Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2006-03-29 19:57:43    
Tushirikiane kuhifadhi kwa pamoja maliasili ya maji duniani

cri
Mkutano wa 4 unaohusu mambo ya Baraza la maji duniani unaoendeshwa kwa pamoja na Baraza la maji duniani na Serikali ya Mexico unafanyika nchini Mexico. Wajumbe zaidi ya elfu 11 kutoka nchi na sehemu zaidi ya 100 wanajadili kwa kina kuhusu namna kuhifadhi, kuendeleza, kusimamia, kutumia na kubana matumizi ya maliasili ya maji.

"Tunahifadhi maliasili ya maji kwa ajili ya Costa Rica, Colombia, Chile, Canada? Mimi ni Dalepa, natoka Bangladesh, tunahifadhi maliasili ya maji kwa ajili ya Bangladesh, Marekani, Umoja wa Mataifa?."

Maneno hayo yanasemwa na watoto kutoka nchi mbalimbali wanaoshiriki kwenye Mkutano wa pili wa watoto uliohusu mambo ya maji duniani. Maji msingi wa uhai, bila maji watu wanakufa. Lakini hivi sasa duniani watu bilioni 1.3 ambao ni moja ya tano ya watu wote duniani wanakosa maji salama ya kunywa, na asilimia 40 ya watu wanakosa zana za kimsingi za afya. Mwenyekiti wa baraza la maji duniani Bw. Loic Fauchon anaona kuwa, hivi sasa hali ya upatikanaji wa maji duniani ni mbaya sana, anasema:

"Leo tunajadili suala la maji ambalo linawatia watu wasiwasi, na linaweza kusababisha migogoro. Hivi sasa hali ya maji iko hatarini, na binadamu wanakabiliwa na hatari kubwa. Watu waliokufa mwaka jana kutokana na ukosefu na uchafuzi wa maji, ni mara 10 ya waliokufa kutokana na vita. Aidha kila asubuhi mamilioni ya wanawake na watoto wanateka maji kiasi kidogo tu yasiyo safi kwa kusafiri kwa miguu kwa masaa kadhaa."

Jumuiya ya kimataifa imefanya juhudi kubwa ili kutatua suala la upungufu wa maji. Kwa mujibu wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya Umoja wa Mataifa yaliyopitishwa kwenye Mkutano wa viongozi wa Milenia wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwaka 2000 huko New York, idadi ya watu wanaokosa maji salama ya kunywa inapaswa kupungua kwa nusu kabla ya mwaka 2015; kutokana na Mipango ya utekelezaji iliyopitishwa kwenye Mkutano wa viongozi wa dunia kuhusu maendeleo endelevu uliofanyika mwaka 2002 huko Johannesburg, Afrika ya Kusini, idadi ya watu wasioweza kupata uhakikisho wa kimsingi wa afya, inapaswa kupungua kwa nusu. Aidha kuanzia mwaka 2005 hadi 2015, imewekwa kuwa ni miaka 10 ya utekelezaji mpango wa "Maji ya Uhai" wa Umoja wa Mataifa. Rais Vicente Fox wa Mexico alisema, serikali zote zinapaswa kutatua suala la maji kwa hatua zenye ufanisi.

"Upatikanaji wa maji ni haki isiyonyimiki ya kimsingi kabisa ya watu. Hivi sasa wajumbe wa mashirika ya kimataifa, wataalamu na wajumbe wa nchi mbalimbali wanaoshughulikia mambo ya maji wanapaswa kutafuta utaratibu wenye ufanisi wa ushirikiano na uratibu, ili kutatua suala hilo linaloikabili dunia nzima."

Kwenye mkutano huo, vijana wengi kutoka nchi mbalimbali pia walishiriki kwenye shughuli za Baraza la Vijana, na mwanafunzi wa mwaka wa pili kutoka Chuo kikuu cha Beijing anayesomea kozi ya sayansi ya mazingira Bi Zhang Xin ni mwakilishi wa vijana hao. Msichana huyo anayedhamiria kutoa mchango wake kwa ajili ya hifadhi ya mazingira, anatoa maoni yake kuhusu namna vijana wanavyoshiriki kwenye shughuli za hifadhi ya mazingira.

"Hivi sasa tunaandaa baraza ili kuyashirikisha mashirika ya vijana ya nchi mbalimbali, hususan mashirika yanayohusika na mazingira ya maji, ili kupata habari kuhusu hali ya mazingira ya nchi mbalimbali, mipango ya mashirika hayo, pamoja na matumaini ya mashirika hayo. Tutakusanya habari hizo, ili kuwawezesha watu wa sehemu mbalimbali wawasiliane, na kutoa mchango kwa maendeleo ya Mashirika ya Vijana ya Hifadhi ya Mazingira."

Maji ni maliasili muhimu kwa binadamu, na hifadhi ya maji ni wajibu wa watu wote duniani. Ryan Hreljac mwenye umri wa miaka 14 kutoka Canada anasisitiza kuwa watu wote wanapaswa kufanya juhudi ili kutatua tatizo la maji. Mwaka 1998, alipokuwa na umri wa miaka 6, alisikia kwa mara ya kwanza kuwa, watu wengi barani Afrika wanapaswa kupata maji baada ya kusafiri muda na mrefu kila siku. Na alitoa msaada kujenga visima 77 kwa Uganda, Zimbabwe na Ethiopia kutokana na msaada wa wazazi wake. Mwezi Machi, mwaka 2001 Mfuko wa fedha wa visima wa Ryan ulianzishwa. Hivi sasa mfuko huo umepata mamilioni ya dola za kimarekani, na kuzisaidia nchi za Afrika kujenga visima zaidi ya 200. Bw. Ryan anasema:

"Watu wengi wanasema tu wanapaswa kufanya nini, lakini n wachache wanaochukua kitendo. Watu wengi wanakufa kutokana na kukosa maji salama, hali ambayo haipaswi kutokea, nataka kubadilisha hali hiyo, na watu wote wanawajibika kufikiria namna ya kuifanya dunia hii iwe nzuri zaidi hata akiwa na umri wa miaka mingapi."

Idhaa ya Kiswahili 2006-03-29