa wa Magenge Matatu ya Mto Changjiang na mradi wa kupeleka maji kutoka kusini hadi kaskazini mwa China, shughuli hizo zinaendelea bila matatizo kutokana na uungaji mkono wa sehemu mbalimbali kote nchini, na uwezo wa taifa wa kiuchumi unasaidia sana shughuli hizo katika sehemu mbalimbali nchini China."

Mradi wa kupeleka maji kutoka kusini hadi kaskazini mwa China ni mradi kabambe ambao lengo lake ni kupeleka maji kutoka sehemu ya kusini ya China penye maji mengi hadi kaskazini mwa China kwa kuchimba mifereji. Kwa sababu maeneo amabyo mifereji ya maji itapita ni chanzo cha utamaduni wa kale, chini ya ardhi yake kuna vitu vingi vya kale, serikali ya China imetenga fedha nyingi kwa ajili ya shughuli za kuhifadhi vitu vya kale vya sehemu hiyo.

Kumbukumbu za Idara ya Vitu vya Kale ya China zinaonesha kuwa, kila mwaka shughuli za kuchimbua vitu vya kale chini ya ardhi zinafikia aina zaidi ya mia tano, shughuli hizo zimeleta vitu vingi kwa ajili ya kusaidia utafiti wa utamaduni wa kale wa China, na pia zimeharakisha maendeleo ya makumbusho. Mwezi Oktoba mwaka 2005 bodi ya kimataifa ya wakurugenzi ya vitu vya kale ilifanya mkutano mjini Xi'an kwa lengo la kutafuta njia mpya ya kuhifadhi vitu vya kale na ilitoa "taarifa ya Xi'an" kuhusu uhusiano kati ya hifadhi bora ya vitu vya kale na mazingira. Bw. Zhang Bai anaona kwamba mkutano huo ni mchango wa kuendeleza juhudi za kuhifadhi vitu vya kale duniani kwa njia ya kisayansi. Alisema "Wajumbe kutoka nchi na sehemu zaidi ya mia moja walihudhuria mkutano huo, washiriki walijadiliana kwa kina umuhimu wa kuhakikisha mazingira bora kwenye maeneo yenye vitu vya kale. Huu ni mchango kwa ajili ya hifadhi ya vitu vya kale duniani."

Kutumia sayansi na teknolojia katika hifadhi ya vitu vya kale limekuwa jambo linalozingatiwa zaidi katika miaka ya karibuni nchini China. Mathalan, sanamu za askari na farasi zilizofukuliwa kutoka kaburi la mfalme Qin Shiyuang, zikikutana na hewa mara zitabadilika rangi, lakini kutokana na ushirikiano na wataalamu wa hifadhi wa vitu vya kale waliotoka Ujerumani, tatizo hilo lilitatuliwa. Bw. Zhang Bai alisema "Matumizi ya sayansi na teknolojia katika hifadhi ya vitu vya kale yamepiga hatua kubwa nchini China, hivi sasa vituo sita vya sayansi na teknolojia kwa ajili ya hifadhi hiyo vimeanzishwa, vifaa vimeongezeka na fedha zaidi zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo."

Kutokana na kuwa China ni nchi kubwa, sehemu tofauti zinatofautiana kwa wingi wa vitu vya kale vilivyokuwa chini ya ardhi. Mikoa ya Henan na Shaanxi iko katika sehemu ya katikati ya China, sehemu hiyo inajulikana kwa kuwa na makaburi mengi ya kale na magofu ya kasri la kifalme. Katika mkoa mwingine na Shan'xi ambao pia uko katika sehemu ya katikati ya China, majengo yaliyokuwepo kwa miaka zaidi ya elfu moja juu ya ardhi yanachukua asilimia 70 ya majengo yote kama hayo nchini China. Miundo ya majengo hayo yote ni ya mbao ambayo inahitaji kuhifadhiwa kwa makini. Mjini Beijing kuna sehemu moja ya tano ya urithi wa kale wa China nzima. Kutokana na hali hiyo tofauti kwa kila sehemu, serikali za mitaa zimetoa sera tofauti. Kwa mfano, kutokana na ujenzi wa sasa wa mji wa Beijing ambao unafuatiliwa sana kimataifa serikali ya Beijing imetoa sheria kuhusu ujenzi wake. Mkuu wa Idara ya Vitu vya Kale ya Beijing Bw. Mei Ninghua alisema "Sheria zilizopitishwa na bunge la umma la Beijing ni muhimu sana kwa ajili ya kuhifadhi mitaa ya kale mjini Beijing na mandhari yake ya kihistoria, hii inamaanisha kuwa hifadhi ya mji wa zamani wa Beijing inalindwa kisheria. Hivi sasa tunafanya utafiti na uchunguzi ili kutunga sheria kwa ajili ya hifadhi ya kasri la kifalme mjini Beijing."

Baadhi ya watu wanasema, kama yasingepatikana maendeleo ya haraka ya ujenzi nchini China shughuli za kuhifadhi ya vitu vya kale zisingekuwa nyingi. Ni sawa kusema hivyo, kwa sababu bila mahitaji ya ujenzi wa kisasa, vitu vingi vya kale visingefukuliwa kwa lazima. Lakini kwa upande mwingine, maendeleo hayo ya uchumi ndio yametuwezesha kifedha kuhifadhi vitu hivyo na visiharibiwe katika kipindi chetu cha mabadiliko ya kihistoria.

Idhaa ya kiswahili 2006-03-27